PANYA ROAD WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Kundi la wahalifu ambao wengi wao ni Vijana maarufu kama ”Panya road” baadhi ya waliokamatwa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Kinyerezi jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha(Mapanga).

Mtuhumiwa wa kwanza Daud Abdallah, miaka 22, mzaramo, dereva na mkazi wa Tungini na wenzake 16 walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Fadhili Luvinga kusomewa mashtaka nane yanayowakabili.

Waendesha Mashtaka, Mawakili wa Serikali Michael Ng’hoboko, Avelina Ombock na Nancy Mushumbusi walidai kuwa watuhumiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo tarehe 24/04/2022 maeneo ya Chanika Ilala jijini Dar es Salaam.

Walidai watuhumiwa hao kwa pamoja na wengine ambao bado wanatafutwa walifanya matukio kwa Wananchi mbalimbali kwa kutumia mapanga na kujeruhi kwa lengo la kuwania mali.

Waendesha Mashtaka walidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na waliomba tarehe kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali.

Watuhumiwa wote walikana mashtaka yao. Kesi hiyo ilihairishwa mpaka tarehe 27/5/2022 na wamepelekwa rumande kutokana na makosa waliyoshtakiwa nayo hayana dhamana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *