Na Emmanuel Charles

Waziri wa Nishati Mhe. Januari Makamba amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwamba, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, Serikali ijibane na ijinyime na zitolewe shilingi bilioni mia moja (Shilingi 100,000,000,000) kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini. Ruzuku hii inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22.
Waziri Makamba ameyasema hayo Leo Mei 10, 2022 Bungeni Jijini Dodoma Wakati akiwasilisha Maazimio ya Serikali Baada ya Hoja za Wabunge na kuagizwa na Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson
“Kutolewa kwa ruzuku hii hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea. Nafuu nyingine, inayotokana na mikopo niliyoieleza hapa awali, itakuja katika mwaka ujao wa fedha itaelezwa kwa kina zaidi na Waziri wa Fedha kwenye Bajeti ya Serikali mwezi ujao.”Amesema
Amesema ruzuku hii ya shilingi bilioni 100 itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei kuanzia tarehe 1 Juni 2022. Hii ni kutokana na kuwa, wafanyabiashara wa jumla wamekwisha lipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei hizi za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wamekwishanunua mafuta kwa bei hii inayotumika sasa.
“Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zisizo za kifedha zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na:
- Kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu kufanya hivyo. Wizara imekamilisha kufanya tathmini ya kampuni zote zilizoonesha nia ya kuweza kuleta mafuta kwa bei nafuu kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wao wa kuleta mafuta hayo ili kuhakikisha uwepo wa mafuta nchini (security of
supply). Mipango hii ikileta matokeo yanayotarajiwa, bei za mafuta zitapungua zaidi kuanzia mwezi Agosti 2022.”
- Pia Hatua nyingine ni Kuanzisha Mfuko wa Kuhimili Ukali wa Bei za mafuta (Fuel Price Stabilization Fund). Serikali imeandaa utaratibu wa kuanzisha mfuko maalumu utakaotumika kupunguza makali ya bei ya mafuta kipindi ambacho bei hizo zinaongezeka kwa kiasi kikubwa. Mpango wa kuanzisha mfuko huu uko katika hatua za mwisho za maandalizi na utakapokamilika, utawasilishwa katika Baraza la Mawaziri.
- Kuanzisha Hifadhi ya Mafuta ya Kimkakati (National Strategic Petroleum Reserve). Serikali inakamilisha marekebisho ya Kanuni za kuanzisha na kuendesha hifadhi mafuta ya kimkakati ili nchi yetu ijihakikishie usalama wa upatikanaji wa mafuta na unafuu wa bei katika vipindi kama hivi.
- Kuwa na kituo kikubwa cha mafuta (Petroleum Hub). Serikali inakamilisha makubaliano ya kujenga maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta kwa ajili ya
kuuzwa ndani na nje ya nchi kulingana na uhitaji. Uwepo wa kituo hiki utawezesha nchi kupata mafuta yenye bei nafuu pale bei zinapopanda kupita kiasi.
Mpango huu na utekelezaji wake unaweza kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu.
- Kuanzisha upokeaji wa mafuta katika ghala moja (Single Receiving Terminal – SRT) kupitia maghala ya TIPER ili kupunguza au kuondoa gharama za meli kusubiri au kuchukua muda mrefu katika upakuaji wa mafuta katika maghala mengi. Gharama hizi nazo zina mchango katika bei ya mafuta (demurrage charges). Hatua hii itaondoa changamoto za udanganyifu na kuongeza ufanisi katika biashara ya mafuta hapa nchini. Hatua hii inaendana na kuyafanya maghala haya kuwa Customs Bonded Warehouse ili kushamirisha biashara ya mafuta yanayokuja nchini na kwenda kwenye nchi nyingine.
- Kuiongezea uwezo TPDC kuagiza mafuta nje ya nchi, ambapo kwa mara ya mwisho ilifanya shughuli hiyo miaka 20 iliyopita.
- Kuimarisha utendaji na weledi wa taasisi za Serikali zinazoshughulika na biashara ya mafuta nchini, ikiwemo EWURA na PBPA (Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja).
“Mheshimiwa Spika, hatua hizi zitafafanuliwa kwa kirefu na fursa ya Wabunge kutoa maoni na ushauri wao wakati wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati wiki tatu zijazo.”
Ameendelea kufafanua kwa kusema kuwa, “Mheshimiwa Spika, bunge lako litakuwa limebaini changamoto za foleni na vurugu katika vituo vya mafuta zilizopo katika nchi nyingine zinazotokana na uhaba wa mafuta. Pamoja na changamoto ya bei, ambalo sio suala letu peke yetu, usimamizi wa sekta ya mafuta hapa nchini, hasa katika kipindi hiki kigumu, umekuwa wa utulivu na wa umakini. Hii sio kwasababu ya ajali bali ni kwa jitihada za makusudi za Serikali kwa ushirikiano na sekta binafsi.”
Amesema Bei za mafuta kupanda ni janga lakini hatari kubwa zaidi hata kwa usalama wa nchi ni kukosekana kwa mafuta. Hili halijatokea hapa kwetu na hatutaruhusu litokee. Leo tunapozungumza tunayo petroli ya kutosheleza kwa mahitaji ya siku 34, dizeli ipo ya kutosheleza kwa mahitaji ya siku 27, mafuta ya taa kwa siku 81 na mafuta ya ndege kwa siku 26. Haya ni mafanikio kwani sote tunafahamu kwamba zipo nchi zimelazimika kutaifisha mafuta ya nchi nyingine yanayopitia kwao kutokana na uhaba.
