Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan
Mitawi amesema changamoto ya kukatika kwa mawasiliano inayowakabili
wananchi wa Kijiji cha Swipese, Pemba inatarajiwa kumalizwa na ujenzi wa
kivuko cha watembea kwa miguu katika eneo hilo.
Tathmini ilionesha kuwa maji ya bahari yameingia katika maeneo ya kilimo cha
mpunga na wananchi wa Shehia ya Mkungu kijijini hapo hivyo kujaa kwa maji
haya pia kumesababisha kukatika kwa mawasiliano kutoka upande wa pili
takribani kilometa 3.3.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo kwa Mkandarasi Dezo Civil
Contractors Co. Limited kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi,
Mary Maganga katika eneo la Kwa Mgogo wilayani Mkoani, Mkoa wa Kaskazini,
Mitawi alisema ujenzi huo utagharimu sh. bilioni 1.2.
Alisema kivuko hicho katachojengwa kwa kiwango cha juu na kudumu kwa
miaka takriban 40 bila kufanyiwa ukarabati, litakuwa msaada mkubwa kwa
wananchi hao kwa kuwapunguzia adha ya kuvuka inayowakabili ambapo ujenzi
wake utakuwa wa kipindi cha miezi 18.
Mitawi alisema utekelezaji wa mradi huo ni matunda ya ziara za viongozi
mbalimbali wa kitaifa walizofanya kwa nyakati tofauti tangu mwaka 2019 na hivyo
kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo ili kazi ifanyike kwa
haraka na ufanisi.
“Leo tumekuja kukabidhi eneo hili kwa mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi
mara moja na tunatarajia atakamilisha chini ya muda uliopanga kama alivyofanya
katika maeneo mengine, niwaombe wananchi mtoe ushirikiano kwa mkandarasi
atakapohitaji eneo la kuweka vifaa vya ujenzi na pia kwa mujibu wa maelekezo
ya Mheshimiwa Makamu wa Pili kuwa kwa zile shughuli ndogondogo kipaumbele
kiwe kwa wakazi wa hapa,” alisema Mitawi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzubar
Bw. Thabit Idarous Faina alisema kuwa athari hizi za kimazingira zimewakabili
wananchi wa eneo hilo kwa kipindi cha muda mrefu kiasi cha kusababisha
washindwe kuvuka upande mmoja kwenda mwingine kufuata mahitaji ya kila
siku.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Kusini Mattar Zahor Masoud akizungumza ofisini kwake
wakati viongozi hao walipofika kujitambulisha, aliahidi kutoa ushirikiano kwa
mkandarasi na kusema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia shughuli kulihifadhi
eneo hilo sambamba na kufanya shughuli za uchumi kufanyika kwa urahisi.
MATUKIO KATIKA PICHA
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan
Mitawi (wa pili kushoto mwenye kofia) akizungumza wakati wa makabidhiano ya
mradi wa ujenzi wa kivuko cha waenda kwa miguu kwa kwa Mkandarasi Dezo
Civil Contractors Co. Limited katika eneo la Kwa Mgogo Kijiji cha Sipwese Wilaya
ya Mkoani, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Wengine wa tatu kushoto ni Katibu Mkuu
Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Thabit Idarous Faina na kushoto ni Mkurugenzi
wa Idara ya Mazingira Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Bi. Farhat Ali
Mbarouk.

Mmoja wa wananchi wa la Kwa Mgogo Kijiji cha Sipwese Wilaya ya Mkoani,
Mkoa wa Kaskazini Pemba akivuka maji kutoka upande mmoja kwenda
mwingine kutokana na athari za maji ya bahari kufurika katika eneo hilo, tayari
Serikali imeanza hatua ya mradi wa ujenzi wa kivuko kitakachowasaidia kuvuka.

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan
Mitawi na viongozi mbalimbali akiwa katika litakalojengwa la mradi wa ujenzi wa
kivuko cha waenda kwa miguu Kijiji cha Swipese, Pemba.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)