MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA WAWAKILISHI WA JUKWAA LA UCHUMI DUNIANI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. Philip Mpango amesema katika karne ya 21 Bara la Afrika linapaswa
kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo pamoja na kuunganisha
mawazo kwa pamoja ili kutatua changamoto zinazokabili bara hilo.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 2 Mei 2022 alipokutana na
kufanya mazungumzo na wawakilishi kutoka Sekretarieti ya Jukwaa la
Uchumi Duniani wakiongozwa na Mkuu wa Ajenda za Afrika bwana
Chido Munyati, Mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu
ya Tanzania Jijini Dodoma.
Amesema kwa sasa bara la Afrika ikiwemo Tanzania linahitaji zaidi
teknolojia ili kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo pamoja na
kuendana na uchumi wa kidijitali. Ameongeza kwamba umoja baina ya
nchi za Afrika utachochea ukuaji wa biashara katika eneo huru la Afrika
na kuinua uchumi baina ya mataifa.
Aidha ameongeza kwamba uwekezaji katika ujenzi miundombinu kama
vile Reli na Barabara baina ya mataifa utaongeza kasi ya ufanyaji
biashara na ukuzaji wa uchumi ndani ya bara la Afrika. Makamu wa Rais
amesema Tanzania inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka
Pwani ya bahari ya Hindi kupitia katikati ya Tanzania hadi Magharibi
mwa Tanzania na kanda ya ziwa itakayosaidia nchi za Afrika mashariki
katika usafiri na biashara.
Wawakilishi hao wamemkaribisha Makamu wa Rais katika mkutano
mkuu wa Jukwaa la Uchumi Duniani unaotarajiwa kufanyika Davos
nchini Uswisi tarehe 22 – 26 Mei 2022. Wamesema mkutano huo utatoa
fursa kwa Tanzania kueleza fursa zinazopatikana nchini ili kuvutia
wawekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za Kilimo, Nishati ,utalii
pamoja na Uchumi wa buluu. Aidha mkutano huo unalenga kuimarisha
ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi katika kuyafikia maendeleo
kwa mataifa ya Afrika.
Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Uchumi Duniani unatarajiwa
kuwakutanisha wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa mbalimbali,
wawakilkishi wa mashirika ya kimataifa , wakuu wa taasisi na
makampuni mbalimbali duniani, pamoja na wafanyabiashara.

MATUKIO KATIKA PICHA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. Philip Mpango akizungumza na wawakilishi kutoka Sekretarieti ya
Jukwaa la Uchumi Duniani wakiongozwa na Mkuu wa Ajenda za Afrika
bwana Chido Munyati, Mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Benki
Kuu ya Tanzania Jijini Dodoma leo tarehe 2 Mei 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *