VIDEO-PANYA ROAD 31 WANASWA DAR BAADA YA OPARESHENI KALI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetangaza kuwanasa Watu 31 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo, uporaji baada ya kuvunja nyumba, kujeruhi na kuiba vitu kwenye makazi ya watu.

Hatua hiyo ni kufuatia Oparesheni Maalum ya msako wa mtaa kwa mtaa iliyolenga kubaini makundi ya vijana wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu maarufu kama Panya Road.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muliro amesema Opareshen hiyo endelevu ilianza April 27, 2022 na hadi kufikia Mei 6, 2022 imefanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao ambao wengi wao ni vijana
wenye umri kati ya miaka 13-20, ambao hutumia Silaha kama Mapanga, visu, nondo, na mikasi mikubwa ili kutekeleza Uhalifu.“Katika mahojiano ya kina, Jeshi la Polisi limebaini kuwa watuhumiwa hao
wamehusika katika vitendo hivyo vya kihalifu na kuonesha baadhi ya vitu walivyoiba zikiwemo TV 12 na simu za mkononi 4″ amesema Kamanda Muliro.

Kufuatia msako huo Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatoa onyo na halitasita kuwakamata watu ambao wamekuwa wakipokea mali mbalimbali za wizi zinazotokana na matukio ya kihalifu ikiwemo kuwafikisha kwenye vyombo vingine vya kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *