WATAALAMU WA OFISI YA RAIS-TAMISEMI WASISITIZA JAMBO KWA CHMTS

WATAALAM kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) wamezitaka Timu za Usimamizi na Uendeshaji wa Shughuli za Afya Ngazi ya Halmashauri (CHMTS) kuandaa ramani ya mpangilio wa majengo ya kutolea huduma za afya.

Maandalizi hayo yanapaswa kufanyika kabla ya kuanza kutekeleza ujenzi ili kuepusha changamoto ya majengo yanayotoa huduma zinazoshabiliana kukaa sehemu tofauti.

Hayo yamebainishwa na msimamizi wa miradi ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya OR-TAMISEMI, Dkt.Sonda Shaaban, Aprili 30,2022 katika kikao kazi cha wataalam kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka OR-TAMISEMI na CHMTS Mkoa wa Simiyu.

Amesema kuwa, halmashauri nyingi zimekuwa hazina mpangilio mzuri wa majengo katika vituo vya kutolea huduma za afya jambo ambalo linapelekea majengo yanayotoa huduma zinazofanana kutawanyika na kuleta usumbufu kwa mwananchi wakati wa kupata huduma.

Aidha,wataalam hao wamezitaka CHMTS kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja katika kuratibu shughuli za afya hasa katika ukaguzi wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba kwa kuwa jukumu hilo sio la Mganga Mkuu wa Wilaya pekee bali ni la CHMTS kwa pamoja.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Bi.Elizabeth Gumbo ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika halmashauri hiyo na ametoa wito kwa Serikali kuangalia kigezo cha jografia za halmashauri wakati wa ugawaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kupunguza baadhi ya changamoto ambazo zinaweza kupelekea ucheleweshwaji wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika ziara hiyo wataalam hao walifanikiwa kutembelea ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ambapo wamezipongeza halmashauri hizo kwa kusimamia vizuri miradi inayotekelezwa huku wakizitaka halmashauri hizo kuongeza kasi katika utekelezaji na kufanya maboresho katika maeneo ambayo yana mapungufu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *