Na Emmanuel Charles

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Sekta Binafsi imesema itaendelea kuhamasisha wadau kuongeza uzalishaji wa zao la parachichi kutoka tani 190,000 mwaka 2018 hadi kufikia tani 215,000 mwaka 2022/2023.
Akiwasilisha Bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo leo Mei 17, 2022 Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema Lengo hilo litafikiwa kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo kwenye mashamba ya uzalishaji wa zao la parachichi, udhibiti wa visumbufu na kuimarisha huduma za ugani kwenye mashamba ya parachichi ya takriban hekta 46,002.
Aidha, Wizara itawatambua na kuwasajili wazalishaji wa miche ya parachichi. Vilevile, Wizara itaendelea kushirikiana na TAHA na wadau wengine wa zao la parachichi katika utafiti, upatikanaji wa takwimu na kutafuta masoko ya mazao ya bustani. Pia, Wizara itaiwezesha TARI kupitia Vituo vya TARI Uyole na TARI Tengeru kuzalisha wa miche 20,000,000 zitakazotosheleza eneo la hekta 114,285.72. Miche hiyo itasambazwa kwa wakulima kwa bei ya ruzuku isiyozidi Shilingi 2,000 kwa mche.
Kwa Upande mwingine amezungumzia Zao la Vitunguu ambapo amesema Wizara imepanga kuongeza uzalishaji wa zao la vitunguu kutoka tani 270,800 mwaka 2018/2019 hadi tani 320,640 mwaka 2022/2023. Ili kufikia lengo hilo,
“Wizara itawezesha ujenzi wa mabwawa ya kimkakati katika miradi ya umwagiliaji ya Mboli (hekta 500), Idodoma (hekta 800), Kisese (hekta 2,000), Msingi (hekta 1,200), Mughamo (1,200), Skimu za bonde la Eyasi (hekta 5,291), Tumati (hekta 270), Mongahay (hekta 300) na Tlawi (hekta 300). Pia, itajenga ghala 16 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 144,000 na kusimikwa mashine 16 za kuratibu kiwango cha unyevu katika maeneo ya uzalishaji.”
