Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza nauli mpya za mabasi ya safari ndefu na mabasi yanayotoa huduma kwenye majiji na miji zitakazoanza kutumika tarehe 14 Mei, 2022.
Akizungumza katika mkutano wa wanahabari na wadau wa Usafiri Ardhini nchini, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA Bw. Gilliard Ngewe amesema kuwa mabasi yanayoenda mikoani, kwa daraja la kawaida, kiwango cha ukomo ambacho Mamlaka imeridhia kwa abiria kwa kilometa ni shilingi 41.29 ambapo ni sawa na ongezeko la shilingi 4.40 sawa na asilimia 11.92 ambapo kiwango kilichokuwa kinatumika zamani ni shilingi 36.89 kwa abiria kwa kilometa.
Vilevile amesema, kwa daraja la kati, kiwango cha sasa kwa abiria kwa kilometa ni shilingi 56.88 ambayo ni sawa na ongezeko la shilingi 3.66 sawa na asilimia 6.88, kiwango kilichotumika hapo awali kilikuwa ni shilingi 53.22 kwa abiria kwa kilometa.
Aidha, Bw. Ngewe ameeleza kuwa viwango vya nauli kwenye barabara za vumbi itakuwa ongezeko la asilimia 25 ya daraja la kawaida kwa barabara ya lami ambayo ni sawa na shilingi 51.61 kwa abiria kwa kilometa
Nauli hizi mpya ni matokeo ya kikao cha pamoja kati ya LATRA na wadau wa usafiri ardhini kilichofanyika kwa ajili ya kukusanya maoni na mapendekezo ya bei mpya za mabasi ya safari ndefu na yale ya mijini.

MAJEDWALI HAPO CHINI YANAONESHA MABADILIKO YA NAULI MPYA ZILIZOTANGAZWA NA ZILE ZA ZAMANI

