MAELEKEZO YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS – TAMISEMI, MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA (MB) KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI WA HESABU ZA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA KWA MWAKA WA FEDHA 2020/21

Ndugu Wanahabari,

Mtakumbuka kuwa taarifa za CAG kuhusu ukaguzi wa hesabu za Mwaka wa Fedha 2020/21 ziliwasilishwa Bungeni Jumanne tarehe 12/04/2022. Baada ya taarifa kuwasilishwa Bungeni, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imechambua taarifa za ukaguzi wa hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuandaa mpango wa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na CAG.

Lengo la kukutana nanyi ni kuwataarifu kwa muhtasari baadhi ya hoja zilizojitokeza kwenye taarifa hiyo na hatua ambazo Serikali imezichukua/inazichukua kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na CAG katika taarifa ya hesabu za Mwaka wa Fedha 2020/21 na mwaka uliotangulia wa 2019/20.

1       Hatua Zilizochukuliwa Kutekeleza Taarifa ya CAG ya Mwaka wa Fedha 2019/20

Ndugu Wanahabari,

Kabla ya kuzungumzia taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2020/21, ni muhimu nikaeleza kwa kifupi hatua ambazo Serikali ilizichukua katika kuhakikisha taarifa ya CAG ya hesabu za mwaka uliotangulia wa 2019/20 inatekelezwa;

 1. Mwezi Septemba 2021, Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliendesha kikao kazi cha wadau wa ukaguzi kujadili matokeo ya ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2019/20 na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizosababisha matokeo yasiyoridhisha ya ukaguzi huo. Wadau walioshiriki kikao hicho walikuwa ni CAG, Wizara ya Fedha na Mipango, TAKUKURU, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, baadhi ya Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waweka Hazina na Wakaguzi wa Ndani;
 2. Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliwaelekeza Wakuu wa Mikoa yote kushiriki kikamilifu vikao maalum vya Mabaraza ya Madiwani kwenye Halmashauri zote kujadili taarifa ya CAG na kutoa maelekezo ya kiutekelezaji. Wakuu wa Mikoa wote walishiriki vikao hivyo;
 3. Watumishi 525 ambao walisababisha hoja za ukaguzi zisizo za lazima au hasara kwa Halmashauri walichukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu/kisheria. Watumishi 206 walipewa onyo, Watumishi 27 walifukuzwa kazi, watumishi wawili (2) walivuliwa madaraka, watumishi 31 walisimamishwa kazi, watumishi 221 walifikishwa Polisi/TAKUKURU (uchunguzi unaendelea) na watumishi 38 walifikishwa Mahakamani ambapo watatu (3) walifungwa jela na wengine kesi zinaendelea. Aidha, Wahasibu 20 waliosaini taarifa za fedha zisizo sahihi walifikishwa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi kwa hatua zaidi;
 4. Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilichambua taarifa za ukaguzi maalum uliofanywa na CAG kwenye Halmashauri 64 na kuzielekeza Ofisi za Wakuu wa Mikoa kusimamia uchukuaji wa hatua stahiki za kinidhamu kwa watumishi zaidi ya 1,000 waliotajwa kuhusika na kasoro mbalimbali. Aidha, TAKUKURU imeombwa kuzifanyia kazi taarifa hizo kwenye maeneo yanayohusu ubadhirifu wa fedha na mali za Halmashauri. Vile vile, Ofisi ya Rais – TAMISEMI inakamilisha uchambuzi wa Wakandarasi na Wahandisi Washauri wote waliotajwa kwenye taarifa hizo ili wafikishwe kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kwa hatua stahiki kufuatia ukiukaji wa maadili ya taaluma zao;
 5. Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango imewezesha Halmashauri zote kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ulipaji Serikalini (MUSE) kuanzia tarehe 1 Julai, 2021. Mfumo huu umeboreshwa zaidi na hivyo utapunguza changamoto za uandaaji wa taarifa za fedha zenye makosa tofauti na ilivyokuwa hapo awali wakati wa matumizi ya mfumo wa EPICOR.

2       Matokeo ya Ukaguzi wa Hesabu za Mwaka wa Fedha 2020/21 na Utekelezaji Wake

Ndugu Wanahabari,

Sasa nizungumzie matokeo ya ukaguzi wa hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 na hatua ambazo Serikali inazichukua:

2.1    Hati za Ukaguzi Zilizotolewa

Taarifa ya ukaguzi ya CAG kuhusu hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 imebainisha kwamba Halmashauri 178 sawa na asilimia 96 zimepata Hati Zinazoridhisha (Hati Safi), Halmashauri 6 sawa na asilimia 3 zimepata Hati Zenye Shaka na Halmashauri 1 sawa na asilimia 1 imepata Hati Mbaya (Hati Chafu).

Kwa ujumla, kwa mwaka wa fedha 2020/21, Halmashauri zimefanya vizuri zaidi ikilinganishwa na matokeo ya ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2019/20 ambapo Halmashauri 124 sawa na asilimia 67 zilipata Hati Zinazoridhisha, Halmashauri 53 sawa na asilimia 29 zilipata Hati Zenye Shaka na Halmashauri 8 sawa na asilimia 4 zilipata Hati Mbaya.

Mlinganisho wa Hati za Ukaguzi kwa Miaka Miwili Inayofuatana

MwakaHati ZinazoridhishaHati Zenye ShakaHati MbayaJumla
2020/21178 (96%)6 (3%)1 (1%)185 (100%)
2019/20124 (67%)53 (29%)(4%)185(100%)

 

2.2    Halmashauri Zilizopata Hati Mbaya na Hati Zenye Shaka

Ndugu Wanahabari,

Halmashauri moja iliyopata Hati Mbaya ni Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, wakati Halmashauri sita (6) zilizopata Hati Zenye Shaka ni Halmashauri za Wilaya za Sengerema, Kisarawe, Longido, Mlele, Musoma na iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Ofisi ya Rais – TAMISEMI imechukua hatua kwa Waweka Hazina wa Halmashauri hizo kwa kuwabadilishia majukumu.

Kati ya Halmashauri saba (7) zilizopata Hati Mbaya na Hati Zenye Shaka, Halmashauri mbili (2) zipo katika Mkoa wa Mara, wakati Halmashauri nyingine zipo katika Mikoa ya Katavi, Pwani, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam. Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imekuwa na mwenendo usioridhisha kwa miaka miwili mfululizo, mwaka 2019/20 na 2020/21, imepata Hati Zenye Shaka.

Mikoa mingi imefanya vizuri, lakini kipekee ninawapongeza sana Wakuu wa Mikoa minne (4) ya Rukwa, Njombe, Morogoro na Mtwara kwa kuwa Halmashauri zote katika Mikoa hii zimepata Hati Zinazoridhisha (Hati Safi) kwa mwaka wa pili mfululizo.

2.3    Chimbuko la Hoja za Ukaguzi Zilizobainishwa Kwenye Taarifa ya CAG kwa Mwaka wa Fedha 2020/21

Ndugu Wanahabari,

Taarifa Kuu ya CAG kuhusu hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2020/21 imebainisha hoja za ukaguzi takribani 103. Uchambuzi umeonesha kuwa hoja hizo zimegawanyika katika makundi makuu mawili kama ifuatavyo:

 1. Hoja za kimfumo/kisera ambazo utekelezaji wake upo nje ya uwezo wa Halmashauri husika, zinahitaji utekelezaji wa Serikali Kuu. Kundi hili lina jumla ya hoja 31 sawa na asilimia 30 ya hoja zote 103;
 2. Hoja ambazo zimetokana na Wataalam wa Halmashauri kutotekeleza ipasavyo majukumu yao, hoja ambazo utekelezaji wake umo ndani ya uwezo wa Halmashauri husika. Kundi hili lina jumla ya hoja 72 sawa na asilimia 70 ya hoja zote 103.

Kwa kuzingatia mgawanyo huo, ni wazi kwamba ikiwa Wataalam wa Halmashauri watatekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo, hoja za ukaguzi zitapungua kwa kiasi kikubwa katika kaguzi zitakazofuata.

2.4    Baadhi ya Hoja za Ukaguzi Zilizobainishwa kwenye Taarifa ya CAG na Ufafanuzi Wake

Ndugu Wanahabari,

Taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2020/21 imebainisha hoja na mapendekezo mbalimbali yanayopaswa kufanyiwa kazi na Serikali. Baadhi ya hoja hizo pamoja na ufafanuzi wa hatua zilizochukuliwa au zinazochukuliwa na Serikali ni kama ifuatavyo:

 1. Hoja: Utekelezaji usioridhisha wa mapendekezo ya ukaguzi yaliyotolewa mwaka 2019/20 ambapo kati ya mapendekezo yote 10,824; mapendekezo 1,864 sawa na asilimia 17 hayajatekelezwa.

Ufafanuzi: Mwezi Januari 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliidhinisha muundo mpya wa Sekretarieti za Mikoa. Miongoni mwa maboresho yaliyofanyika kupitia muundo huo, ni kuanzishwa kwa Seksheni ya Menejimenti, Ufuatiliaji na Ukaguzi ambayo pamoja na majukumu mengine, itakuwa na jukumu la kufuatilia kwenye Halmashauri utekelezaji wa mapendekezo ya CAG na maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC). Vile vile, Serikali imeongeza bajeti ya matumizi mengineyo ya Ofisi za Wakuu wa Mikoa kutoka Shilingi billion 57.44 hadi Shilingi bilioni 79.09 na Ofisi za Wakuu wa Wilaya kutoka Shilingi bilioni 17.13 hadi Shilingi 26.68 sawa na ongezeko la Shilingi bilioni 9.55 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hizo, ikiwemo ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za Halmashauri.

 1. Hoja: Madiwani kushiriki katika shughuli za kiutendaji ambazo zilitakiwa zitekelezwe na menejimenti, hivyo kuathiri dhana ya utawala bora. Shughuli hizo ni pamoja na zifuatazo;
 2. Mwenyekiti/Meya wa Halmashauri kusaini mikataba kati ya Halmashauri na wazabuni/mawakala wa ukusanyaji wa mapato, taarifa za mwaka za hesabu na hati za makabidhiano ya ofisi baina ya Wakurugenzi,
 3. Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani kuwa na wajibu wa kujadili majibu ya taarifa za ukaguzi kabla ya kuyawasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,
 4. Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani kuidhinisha mali zote ambazo Halmashauri zimeamua kuacha kuzitumia na
 5. Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani kuwa na mamlaka ya nidhamu ya watumishi wa Halmashauri.

         Ufafanuzi: Shughuli zilizobainishwa na CAG zinatekelezwa na Mabaraza ya Madiwani kwa mujibu wa Sheria. Hivyo, Ofisi ya Rais – TAMISEMI itafanya uchambuzi husika ili kuona namna bora ya kutekeleza mapendekezo ya CAG bila kuathiri dhana nzima ya ugatuaji madaraka kwa Umma.

 1. Hoja: Mapungufu katika utendaji wa Vitengo vya Ukaguzi wa Ndani

Ufafanuzi; Kati ya mwezi Machi na Mei 2021, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilitoa mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Malipo Serikalini (MUSE) kwa Wakaguzi wa Ndani wa Halmashauri zote 184 na Wakaguzi wa Ndani wa Mikoa yote 26 Tanzania Bara. Mfumo huu ulioboreshwa, ulianza kutumika kwenye Halmashauri zote 184 kuanzia Julai 2021. Serikali itaendelelea kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani ili waweze kutekeleza majumu yao kwa ufanisi zaidi.

Kuhusu upungufu wa Wakaguzi wa Ndani, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imewasiliana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuomba kibali maalum cha ajira kwa kada mbalimbali za Watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wakiwemo Wakaguzi wa Ndani.

 1. Hoja; Mapungufu katika udhibiti wa mashine za POS

Ufafanuzi; katika kuimarisha usalama na udhibiti wa miamala katika mfumo wa mapato na mashine za kukusanyia mapato (PoS), Ofisi ya Rais – TAMISEMI ipo katika ukamilishaji wa maandalizi ya mfumo mpya wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato ya ndani (TAUSI). Lengo ni kuongeza udhibiti na ufanisi kwa kurekebisha dosari zote zilizobainika katika toleo la awali la mfumo wa kielekroniki wa LGRCIS. Aidha, mfumo wa mashine za kukusanyia mapato (PoS) umeboreshwa pamoja na mambo mengine, imeondoa changamoto ya kukusanya mapato wakati mashine hizo zikiwa nje ya mtandao kwa muda mrefu. Kwa sasa mashine hizo zinaruhusiwa kukusanya zikiwa nje ya mtandao kwa muda usiozidi masaa 24.

 • Hoja: Uandaaji wa taarifa za fedha zenye makosa na marekebisho mengi

Ufafanuzi: Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya uandaaji wa taarifa za fedha ili kuwa na taarifa zilizo sahihi. Kutokana na juhudi hizo, kiasi cha makosa kwenye taarifa za fedha kimepungua kwa kiasi kikubwa kama inavyothibitishwa na kupungua kwa idadi ya Halmashauri zilizopata Hati Zenye Shaka na Hati Mbaya kutoka Halmashauri 61 sawa na asilimia 33 mwaka 2019/20 hadi Halmashauri 7 sawa na asilimia 4 mwaka 2020/21. Serikali itaendelea kufanyia kazi mapendekezo ya CAG ili kuhakikisha kuwa Halmashauri zinaandaa taarifa za fedha zilizo sahihi.

 • Hoja; Halmashauri zilipokea kiasi pungufu cha ruzuku ya matumizi ya kawaida, Shilingi Trilioni 4.48 sawa na asilimia 89 ya bajeti ya Shilingi Trilioni 5.06 ikimaanisha kuwa Shilingi Bilioni 573.51 hazikupokelewa. Vile vile, Halmashauri zilipokea Shilingi bilioni 662.70 za ruzuku ya miradi ya maendeleo ikiwa ni asilimia 71 ya makadirio yaliyoidhinishwa

Ufafanuzi; Serikali imeendelea kuimarisha mifumo yake ya ukusanyaji wa mapato ya ndani. Juhudi hizo zimewezesha Serikali kupunguza changamoto ya kutotolewa kwa ukamilifu fedha za matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mfano, kiasi cha fedha za matumizi ya kawaida ambacho hakikutolewa kimepungua kutoka Shilingi Bilioni 774.50 sawa na asilimia 18 mwaka 2019/20 hadi Shilingi Bilioni 647.90 sawa na asilimia 16 mwaka 2020/21.

Vile vile, kiasi cha fedha za maendeleo ambacho hakikutolewa kimepungua kutoka Shilingi Bilioni 390.40 sawa na asilimia 41 mwaka 2019/20 hadi Shilingi Bilioni 265.30 sawa na asilimia 29 mwaka 2020/21.

 • Hoja; Kutokusanywa kwa Ushuru wa Huduma wa Shilingi bilioni 1.91 kutokana na ukosefu wa Mfumo wa kielektroniki wa kupeana taarifa za mauzo ghafi kati ya OR – TAMISEMI na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Ufafanuzi; Ushuru wa Huduma ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa unaolipwa kwa kiwango kisichozidi asilimia 0.3 ya mauzo ghafi baada ya kuondoa VAT na ushuru wa bidhaa.

Ofisi ya Rais – TAMISEMI inakamilisha maboresho ya mfumo wa mapato wa LGRCIS/TAUSI ambao pamoja na maboresho mengine, utaunganishwa na mifumo ya TRA ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa za mauzo ghafi ya Wafanyabiashara kwa ajili ya ukokotoaji wa kiasi sahihi cha ushuru wa huduma unaopaswa kulipwa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na hivyo kuondoa mianya ya udanganyifu.

 • Hoja: Uwepo wa miradi isiyokidhi ubora yenye thamani ya shilingi bilioni 6.06 iliyotekelezwa kwa njia ya nguvukazi katika Halmshauri;

Ufafanuzi: katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la kiasi cha fedha kinachopelekwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha, mwaka 2021/22 Serikali imeajiri Wahandisi 260 kwa ajili ya Halmashauri, Mikoa na TARURA. Vile vile, muundo wa Sekretarieti za Mikoa umeboreshwa na kuongezewa bajeti ili kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji kwenye Halmashauri.

 1. Hoja: Upungufu wa Miundombinu katika Shule za Msingi na Sekondari

Ufafanuzi: Serikali imekuwa ikishughulikia changamoto ua upungufu wa miundombinu katika Sekta ya Elimu kwa kutoa fedha kila mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2021/22, Serikali imeidhinisha na kutoa takribani Shilingi bilioni 561.49 kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 19,767 kwa shule za msingi na sekondari, mabweni 58, madawati 47,149; meza na viti 451,918; maabara 875; ofisi 3,184; matundu ya vyoo 3,025; nyumba za walimu 11 na majengo ya utawala manne (4).

Fedha hizo zimetokana na vyanzo mbalimbali, ikiwemo Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO – 19, SEQUIP, Mamlaka ya Elimu, EP4R, GPE LANES II, Ruzuku ya Serikali na Tozo ya Miamala ya Simu.

Vile vile, kwa mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imetenga takribani Shilingi bilioni 164.93 kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu mingine ya shule za msingi na sekondari.

 • Hoja: Upungufu wa Walimu katika Shule za Msingi kwa asilimia 41 katika Halmashauri 48;

Ufafanuzi: Upungufu wa Watumishi ni changamoto ya muda mrefu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hata hivyo, Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto hiyo. Mfano, kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21, Mamlaka za Serikali za Mitaa zilipata vibali na kuajiri Watumishi 14,949 wa Kada ya Elimu. Kati ya Watumishi hao, Walimu wa Shule za Msingi walikuwa 8,649; Walimu wa Shule za Sekondari 6,200 na mafundi sanifu maabara 100 ambao walipangwa kwenye Shule za Sekondari.

Vile vile, Serikali imetoa kibali kingine cha kuajiri walimu 9,800 watakaopangwa kwenye shule za msingi na sekondari zenye uhitaji mkubwa zaidi. Serikali itaendelea kuimarisha huduma ya elimu kwa kuajiri Walimu ili kuendana na kasi iliyopo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu na ongezeko la uandikishaji wanafunzi.

 • Hoja: Ufanisi usioridhisha wa Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ikiwemo kutorejeshwa kwa mikopo ya Shilingi bilioni 47.01, Halmashauri kutochangia Shilingi bilioni 6.68, kutolewa kwa mikopo ya Shilingi milioni 178.61 kwa vikundi visivyokuwa na sifa na mikopo ya Shilingi bilioni 3.26 kutolewa bila kuzingatia uwiano wa utoaji mikopo.

Ufafanuzi:  katika kuimarisha uratibu na usimamizi wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya mfumo wa kielekroniki pamoja na mwongozo wa utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo. Pamoja na mambo mengine mfumo utawezesha kusimamia vigezo vya utoaji wa mikopo, kubainisha aina ya biashara inayoombewa mkopo, wanufaika wa mkopo na mahali walipo.

Aidha, mfumo huo ambao unatarajiwa kuanza kutumika kwenye Halmashauri zote ifikapo tarehe 1 Julai, 2022, utaunganishwa na mifumo mingine kama ya NIDA na Benki ili kuongeza udhibiti wa utoaji wa mikopo, uwazi, usawa, uwajibikaji na ushirikishaji. Juhudi zote hizi zinatarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mikopo hiyo na hivyo kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuviwezesha kiuchumi vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

Kuhusu Halmashauri kutotoa fedha kwa ajili ya kukopesha vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu, mwezi Julai 2018 yalifanyika marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290, kwa kuongeza Kifungu cha 37A ambapo kuanzia wakati huo, utoaji wa mikopo hiyo sio suala la hiyari bali ni matakwa ya kisheria. Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeweka kigezo cha utoaji wa mikopo na pamoja na marejesho yake kuwa sehemu ya vigezo vitakavyotumika kupima utendaji wa Wakurugenzi wa Halmashauri. Upimaji huo utafanyika kila robo mwaka na tathmini ya kina itafanyika mwisho wa mwaka.

 • Hoja: Kutokusanywa kwa mapato kiasi cha Shilingi milioni 900 kutokana na kubomolewa kwa Soko la Tarime na ujenzi wa Soko la Kisasa kusitishwa.

Ufafanuzi: Serikali ilianzisha mkakati wa kuziwezesha Halmashauri kuongeza mapato ya Ndani kupitia utekelezaji wa miradi ya Kimkakati. Kupitia utaratibu huo, Halmashauri huandaa maandiko ya miradi na kuwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uchambuzi. Chini ya utaratibu huo, miradi 38 ilikidhi vigezo na kuidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 298.61 kwa ajili ya utekelezaji. Hadi Machi, 2022 Serikali imeshatoa Shilingi bilioni 196.06 sawa na asilimia 65.70.

Ujenzi wa Soko la Kisasa Kata ya Bomani katika Halmashauri ya Mji Tarime ni miongoni mwa miradi 38 inayotekelezwa chini ya utaratibu huo. Mradi huo umekisiwa kugharimu Shilingi bilioni 8.07 ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 mradi huo ulitengewa Shilingi billion 3 ambapo hadi Machi 2022 zimeshatolewa Shilingi bilioni 1.39 na utekelezaji wa mradi unaendelea.

 • Hoja: Ukosefu wa watumishi waliobobea katika kusimamia uwekezaji katika hisa. Halmashauri hazina vitengo au wafanyakazi maalum wa kusimamia uwekezaji hasa katika hisa. Maafisa mipango hawawezi kutathmini kwa ufanisi fursa za uwekezaji hasa katika hisa kwa kufuatilia na kutathmini hasara na faida zinazohusiana na uwekezaji

Ufafanuzi: Mwezi Januari 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliidhinisha muundo mpya wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Miongoni mwa maboresho yaliyofanyika kupitia muundo huo, ni kuanzishwa kwa Idara mpya ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambayo pamoja na majukumu mengine, itakuwa na jukumu la kuandaa mapendekezo ya kitaalam ya uwekezaji. Hivyo, ni matumaini ya Serikali kwamba changamoto zilizobainishwa na CAG zitaweza kufanyiwa kazi kwa ukamilifu kupitia Idara hiyo mpya.

3       Maelekezo Kuhusu Utekelezaji wa Taarifa ya CAG

Ndugu Wanahabari,

Ili kuhakikisha kuwa mapendekezo yaliyotolewa na CAG yanatekelezwa kwa ukamilifu, ninatoa maelekezo yafuatayo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri:

 1. Menejimenti ya OR-TAMISEMI iandae Mpango Kazi wa utekelezaji wa hoja zote za kimfumo/kisera, ambazo zipo nje ya uwezo wa Halmashauri kuzitekeleza. Utekelezaji wa Mpango Kazi huo iwe agenda ya kudumu kwenye vikao vya Menejimenti ya Wizara. Utaratibu huu utasaidia kuhakikisha kuwa kunakuwa na mwendelezo katika utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya CAG;
 2. Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI awatake maelezo Wakurugenzi wa Halmashauri zote zenye hoja za ukaguzi zenye viashiria vya kutowajibika ipasavyo, pamoja na upotevu wa fedha za Halmashauri;
 3. Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI awasiliane na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ili Taasisi hiyo iweze kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua stahiki, kwa kuwa baadhi ya hoja za ukaguzi zilizobainishwa kwenye taarifa ya CAG, zimetokana na matumizi mabaya ya fedha za umma;
 4. Kwa mujibu wa Kifungu cha 36 cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, na Agizo la 31(1) la Memoranda ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa – 2009, Wakurugenzi wa Halmashauri wana wajibu wa kuhakikisha kuwa taarifa za hesabu za mwisho zinaandaliwa kwa usahihi. Hivyo, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Bunda, Sengerema, Kisarawe, Longido, Mlele, Musoma, na iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambazo zimepata Hati Mbaya na Hati Zenye Shaka, wajitathmini kuhusiana na utendaji wao kwa mujibu wa vifungu hivyo vya Sheria;
 5. Kwa kuwa sehemu kubwa (asilimia 70) ya hoja zilizobainishwa na CAG, zipo ndani ya uwezo wa Halmashauri kuzifanyia kazi, (hoja ambazo zimetokana na Wataalam wa Halmashauri husika kutowajibika ipasavyo), Wakuu wa Mikoa wahakikishe kuwa Halmashauri zote zinatekeleza yafuatayo:
 6. Kuandaa Taarifa ya Majibu na Mpango Kazi wa utekelezaji wa hoja zote zilizobainishwa na CAG, na kuiwasilisha kwa Wakaguzi na nakala OR-TAMISEMI kwa ajili ya ufuatiliaji;
 7. Kuwabainisha Watumishi wote ambao hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo, pamoja na wale ambao walijihusisha na vitendo vya ubadhirifu, na hivyo kusababisha hasara au hoja za ukaguzi zisizo za lazima. Watumishi hao wachukuliwe hatua stahiki za kinidhamu na kisheria na kuwasilisha taarifa za utekelezaji. Hatua hizo zitasaidia kuongeza umakini kwa Watumishi hao, na hivyo kupunguza hoja za ukaguzi zisizo za lazima katika miaka itakayofuata.
 8. Wakuu wa Mikoa washiriki Mikutano Maalum ya Mabaraza ya Madiwani, kujadili taarifa za CAG, na kutoa maelekezo yenye lengo la kuhakikisha kuwa hoja zote za ukaguzi zinafanyiwa kazi;
 9. Ofisi za Wakuu wa Mikoa zihakikishe zinaratibu na kuweka mazingira mazuri ya kufanyika kwa uhakiki wa majibu ya hoja za ukaguzi kwa wakati, na kutoa taarifa kuhusu hoja zilizofungwa. Kama kutakuwa na hoja ambazo hazitafungwa, yatolewe maelezo ya sababu za hoja hizo kutofungwa na mkakati uliowekwa kuhakikisha zinafanyiwa kazi na kufungwa;
 10. Mamlaka za Nidhamu za Waweka Hazina wa Halmashauri zilizopata Hati Mbaya na Hati Zenye Shaka (Halmashauri za Wilaya za Bunda, Sengerema, Longido, Mlele, Kisarawe, Musoma na iliiyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam) ziwachukulie hatua stahiki za kinidhamu kwa kutotekeleza ipasavyo wajibu wao kwa mujibu wa Agizo la 27(3) la Memoranda ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa – 2009. Waweka Hazina wana wajibu wa kutunza kumbukumbu sahihi za fedha kwa mujibu wa miongozo ili kuwezesha uandaaji wa taarifa za hesabu za mwisho;
 11. Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanawawezesha na na kuwatumia Wakaguzi wa Ndani kikamilifu katika kutathimini ufanisi wa mifumo ya udhibiti wa ndani na kuchukua hatua stahiki. Vile vile, Kamati za Ukaguzi ziwezeshwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi ikiwa ni pamoja na kujiridhisha kuwa zimeundwa kwa kuzingatia miongozo iliyopo na pia kuhakikisha kuwa zinajengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao.

4       Hitimisho

Ndugu Wanahabari,

Kipekee napenda kumshukuru na kumpongeza CAG, yeye binafsi na wasaidizi wake kwa ujumla, kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kubainisha maeneo yenye udhaifu na kutoa mapendekezo  yanayosaidia kuboresha utendaji wa Halmashauri na hivyo kutoa nafasi ya utoaji huduma kwa ufanisi zaidi kwa wananchi.

Kwa niaba ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI napenda kumhakikishia CAG ushirikiano wa kutosha ili kuziwezesha Halmashauri kuendelea kuboresha utendaji wake na kuhakikisha matarajio yetu ya kupata maendeleo katika nchi yanafikiwa kwa haraka na kwa faida ya Wananchi wote. Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaendelea kufanya ufuatiliaji kwenye Halmashauri zote ili kuhakikisha kuwa mapendekezo yaliyotolewa na CAG yanatekelezwa kiukamilifu

Ndugu Wanahabari,

Kwa niaba ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI ninawashukuru kwa ushiriano wenu na kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhabarisha Umma kuhusu utendaji wa Serikali ikiwemo namna Serikali inavyowajibika kwa Wananchi katika utoaji wa huduma bora na kwa kuzingatia thamani ya fedha. Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaendelea kufanya kazi nanyi bega kwa bega katika masuala yanayohusu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Asanteni Sana kwa Kunisikiliza

            ————————————–

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *