WAZIRI MKENDA AWATAKA WATANZANIA KUJITOKEZA KUONESHA BUNIFU ZAO, MAKAMU WA RAIS MGENI RASMI

Na Emmanuel Charles

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mara nyingine imeandaa Wiki ya Kitaifa ya Ubunifu inayoambatana na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama MAKISATU kwa mwaka 2022.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Prof. Adolf Mkenda wakati Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Wizara ya Elimu, Sayansi na, Teknolojia Jijini Dodoma
Amesema kuwa katika ngazi ya Mikoa maadhimisho hayo yalianza tarehe 27 Apili, 2022 na yanatarajiwa kukamilika tarehe 14 Mei, 2022.

Prof. Mkenda amesema lengo la wiki ya kitaifa ya Ubunifu ni ni sehemu ya kuongeza hamasa ya matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kama nyenzo ya kutatua Changamoto za Kiuchumi na kijamii.

“Maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu yanafanyika katika ngazi ya Mikoa na Taifa.katika ngazi ya Mikoa, maadhimisho haya yanaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH) na Programu ya FUNGUO chini ya UNDP kupitia kumbi za ubunifu, Vituo vya ubunifu, Taasisi za Umma na binafsi katika Mikoa husika”amesema

Prof. Mkenda amesema Maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu Kitaifa yatafanyika kuanzia ttarehe 15 hadi 20 Mei, 2022 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma ambapo yanatarajiwa kufunguliwa Rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi na hafla ya kufunga itaambatana na utoaji wa Tuzo mbalimbali kwa washindi wa MAKISATU, Washiriki wa maonesho na wadau mbalimbali ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango.

Waziri Mkenda ameendelea kueleza kuwa, Maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu yanaambatana na matukio ya Kilele cha MAKISATU yanayolenga kupata washindi kwa mwaka 2022 katika ngazi ya Kitaifa; Majukwaa ya majadiliano kuhusu maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini yanayohusisha watafiti na wabunifu, Serikali na wadau mbalimbali wa ubunifu na maendeleo ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuhamasisha maendeleo na matumizi ya teknolojia na ubunifu kwaajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, katika maadhimisho hayo kutakuwa na mafunzo na Semina kwa wabunifu ikiwemo elimu ya ujasiriamali.

Pamoja na mambo mengine Mashindano ya Wiki ya Ubunifu na MAKISATU yanalenga kuibua, kutambua na kuendeleza jitihada zinazofanywa na wabunifu wa kitanzania na kuhamasisha matumizi ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu.
“Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Ubunifu yanatoa fursa kwa wabunifu au wagunduzi kujitangaza na kujulikana kwa wawekezaji, watumiaji wa bidhaa na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi” amesema Mkenda

Pia ameitaja Mikoa iliyofanikiwa kuandaa maadhimisho hayo ni pamoja na Dodoma, Dar es salaam, Mbeya, Arusha, Iringa, Mwanza, Zanzibar, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro, Njombe, Kagera, Mtwara, Kigoma, Mara na Ruvuma .
Kwa Upande mwingine Waziri Mkenda ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wabunifu na wananchi wote KUSHIRIKI Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya ubunifu pamoja na kilele cha MAKISATU

“Napenda Kutoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kutumia bunifu mbalimbali za Kitanzania katika Shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi ili kukuza na kuendeleza bunifu na Teknolojia.”Amesema Waziri Mkenda

Kauli Mbiu ya Wiki ya Kitaifa ya Ubunifu kwa Mwaka 2022 ni “Ubunifu kwa Maendeleo Endelevu”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *