Na Emmanuel Charles

- Wizara ya Kilimo itahamasisha uzalishaji wa zao la zabibu kutoka tani 16,138.8 mwaka 2018/2019 hadi tani 17,430 mwaka 2022/2023 kwa kuongeza eneo la uzalishaji kutoka hekta 3,426 hadi hekta 3,700. Vilevile, itaendelea kuhamasisha ufufuaji wa mashamba ya Mradi wa Umwagiliaji wa Zabibu Chinangali II, Gawaye, Hombolo na Dabalo pamoja na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya zabibu.
- Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo Nchini Mhe. Hussein Bashe wakati Akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
Amesema Wizara itahamasisha uwekezaji wa viwanda vidogo vya kusindika zabibu na kuongeza uzalishaji na tija kutoka tani 6.25 kwa hekta hadi kufikia tani 10 kwa hekta kwa kuimarisha huduma za ugani na kuimarisha uwezo wa TARI-Makutupora kuongeza uzalishaji wa miche kutoka 120,685 hadi 2,000,000 kwa msimu.
- Aidha, katika kuongeza thamani, kipato kwa mkulima na kupunguza upotevu wa zao la zabibu, Wizara itanunua mashine tatu (3) za kusindika zabibu ghafi ambapo mashine hizo zitasimikwa katika mkoa wa Dodoma.
- “katika mwaka 2022/2023, Wizara kupitia TARI itakamilisha tathmini ya kubaini utofauti, usawa na uthabiti kwa aina tano (5) za mbegu bora za mizabibu ambapo TARI kwa kushirikiana na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) watahitimisha utambuzi wa muda wa kuchipua (sprouting time) na muda wa kutoa maua (time of flowering) kwa aina hizo tano za mbegu. Pia, Wizara kupitia TARI itaendesha mafunzo ya kanuni bora za kilimo cha zabibu kwa wakulima 2,000 na maafisa ugani 50 katika wilaya zote za Mkoa wa Dodoma.”
Ameendelea kueleza kuwa Wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaimarisha maendeleo ya ushirika katika tasnia ya zabibu kwa kuongeza idadi na Thamani ya Hisa za Wanachama angalau kwa asilimia 25. Pia, Wizara itahamasisha uanzishwaji wa mashamba ya pamoja (block farming) ya zabibu ili kurahisisha utoaji wa huduma za ugani. Vilevile, Wizara itaweka mazingira bora ya uwekezaji katika tasnia ya zabibu na kuhimiza kilimo cha mkataba ili kumhakikishia mkulima soko la uhakika.
