PANYA ROAD WENGINE 23 WANASWA NA JESHI LA POLISI DAR

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limeendelea kuisimamia oparesheni maalum kali ya mtaa kwa mtaa , Kata kwa Kata dhidi ya makundi ya wahalifu  ambao wengi wao ni vijana wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu  @ Panya Road. Kufikia tarehe 11.5.2022  tayari wamekamatwaa watuhumiwa 23 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya unyanganyi wa Kutumia silaha  mapanga na visu ,  kuvunja nyumba usiku, kujeruhi na kuiba vitu mbalimbali  hasa maeneo ya Kitunda, Mwanagati  Ilala na Kinondoni maeneo ya  Kunduchi Mtongani  na Tegeta. 

Akizungumza leo Mei 12, 2022 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam SACP. Muliro. J. Muliro amesema Oparesheni hii ambayo ni endelevu inafanywa usiku na mchana  na ilianza tarehe 27/04/2022 na imefanikiwa kuwakamata wahalifu hao ambao wengi wao wana  umri kati ya miaka 13-24. Katika mahojiano, Jeshi la Polisi limebaini kuwa  baadhi ya watuhumiwa hao hawakumaliza shule ya Msingi kwa utoro na sababu zingine  mbalimbali. 

“Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walifanya  tukio la unyanganyi tarehe 10/05/2022, huku wakidai kulipa kisasi kwa baadhi ya watu wa  maeneo hayo baada ya  mtuhumiwa mwenzao  kufariki kwa kushambuliwa na Wananchi wenye hasira kali kwa kujihusisha na  wizi.”

Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na   wananchi wa eneo hilo ilifanikiwa kuvipata vitu vilivyoibwa na wahalifu hao zikiwemo TV 3 na simu 1.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum la Dar es Slaam, limebaini pia kuwepo kwa watu wanaojenga taharuki miongoni mwa wananchi na kusambaza taarifa mbalimbali za matukio ambayo hayapo kwenye maeneo wanayoyataja  kwa lengo la kujenga hofu na taharuki. Jeshi linakemea vikali tabia hiyo .

“Lakini pia kuna wakati Vijana wanapotoka kucheza mpira jioni wanapokuwa wanarejea nyumbani wakiwa kwenye makundi baadhi ya watu wamekuwa wakitumiana ujumbe kuwa kuna makundi hayo ya kihalifu yamezagaa mtaani na wanatenda uhalifu.  Wananchi pia watambue kuwepo na kuimarishwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo navyo vinaanza kazi mapema na baadhi wakiona vikundi hivyo huvihusisha na makundi ya kihalifu. “Amesema Muliro

Ameongeza kuwa Vikundi hivi kwa wale ambao hawavitambui wamekuwa pia wakitumiana ujumbe kuwa wamekutana na makundi ya wahalifu.

“Tunawaomba wananchi wanapokuwa wana taarifa yoyote katika Kanda ya Dar es Salaam   au kama wanataka ufafanuzi wa jambo lolote watumie no  0787 66 83 06 au 0735 00 99 83 . Operation inaendelea na kipindi hiki inawakumbusha  wazazi au walezi  wajibu wao na ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao kisheria  wa kutoa matunzo kwa watoto ikiwemo chakula, mavazi, malazi na elimu kama inavyoelezwa katika Sheria ya Mtoto namba 21 ya Mwaka 2009 ambayo imefanyiwa marekebisho Mwaka 2019 imeelekeza adhabu ya faini au kwenda  gerezani au vyote kwa  pamoja kwa atakayepatikana na hatia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *