SENSA 2022: BAJETI YAKE CHANGIA,IDADI KUJIFAHAMU,MAENDELEO YATIMU

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)


AGOSTI 23, 2022 ni siku muhimu ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi bara na visiwani.
Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo kwenye maandalizi ya kufanya sensa hiyo.
Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.
Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.Kwa nini Sensa?
Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum.

Kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi.
Takwimu hizi za msingi ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.
Bw.Lwaga Mwambande ambaye ni Mshairi wa Kisasa anakushirikisha jambo kuhusu ukubwa wa Sensa ya Watu na Makazi na umuhimu wake kwa Taifa kupitia shairi lifuatalo, Karibu;
A:Sensa ni jambo muhimu, kuifanya kumetimu,Tunaifanya kwa zamu, ili kupata takwimu,
Tuweze kujifahamu, namna ya kujikimu,
Chondechonde marafiki, bajeti yake changia.

B: Kuzikusanya takwimu, kwa sensa tunafahamu,
Gharama zake ni ngumu, kote kule inadumu,
Kuchangiana muhimu, ni undugu damu damu,Chondechonde marafiki, bajeti yake changia.
C: Serikali twafahamu, imeitumia zamu,
Marafiki wa muhimu, kawaita kama timu,
Sio kufanya karamu, kuhusu sensa takwimu,
Chondechonde marafiki, bajeti yake changia.

D: Tarehe twaifahamu, Agosti ya muhimu,
Sisi sote wanadamu, humu Tanzania humu,
Kwa kutumia kalamu, zitakusanywa takwimu,Chondechonde marafiki, bajeti yake changia.

E: Ishinatatu ikitimu, tarehe ile muhimu,
Tukusanyike kitimu, zipatikane takwimu,
Mipango itayoitimu, kwetu ibaki mitamu,
Chondechonde marafiki, bajeti yake changia.

F: Sensa ni kitu adhimu, kila taifa muhimu,
Idadi kujifahamu, maendeleo yatimu,
Tusiendelee dumu, kubahatisha takwimu,
Chondechonde marafiki, bajeti yake changia.

G: Nasi sote wanadamu, sensa tusijekaimu,
Tukaziacha salamu, sisi mbali tukadumu,
Tushiriki zamu zamu, kwa usahihi takwimu,
Chondechonde marafiki, bajeti yake changia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *