WAZIRI BASHUNGWA AWATAKA WANANCHI KUPAZA SAUTI SERIKALI ICHUKUE HATUA

NA OR-TAMISEMI


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kupaza sauti pale wanapoona hali isiyo ya kawaida kwenye utekelezaji miradi ya maendeleo katika maeneo yao ili Serikali iweze kuchukua hatua.

Bashungwa ametoa wito huo katika futari maalum iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Karagwe kwa kushirikiana na Shekhe wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, Nassibu Abdu Abdalah iliyofanyika katika Msikiti wa Omurushaka, Aprili 27, 2022.

“Ofisi ya Rais – TAMISEMI tutakuwa wakali sana katika usimamizi wa miradi katika halmashauri na niendelee kutoa wito kwa watanzania katika vijiji na vitongoji mnapoona hali isiyo ya kawaida pazeni sauti ili tuchukue hatua,” amesema Bashungwa.

Bashungwa ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ndani ya mwaka mmoja amepeleka fedha za maendeleo na miradi kwa kila kata nchi nzima.

Aidha, Bashungwa amewashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kushirikiana Serikali na kwa kuimarisha amani na upendo katika jamii yetu.

Vile vile, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu operesheni ya uwekaji wa Anwani za Makazi inayofanyika nchi nzima na sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwezi Agosti, mwaka huu.

Awali, Shekhe wa Mkoa wa Kagera, Shekhe Haruna Kichwabuta ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha umoja na mshikamano katika jamii inayowazunguka bila kujali dini na kabila la mtu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *