OFISI YA RAIS-TAMISEMI yavutiwa na ufanisi wa ujenzi Kituo cha Afya Chabalasi

KITUO cha kutolea huduma za afya cha Chabalasi kilichopo katika Kata ya Nyabionza Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ni moja ya kituo cha mfano katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya ambapo thamani ya fedha imeonekana huku ujenzi huo ukitekelezwa katika viwango bora.Ujenzi huo ambao unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 105 ambapo nguvu ya jamii ni shilingi milioni 12, mfuko wa jimbo shilingi milioni 5.5, mapato ya ndani ya halmashauri shilingi milioni 25 pamoja na fedha kutoka Serikali Kuu shilingi milioni 50 upo katika hatua ya ukamilishaji na unatarajia kukamilika Mei 17, 2022.

Akizungumza kwa niaba ya timu ya ufatiliaji wa shughuli za afya kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mkurugenzi wa Afya,Lishe na Ustawi wa Jamii, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa, timu imeridhishwa na kasi,viwango pamoja na matumizi ya fedha katika mradi huo.

Aidha,timu imewapongeza wananchi wa Kata ya Nyabionza kwa kuchangia fedha katika utekelezaji huo na imeahidi kuleta watumishi katika kituo hicho huku ikitafutia ufumbuzi uwepo wa nyumba ya watumishi ili kurahisha upatikaji wa huduma kwa wananchi.

Wananchi wa kata hiyo wameishukuru Serikali kwa kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na kuahidi kushirikiana na Serikali katika kusimamia utekelezaji wa miradi,pia wamehaidi kutoa nyumba kwa ajili ya watumishi watakaotoa huduma katika kituo hicho huku wakisubiria ujenzi wa nyumba ya watumishi.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Chabalasi, Bw.Moris Pantelope amesema, ataendelea kuhamasisha wananchi ili kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mingine ya kutolea huduma za afya ili kituo hicho kiweze kuongeza wigo katika utolewaji wa huduma za afya.

Aidha timu hiyo ilitembelea Zahanati ya Kakulaijo na kufanya ukaguzi wa bidhaa za afya, ambapo ilibaini mapungufu machache na kutumia ziara hiyo kutoa elimu ya utunzaji na ujazaji wa taarifa za bidhaa za afya katika kituo hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *