WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO, ATAKA TIMU IUNDWE KUSIMAMIA ZAO LA KAHAWA

WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera uunde timu za kusimamia zao la kahawa kuanzia uoteshaji wa miche, kilimo chenyewe hadi mauzo ya zao hilo.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa zao la kahawa alichokiongoza kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba leo mchana (Jumapili, Mei 15, 2022) Mheshimiwa Majaliwa amewataka viongozi wa Mkoa huo na wilaya zake waandae vitalu vya miche ya kahawa na kuigawa kwa wananchi ikiwa na moja ya mbinu za kuwahamasha kulima zao hilo.

Amewataka viongozi na watendaji wa mkoa na wilaya kuishawishi sekta binafsi iwekeze kwenye vitalu vya miche ya kahawa ili kupata miche ya kutosha ya kuwauzia wananchi hatua ambayo itaisaidia kujipatia fedha na kutengeneza ajira.

Pia amewataka viongozi na watendaji wa Mkoa na wilaya wahakikishe kuwa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani unafanikiwa kwa kuwaelimisha wananchi faida kubwa watakazozipata kutokana na mfumo huo.

Amesema ili kufanikisha mfumo huo, lazima viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) na kile cha Karagwe (KDCU) wabainishe maeneo itakapofanyika minada ya kahawa na wahakiki na kutangaza hadharani uwepo na wingi wa kahawa inayopigwa mnada.

“Hakuna mnunuzi atakayeruhurusiwa kwenda majumbani au kwenye Chama cha Msingi kupatana bei au kununua kahawa. Kahawa yote inunuliwe kwenye maeneo ya mnada.”

Alisisitiza kwamba wafanyabiashara lazima waratibiwe na wasipewe kabisa fursa ya kujadili bei na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi au wananchi mashambani au majumbani kwani mipango yote ya bei na ununuzi wa kahawa inapaswa kufanyika mnadani.

Mheshimiwa Majaliwa ameagiza kuwa minada iwe wazi na maeneo ya inakofanyika yajulikane pia wakulima washirikishwe ili wajue bei ya mazao yao.

Mheshimiwa Majaliwa pia ameagiza kuwa wanachi washawishiwe kufungua akaunti benki ili malipo ya pesa zitakazotokana na mauzo ya kahawa yao yaingizwe kwenye akaunti hizo hatua ambayo itasaidia kuondoa hatari ya wakulima kuibiwa malipo yao.

Waziri Mkuu aliwasihi viongozi wa Serikali na wa ushirika wajiepushe na biashara ya ununuzi wa kahawa kwani endapo yatatokea mapungufu watawajibika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *