
Waziri wa Madini Mhe. Dkt Dotto Biteko ameliomba Bunge kupitisha Makadirio ya shilingi 83,445,260,000.0 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 leo Bungeni Dodoma amesema ili Wizara iweze kutekeleza majukumu na malengo yaliyopangwa, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha makadirio ya shilingi 83,445,260,000.0 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
“Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha uwezo wa Taasisi katika kutoa huduma, GST inakusudia kufanya yafuatayo: kuboresha mifumo ya uchakataji, uhifadhi na usambazaji wa taarifa za jiosayansi kuhusu upatikanaji wa madini; kuwawezesha watumishi kupata mafunzo ya muda mfupi na mrefu; kuboresha mazingira ya utendaji kazi na maslahi ya watumishi; kutangaza (marketing) bidhaa na huduma zitolewazo na GST; na kukamilisha kufanya mapitio na maboresho ya Muundo wa Taasisi ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya GST”
Kwa upande mwingine ameeleza kuwa katika kukabiliana na majanga ya asili ya jiolojia kama vile matetemeko ya ardhi, maporomoko ya ardhi, na milipuko ya volkano, GST inakusudia kufanya mambo yafuatayo: kukusanya takwimu kutoka vituo vitano (5) vya kudumu vya kupimia matetemeko ya ardhi vilivyoko Arusha, Dodoma, Geita, Mtwara na Mbeya ili kujua matukio mbalimbali ya mitetemo; kuchakata takwimu zilizokusanywa kutoka katika vituo hivyo na kuhuisha ramani inayoonesha vitovu vya matetemeko ya ardhi nchini;
Amesema Tume ya Madini itaendelea kuzihusisha mamlaka nyingine za Serikali zinazofungamana na sekta katika utekelezaji wa majukumu ikiwa ni pamoja na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),
Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Taasisi za Fedha, pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha changamoto mbalimbali zikiwemo za kisheria, mitaji, upatikanaji wa vibali, tozo na kodi ambazo zimekuwa zikiwakabili wachimbaji nchini zinatatuliwa kwa wakati na kwa maridhiano.
” Mheshimiwa Spika, Tume ya Madini itaendelea kuimarisha utendaji kazi wake kwa lengo la kuisimamia ipasavyo Sekta ya Madini nchini kwa kuboresha mazingira na vitendea kazi na kuwaongezea ujuzi na weledi”
