MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA MWAKILISHI WA UNHCR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 6 Mei 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) hapa nchini Mahoua Parums, mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo Bi. Mahoua Parums amesema Tanzania imeendelea kuwa nchi muhimu zaidi kwa Shirika la kuwahudumia wakimbizi pamoja na wakimbizi wenyewe kutokana na kuwa nchi iliopokea idadi kubwa ya wakimbizi kwa miongo kadhaa. Ameongeza kwamba mchango wa Tanzania katika kupokea na kuhudumia wakimbizi hautasahaulika ikiwa ni pamoja na ukarimu wanaopata wakimbizi mahali wanapofikia.

Bi. Parums amesema anafurahi kuwa katika nchi ambayo ina umoja na mshikamano na mataifa mengine wakati wa kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo za wakimbizi.

Makamu wa Rais Dkt. Mpango amemkaribisha Mwakilishi huyo mkazi hapa nchini na kumuahidi kwamba serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) hapa nchini.

Aidha ameongeza kwamba Tanzania imekua mstari wa mbele katika kutafuta muafaka wa amani na utulivu katika nchi zinazokumbwa na migogoro mbalimbali ikiwemo vita ili kupunguza idadi ya wakimbizi wanaokimbia nchi hizo. Amesema kinachohitajika ni kuhakikisha kunapatikana suluhu za kudumu katika mataifa yaliokumbwa na migogoro ili wakimbizi hao wapate kurudi katika nchi zao na kushiriki katika shughuli za maendeleo katika nchi hizo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Jumuiya ya Madola wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Mheshimiwa Patricia Scotland, mazungumzo yaliofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *