HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA BAJETI YA MWAKA 2022/2023  

HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA  

RAIS KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA

MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2021/22 NA

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI

KWA MWAKA 2022/23

Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo (Mb.),

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor

Mpango akishuhudia   utiaji saini wa hati za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi. Hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii, Maruhubi, Zanzibar Agosti 24, 2021.

Aprili, 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo. Uzinduzi ulifanyika Februari 12, 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akipanda mti katika shamba la miti lililopo katika msitu wa Rubare wilayani Bukoba mkoani Kagera wakati alipotembelea na kukagua mistu huo Machi 18, 2022.

A. UTANGULIZI

 1. Mheshimiwa Spika, baada ya Bunge lako

Tukufu kupokea taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka 2021/22 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2022/23, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka 2021/22 na kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2022/23.

 • Mheshimiwa Spika, kwa dhati naomba kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuwaletea maendeleo wananchi.  Katika kipindi cha mwaka mmoja tumeshuhudia mambo makubwa katika nyanja za elimu, afya, maji, miundombinu na kuimarika kwa Muungano na Uhifadhi wa Mazingira. 
 • Aidha, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumsaidia Rais wa

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutimiza majukumu yake na kuisimamia ipasavyo Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

 • Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumpongeza pia Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi nzuri anazofanya kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kuuenzi na kuudumisha Muungano wetu.
 • Mheshimiwa Spika, ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hotuba yake nzuri ambayo imetoa mwelekeo wa kisera katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kipindi cha mwaka 2022/23. Aidha, nampongeza kwa uongozi wake thabiti katika kusimamia shughuli za Serikali ndani na nje ya Bunge lako Tukufu. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wote kwa ushirikiano walionipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kusimamia shughuli za Muungano na

Mazingira.

 • Mheshimiwa Spika, ninapenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita. Aidha, nawapongeza kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kuiletea nchi yetu maendeleo.
 • Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kukupongeza wewe Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb.), kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ninampongeza Mheshimiwa Mussa Hassan Zungu (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa kuwa Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuwa wajumbe wa kamati hizo; na ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuwa Wabunge wa

Bunge hili Tukufu. 

 • Mheshimiwa Spika, ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama (Mb.); Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira, Mheshimiwa David Kihenzile Mwakiposa (Mb.); na Waheshimiwa wajumbe wa Kamati hizo kwa kupokea, kujadili na kupitisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2021/22 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka 2022/23. 
 • Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, sasa ninaomba kutoa taarifa ya utekelezaji wa kazi za Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kipindi cha mwaka 2021/22 na malengo ya mwaka 2022/23.

B. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2021/22

Bajeti Iliyoidhinishwa kwa Mwaka 2021/22

10. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais ina mafungu mawili ya kibajeti ambayo ni Fungu 26 kwa ajili ya Ofisi Binafsi ya Makamu wa Rais na Fungu 31 kwa ajili ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

Fungu 26

11. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, jumla ya Shilingi 12,915,077,000.00 ziliidhinishwa kwa ajili ya Fungu 26. Kati ya fedha hizo, Shilingi 11,930,965,000.00 zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 984,112,000.00 zilikuwa kwa ajili ya malipo ya Mishahara.

Fungu 31

12. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Fungu 31, Shilingi 22,138,382,500.00 ziliidhinishwa. Kati ya fedha hizo Shilingi 15,287,594,500.00 zilikuwa kwa ajili yaMatumizi ya Kawaida na Shilingi 6,850,788,000.00 zilikuwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Bajeti ya Matumizi ya Kawaida inajumuisha Shilingi 3,021,908,000.00 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Shilingi 3,751,798,000.00 kwa ajili yaMishahara ya Watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)na

Shilingi 8,513,888,500.00 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Bajeti ya Miradi ya Maendeleo inajumuisha Shilingi 4,280,000,000.00 fedha za ndani na Shilingi 2,570,788,000.00 fedha za nje.

Fedha zilizopokelewa na kutumika hadi Machi,

2022

Fungu 26

13. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai,

2021 hadi Machi 2022, jumla ya Shilingi 9,529,714,319.33 sawa na asilimia 73.8 ya bajeti iliyoidhinishwa zilipokelewa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yaliyopo chini ya Fungu 26. Kati ya fedha hizo, Shilingi 8,947,914,319.33 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo, sawa na asilimia 75.0na Shilingi 581,800,000.00 ni kwa ajili ya mishahara sawa na asilimia59.1.Aidha, katika kipindi hicho jumla ya Shilingi 9,380,571,137.48 sawa na asilimia98.4ya fedha zilizopokelewa zilitumika.

Fungu 31

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi, 2022 Ofisi ilipokea jumla ya Shilingi 11,326,006,101.83 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida sawa na asilimia 74.1 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya kiasi kilichopokelewa, Shilingi 2,034,315,643.56 ni mishahara ya Watumishi Ofisi ya Makamu wa Rais, Shilingi 3,092,783,799.00 ni Mishahara ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na Shilingi 6,198,906,659.27 ni Matumizi Mengineyo. Kati ya kiasi kilichopokelewa, Shilingi 10,600,098,525.05 zilitumika sawa na asilimia 93.6.
 1. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa bajeti ya Maendeleo jumla ya Shilingi 11,261,679,547.53 zilipokelewa sawa na asilimia 164.4 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya kiasi hicho fedha za ndani ni Shilingi 3,092,406,494.26 sawa na asilimia 72.3 na fedha za nje ni Shilingi 8,169,273,053.27 sawa na asilimia 317.8. Aidha, katika kipindi hicho, Shilingi 7,712,508,184.50 zilitumika ambapo Shilingi 2,096,925,907.74 ni fedha za ndani sawa na asilimia 67.8 na Shilingi 5,615,582,276.76 ni fedha za nje sawa na asilimia 68.7.   
 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi, 2022 Ofisi imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa

Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22– 2025/26); Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha

Mapinduzi (2020– 2025); Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021; Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura,191; Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063, Malengo ya Maendeleo Endelevu; na Maelekezo na Miongozo mbalimbali inayotolewa na Viongozi Wakuu.

KAZI ZILIZOTEKELEZWA KATIKA MWAKA 2021/22

MASUALA YA MUUNGANO 17. Mheshimiwa Spika, Muungano wetu umekuwa ni msingi mkuu wa amani na maendeleo uliojengeka kwa      umoja,   ushirikiano,        mashauriano        na kuheshimiana. Aidha, Serikali inatambua kuwa Muungano wetu ni Tunu ya Taifa letu na ndio utambulisho wetu       duniani, hivyo      kuulinda, kuudumisha na kuuenzi ni jukumu letu sote. Katika mwaka wa fedha 2021/22, Ofisi ya Makamu wa Rais

ilipanga na kutekeleza yafuatayo:-

(i) Kuratibu Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano

 1. Mheshimiwa Spika, Kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kilichofanyika Dodoma tarehe 09

Februari, 2019 kilitoa maagizo kuhusu hoja 18 za Muungano zilizohitaji kutafutiwa ufumbuzi. Hadi kufikia tarehe 24 Agosti, 2021 Wizara zenye hoja ziliendelea kufanyia kazi maagizo ya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ. 

 1. Mheshimiwa Spika,  Katika mwaka 2021/22 Ofisi ya Makamu wa Rais imeratibu vikao sita (6) vya kutafuta ufumbuzi wa  hoja 18 za Muungano. Vikao hivyo vilifanyika katika ngazi ya Mawaziri; Makatibu Wakuu wa SJMT na SMZ; Kamati ya Uchumi, Fedha na Biashara; na Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ.

Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Fedha, Uchumi na Biashara ngazi ya Makatibu Wakuu wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukamilika kwa kikao kazi. Katikati ni Mwenyekiti wa Kikao hicho Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango (SMT), Bw. Emmanuel Mpawe Tutuba. Kikao kilifanyika Dodoma tarehe 2 Agosti, 2021

 • Mheshimiwa Spika, Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ kilifanyika Zanzibar tarehe 24 Agosti, 2021 chini ya Uongozi na Uenyekiti wa Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kikao hicho ilikubalika kuwa, hoja kumi na moja (11) zimekwishafanyiwa kazi na kukamilika na  hivyo ziondolewe kwenye orodha ya hoja za Muungano.
 • Mheshimiwa Spika, hoja zilizopatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya Hoja za

Muungano ni: 

 • Uvuvi kwenye Ukanda wa Uchumi wa

Bahari Kuu;

 • Uingizaji wa maziwa kutoka Zanzibar;
 • Ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano;
 • Mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada ya kibajeti;
 • Mkataba wa Mkopo wa Fedha za Mradi wa Ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja;
 • Mkataba wa Mkopo wa Fedha za Ujenzi wa Barabara ya Chake Chake hadi Wete – Pemba;
 • Mkataba wa Mkopo wa Fedha za Ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri;
 • Usimamizi wa Ukokotoaji na Ukusanyaji wa Kodi kwenye Huduma za Simu unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar;
 • Mapato yanayokusanywa na Uhamiaji kwa upande wa Zanzibar;
 • Uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Rufaa za Kodi kutoka Zanzibar; na
 • Uteuzi wa Mjumbe wa Bodi ya Bima ya Amana kutoka Zanzibar. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akishuhudia   utiaji saini wa hati za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi. Hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii, Maruhubi, Zanzibar Agosti 24, 2021.

 • Mheshimiwa Spika, Serikali zote mbili zina nia ya dhati na thabiti katika kuhakikisha kuwa, changamoto za Muungano zilizopo na zitakazojitokeza zinashughulikiwa kwa ushirikiano mkubwa kwa lengo la kuendelea kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano wetu. Hivyo, wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali za pande mbili za Muungano kwamba changamoto zilizobakia na ambazo kimsingi zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi zitakamilishwa. Aidha, makubaliano yaliyofikiwa na pande mbili kwa hoja zilizopatiwa ufumbuzi, yatatekelezwa kama ilivyokubalika.
 • Mheshimiwa Spika, hoja za Muungano zinazoendelea kutafutiwa ufumbuzi ni: – Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu; Malalamiko ya Wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili; Kodi ya Mapato yatokanayo na mishahara (Pay As You Earn – PAYE) na Kodi ya Mapato inayozuiliwa (Withholding Tax); Usajili wa Vyombo vya Moto; Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha; Ongezeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO; na Changamoto ya Uingizaji wa sukari katika soko la Tanzania Bara.

        (ii)      Kuratibu Masuala ya Kiuchumi na Kijamii 

Gawio kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

24. Mheshimiwa Spika, Ofisi imeratibu gawio la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo hadi Machi, 2022 Shilingi 27,038,498,469.01 zimepelekwa SMZ. Kati ya Fedha hizo Shilingi 1,400,000,000.00 ni fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo Zanzibar; Shilingi 13,318,640,304.00 nifedha za mapato ya PAYE; Shilingi 2,348,388,513.01 ni fedha za misaada kutoka nje (GBS); Shilingi 9,000,000,000.00 ni gawio la faida ya Benki Kuu; na Shilingi

971,469,652.00 ni gawio la Miamala ya Simu.

Fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo, Zanzibar

25. Mheshimiwa Spika, fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo zimeendelea kutolewa katika Majimbo yote Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kila mwaka kwa ajili ya kuchochea maendeleo. Ofisi ya Makamu wa Rais ilifanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kwa kutumia fedha hizo mwezi Machi, 2022 kwa lengo la kubaini mafanikio na changamoto za utekelezaji na kushauri namna ya kukabiliana nazo. Katika ufuatiliaji huo imebainika kuwa fedha hizo zimesaidia kuibua na kutekelezwa kwa miradi ya kijamii ikiwemo maji, afya, elimu na umeme ambayo imewanufaisha wananchi wa majimbo husika.

Utekelezaji katika Taasisi zinazohusu Muungano 26. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais ilifanya ufuatiliaji wa utekelezaji  katika  Taasisi za Muungano zinazotekeleza masuala ya Muungano. Tathmini ilifanyika ili kubaini mafanikio na changamoto za utekelezaji ambapo Taasisi 20 zilifanyiwa tathmini hiyo ambayo imebainisha kuwa, Taasisi za Muungano zinafanya kazi kwa ufanisi pande zote mbili za Muungano na changamoto zilizopo zimebainishwa na kushauri namna ya kukabiliana nazo.

Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa pande zote mbili za Muungano

 • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwawezesha wananchi wa pande zote mbili za Muungano kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo. Miradi na Programu hizo zimefanikiwa kuinua hali ya wananchi, kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato na kuinua ubora wa maisha na ustawi wa jamii. Miradi hiyo inagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo. 
 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22 miradi na programu zinazotekelezwa pande zote mbili za Muungano ni: Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Mzunguko wa Pili, Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA);Mradi wa Udhibiti wa Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi; Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga; Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo Kame ya Tanzania; Mpango wa Kupanua Usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania; Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia; Mradi wa uboreshaji wa Elimu kupitia “Global Partnership for Education”; na Mradi wa Sumu Kuvu.
 • Kuratibu masuala yasiyo ya Muungano ili kuimarisha ushirikiano kati ya SJMT na SMZ
 • Mheshimiwa Spika, Ofisi imeendelea kuratibu masuala yasiyo ya Muungano kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya pande zote mbili za Muungano. Katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi, 2022, Vikao kumi na nane (18) vya ushirikiano vilifanyika katika sekta za Fedha, Ujenzi na Uchukuzi, Uchumi wa Buluu, Madini, Nishati, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Afya na Maendeleo ya Jamii, Maji, Maliasili, Elimu, Huduma za Sheria, Viwanda, Biashara, Uvuvi na Mifugo.
 • Kutoa Elimu kwa Umma kuhusu Muungano 30. Mheshimiwa Spika, Ofisi imeendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu na faida za Muungano kupitia Redio, Runinga, Magazeti, Jarida la Ofisi ya Makamu wa Rais na Mitandao ya Kijamii. Aidha, Ofisi imeandaa Andiko la Historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu chimbuko, misingi na maendeleo ya Muungano. Andiko hilo litazinduliwa kesho wakati wa madhimisho ya miaka 58 ya Muungano.

HIFADHI NA USIMAMIZI ENDELEVU WA  MAZINGIRA

 • Mheshimiwa Spika, maendeleo ya nchi yetu yanategemea usimamizi endelevu wa mifumo-ikolojia na maliasili zilizopo nchini. Katika kipindi cha mwaka 2021/22 Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu na kusimamia shughuli mbalimbali zinazolenga kuboresha uhifadhi wa Mazingira nchini. Hata hivyo, Nchi yetu inaendelea kukabiliwa na changamoto za kimazingira ambazo ni: uharibifu wa ardhi; ukosefu wa maji safi na salama; upotevu wa makazi ya wanyamapori na bionuai; uharibifu wa mifumo ikolojia ya maji; ukataji holela wa miti; uchafuzi wa mazingira; mabadiliko ya tabianchi; na matumizi yasiyo salama ya bioteknolojia ya kisasa.
 • Mheshimiwa Spika, Uharibifu wa mazingira huathiri afya ya binadamu, mifumo ikolojia na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla. Katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira nchini, Ofisi imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Mikakati, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda na Miradi ya hifadhi ya mazingira. Katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi ya Makamu wa Rais imeweza kutekeleza azma hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama ifuatavyo: –

(i) Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura, 191,

Kanuni za Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Miongozo na Mikakati.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo na kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira, Mhe. David Kihanzile.  Uzinduzi ulifanyika Februari 12, 2022.

Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997

33. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi ya Makamu wa Rais imefanikiwa kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 na kujumuisha maeneo mapya ya kimazingira ambayo ni; kuongezeka kwa viumbe vamizi; taka za kielektroniki; matumizi ya kemikali na bioteknolojia ya kisasa yasiyo salama; kukua kwa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; na uwekezaji katika miradi ya mazingira na masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Sera mpya ya Mazingira ya mwaka 2021 pamoja na mkakati wa utekelezajiwake ilizinduliwa tarehe 12 Februari, 2022 na Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uzinduzi huo ulitanguliwa na zoezi la wiki moja ya kuhamasisha usafi wa mazingira na upandaji miti katika Jiji la Dodoma. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuelimisha wadau mbalimbali kuhusu maudhui ya Sera ya Mazingira ya Mwaka 2021 ili kuwezesha utekelezaji wake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipanda mti katika eneo la wazi Medeli jijini Dodoma Februari 7, 2022 ikiwa ni mojawapo ya shughuli za mazingira kuelekea Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 uliofanywa Februari 12,2022 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191

34. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza maandalizi ya mapitio ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 ili kuakisi matakwa ya Sera ya Mazingira ya mwaka 2021 pamoja na masuala mengine ya Uhifadhi wa Mazingira. Aidha, Ofisi imefanya marekebisho madogo katika Sheria ya Mazingira kwa kufuta Kifungu cha 194 na kukiandika upya ili kupunguza mlolongo wa kufungua mashauri yanaohusiana na ukiukwaji wa Sheria ya Mazingira pamoja na kanuni zake.

Kanuni na Miongozo ya Uhifadhi wa Mazingira

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi ya Makamu wa Rais, imeendelea kuratibu utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 kwa kuandaa na kufanya mapitio ya Kanuni na Miongozo mbalimbali. Kanuni zilizoandaliwa ni pamoja na: Kanuni ya Uhifadhi wa Maeneo Lindwa na Nyeti ya mwaka 2022 ili kuyalinda maeneo husika; Mapitio ya Kanuni ya Marufuku ya Mifuko ya Plastiki ya mwaka 2019 ili kudhibiti matumizi ya lakiri kwenye mifuniko ya chupa; na Mapitio ya Kanuni za Udhibiti wa Kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni ili kupunguza madhara yanayosababishwa na matumizi ya kemikali hizo. 
 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Ofisi iliandaa Mwongozo wa Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira Utokanao na Kelele na Mitetemo wa mwaka 2021 ikiwa ni hatua za kukabiliana na ongezeko la kelele hususan katika maeneo ya mijini. Aidha, Ofisi imeandaa Mwongozo wa Udhibiti wa Taka Ngumu kwa kutumia dhana ya Punguza, Tumia tena na Rejeleza wa mwaka 2021. Lengo la Mwongozo huu ni kupunguza uchafuzi wa mazingira na kutoa fursa kwa jamii kuongeza kipato kutokana na shughuli za urejelezaji wa taka. Kukamilika kwa miongozo hiyo ni hatua muhimu katika kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya athari zitokanazo na uchafuzi wa mazingira.

Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi

37.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Serikali iliandaa Mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi wa Mwaka 2021/22 –

2025/26. Aidha, ili kuungana na jitihada za kimataifa zinazosimamiwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuhimili mabadiliko ya Tabianchi, Serikali iliandaa taarifa ya Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi unaolenga kuiwezesha nchi kuchangia upunguzaji wa uzalishaji wa gesijoto kwa asilimia 30 hadi 35 kupitia sekta za misitu, nishati, usafirishaji na udhibiti wa taka katika kipindi cha kuanzia 2021 hadi 2030.

Kuimarisha usimamizi wa shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira katika Wizara za Kisekta na Mamlaka za Serikali za Mitaa

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea kuimarisha usimamizi wa mazingira katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika kipindi hicho, Ofisi imeratibu vikao viwili (2) vya ngazi ya Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Maji na kupitisha mapendekezo ya hatua za kuchukua katika kuboresha muundo wa usimamizi wa mazingira katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mazingira.  
 • Mheshimiwa Spika, Ofisi imetoa ushauri kwa Wizara za Kisekta kuhusu uandaaji na utekelezaji wa Tathmini ya Mazingira Kimkakati (TMK). Wizara zilizohusika ni: Wizara ya Maji katika mabonde sita (6) ya Maji; Wizara ya Madini; Wizara ya Nishati; Wizara ya Maliasili na Utalii katika Pori la akiba la Selous; na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha katika maeneo ya Kongani za Viwanda.
 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Ofisi iliendelea kujenga uwezo kwa wataalam wa mazingira katika Sekretarieti za Mikoa 26 na Maafisa Mazingira katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 184 kupitia warsha na semina ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira. Maafisa mazingira 40 wamejengewa uwezo katika masuala ya udhibiti na usimamizi wa taka ngumu na taka hatarishi; elimu kuhusu matumizi sahihi ya Zebaki katika shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu; matumizi ya nishati mbadala; mabadiliko ya tabianchi; Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM); na Tathmini ya Mazingira Kimkakati (TMK).  

Wadau mbalimbali wa mazingira kutoka Mkoa wa Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Mhe. Selemani Jafo baada ya kukutana nao Januari 26, 2022, Dodoma.

 • Hifadhi ya Mazingira na mifumo Ikolojia katika Vyanzo vya Maji
 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa Mkakati wa Hifadhi ya Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji 2021 – 2025. Aidha, katika kipindi hicho, Ofisi ilifanya ufuatiliaji katika Halmashauri 25 ili kubaini changamoto za uhifadhi wa mifumo ikolojia. Vilevile, Ofisi imeendelea kuratibu shughuli za Kamati ya Kitaifa ya kuokoa Mifumo Ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu pamoja na eneo la Ihefu. Jukumu la Kamati hii ni kufuatilia utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kuokoa maeneo yaliyoharibika katika Bonde hilo ambalo ni chanzo muhimu cha maji cha Mto Ruaha na ikolojia yake. 
 • Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 katika

Halmashauri 19 zilizopo katika mikoa minne (4) ya nyanda za juu kusini ikiwemo Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa. Changamoto zilizobainika ni pamoja na: uharibifu wa vyanzo vya maji; shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini zisizozingatia kanuni za uhifadhi; uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na kilimo kisicho endelevu; ukataji miti ovyo kwa ajili ya kilimo na mkaa; na ufugaji holela. Aidha, kupitia zoezi hilo Ofisi iliweza kuhimiza Mamlaka katika ngazi za Mikoa na Halmashauri husika kuhamasisha wananchi kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira katika shughuli za kiuchumi. Vilevile, Mamlaka hizo zilielekezwa kutunga na kusimamia Sheria ndogo za uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao.

 • Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira

Udhibiti wa Mifuko ya Plastiki

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea kufuatilia utekelezaji waKatazo la Serikali la tarehe 1 Juni, 2019 la Kupiga

Marufuku Uzalishaji, Uingizaji, Uuzaji, Usambazaji, Usafirishaji nje ya nchi na matumizi ya Mifuko ya Plastiki nchini. Kupitia ufuatiliaji huo, imebainika kuwa matumizi ya bidhaa za plastiki zilizopigwa marufuku hazitumiki tena bali bado ipo changamoto ya vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango vya ubora. Aidha, katika kipindi hicho, Serikali ilipiga marufuku matumizi ya lakiri za plastiki katika vifuniko vya chupa za vinywaji hususan maji zinazozalishwa na kuingizwa nchini ifikapo tarehe 11 Aprili, 2022. Marufuku hiyo inahusu Uzalishaji; Usambazaji; Uingizaji nchini na Utumiaji wa lakiri hizo. Vilevile, katika kutekeleza mabadiliko ya Sheria ya Mazingira, Sura 191 yaliyofanyika mwaka 2021 Ofisi ya Makamu wa Rais imetunga Kanuni za Ufifilishaji makosa yanayohusiana na ukiukwaji wa Sheria ya Mazingira ili kutekeleza matakwa ya Kifungu cha 194 cha Sheria hiyo kwa lengo la kuruhusu makosa hayo kushughulikiwa bila kufungua mashauri mahakamani.

 • Mheshimiwa Spika, ninaomba kupitia Bunge lako Tukufu kuutaarifu umma wa Watanzania hususan wazalishaji, wasambazaji na waingizaji wa vinywaji vinavyotumia chupa zenye lakiri za plastiki kuacha mara moja kwakuwaSerikali itachukua hatua stahiki dhidi ya uchafuzi wa mazingira utokanao na matumizi ya lakiri hizo.

Usimamizi wa Taka Hatarishi na matumizi ya taka kama rasilimali viwandani

45. Mheshimiwa Spika, katikakipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kusimamia uzalishaji, ukusanyaji, usafirishaji  na utupaji wa taka hatarishi  hususan chuma chakavu, mafuta machafu, betri chakavu na taka za kielektroniki kwa mujibu wa Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Taka Hatarishi za Mwaka 2021 na Kanuni za Taka za Kieletroniki za mwaka 2021. Katika kipindi hicho, Ofisi imetoa vibali 270 vya taka hatarishi, na vibali 32 vya taka za kielektroniki kwa makampuni 83 na watu binafsi 46. Kupitia vibali hivyo jumla ya tani 518,207.9 na lita 977,458 za taka hatarishi zimeondolewa kwenye mazingira. Aidha, katika kurahisisha utekelezaji na kuongeza wigo wa wadau wanaojishughulisha na shughuli za urejelezaji wa taka hatarishi, Ofisi imetafsiri Kanuni za Usimamizi na Udhibiti wa Taka Hatarishi za Mwaka 2021 na Kanuni za Usimamizi na Udhibiti wa Taka za

Kielekitroniki za Mwaka 2021 kwa lugha ya Kiswahili. 

Kuratibu utekelezaji wa Mpango – Kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini 

46. Mheshimiwa Spika, Ofisiimeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango – Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu nchini. Aidha,Ofisi imetoa elimu kuhusu hifadhi ya mazingira na madhara yatokanayo na matumizi ya zebaki katika shughuli za wachimbaji wadogo wapatao 2,200 katika maeneo 22 ya wachimbaji kutoka mikoa 10 ya kimadini ikiwa ni pamoja na Mara, Shinyanga, Geita, Kahama, Mbeya, Katavi, Tanga, Tabora, Singida na Dodoma.Vilevile, Ofisi imetoa elimu kwa wanahabari 50 kutoka vyombo vya habari 10 vikiwemo runinga, magazeti, redio na mitandao ya kijamii; viongozi 29 wa vyama vya wachimbaji wadogo; na Maafisa wandamizi 46 kutoka Wizara za kisekta na Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi na udhibiti wa kemikali. Pia, Ofisi imeshirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara na watumiaji 33 wa kemikali za viwandani na migodini.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bw. Edward Nyamanga akifungua Warsha ya Uhamasishaji wa Utekelezaji wa Mpango – kazi kitaifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwenye Uchimbaji mdogo wa Dhahabu (2020-25) iliyofanyika Dodoma Machi 15, 2022.

Kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira katika Migodi, Viwanda na Madampo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo (wa tatu kushoto) akisikiliza maelezo kuhusu mradi wa dampo la kisasa la Chidaya jijini Dodoma kutoka kwa Meneja wa dampo hilo, Bw. John Kiwanga, alipofanya ziara Septemba 3, 2021.

47. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi za Kisekta imefanya kaguzi 15 katika migodi iliyopo mikoa ya Shinyanga, Mara, Geita, Ruvuma, Mbeya na Dodoma. Aidha, ukaguzi ulifanyika katika viwanda nane (8) kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza kwa lengo la kuhimiza uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira Sura, 191. Vilevile, ukaguzi wa usimamizi na uteketezaji wa taka ngumu umefanyika katika madampo ya Chidaya – Dodoma, Pugu Kinyamwezi – Dar Es Salaam, Muriet Arusha na Mpirani – Tanga. Changamoto zilizobainika ni pamoja na kutiririsha majitaka katika mazingira; uchafuzi wa hewa; matumizi yasiyo salama ya kemikali katika kuchenjua dhahabu kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu; ukataji wa miti ovyo kwa ajili ya kuimarisha mashimo ya wachimbaji wadogo; na usimamizi hafifu wa taka ngumu ikiwemo uchomaji holela wa taka. 

        (iv)     Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi

Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22 Ofisi imeendelea kuratibu shughuli mbalimbali zenye lengo la upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi. Kazi zilizofanyika ni pamoja na; kutoa mafunzo kuhusu utafutaji fedha kwa ajili ya miradi ya kuhimili mabadiliko ya Tabianchi, uandaaji wa mipango katika ngazi ya jamii inayozingatia kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi; kuratibu Taasisi za Serikali na zisisizo za Serikali zikiwemo UNDP, Foreign Commonwealth Development Organisation – FCDO, Climate Action Network in Tanzania – CANTZ, Forum CC, Care International -Tanzania, Gender and Climate Change Tanzania Coalition (GCCTC), Research and Poverty Alleviation – REPOA zenye nia ya kutafuta fedha kupitia mifuko mbalimbali ya mabadiliko ya Tabianchi duniani. Aidha, Ofisi kwa kushirikiana na Kituo cha Kitaifa Cha Uratibu wa Hewa Ukaa na UNDP ilishiriki kutoa mafunzo kwa wataalam 55 kutoka taasisi za Serikali na Sekta binafsi Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kuhusu ukusanyaji wa Taarifa za Gesijoto, Mfumo wa

Upimaji, Ufuatiliaji na Uhakiki.

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea kuratibu wadau wanaolenga kuanzisha miradi inayohusu biashara ya hewa ukaa kwa mfumo wa mkopo wa hewa ukaa (Carbon Credit). Aidha, katika kipindi hicho, Ofisi imeratibu Kampuni moja (1) iliyowekeza na Mashirika matatu (3) yenye nia ya kuwekeza katika biashara ya hewa ukaa. Vilevile, Ofisi imeanza kuandaa Kanuni na Mwongozo wa kusimamia biashara ya hewa ukaa nchini katika maeneo ya hifadhi ya hewa ukaa ikiwemo rasilimali za misitu, maji na ardhi.

Kuimarisha Miundombinu ya Fukwe ili kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi zitokanazo na ongezeko la kina cha bahari 

 • Mheshimiwa Spika, Ofisi imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko yaTabianchi ikiwa ni pamoja na Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Katika kipindi hicho, Ofisi imefanya kazi mbalimbali ikiwemo kufanya tathmini ya uharibifu wa fukwe unaosababishwa na kuongezeka kwa kina cha maji katika ukanda wa Bahari katika maeneo ya Mikadi Beach na Ndege Beach – Dar Es Salaam; Mikindani – Mtwara; na fukwe za Msuka na Sipwese zilizopo Micheweni Pemba. Aidha, tathmini zimefanyika katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria.
 • Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na uharibifu wa fukwe katika bahari unaotokana na mmomonyoko, Ofisiimekamilisha maandalizi ya miradi yenye lengo la kukabiliana na mmomonyoko wa fukwe hizo katika maeneo ya Mikindani Mtwara na Sipwese Pemba. Miradi hii inalenga kujenga kuta za bahari katika maeneo ya Mikindani Mtwara (mita 1,750) na Sipwese Pemba (mita 500). Miradi hiyo inatekelezwa kwa fedha za ndani na inakadiriwa kugharimu Shilingi Bilioni 4.4 itakapokamilika. Serikali inaendelea kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine ya aina hiyo katika maeneo ya fukwe mbalimbali nchini. 

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Dezo Construction Co. Ltd Bw. Premji Pindoria wakisaini mkataba wa ujenzi na ukarabati wa kingo za fukwe katika maeneo ya mwambao wa Mikindani (Mtwara) hafla iliyofanyika Machi 31, 2022 wanaoshuhudia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Dustan Shimbo na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi.

Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi 

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea kuratibu shughuli za Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi uliopo chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi. Katika kipindi hiki Tanzania imefanikiwa kupata mradi wa Dola za Marekani milioni 100 kupitia benki ya CRDB kwa ajili ya kujenga uwezo wa kiteknolojia wa kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi katika sekta ya kilimo. Mradi huu utawezesha Benki ya CRDB kukopesha wakulima kwa riba nafuu ili kutekeleza miradi ya kilimo cha kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi.  Aidha, natoa rai kwa wakulima na wadau wengine kuchangamkia fursa hii. 

(v) Kukabiliana na changamoto za Uhifadhi na

Usimamizi wa Mazingira 

Kampeni ya Upandaji Miti milioni 1.5 kwa Kila Halmashauri kwa Mwaka

53. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea kuratibu utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji na utunzaji wa miti inayotekelezwa nchini kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka. Katika kipindi cha mwaka 2020/21, idadi ya miti iliyopandwa ni 202,923,907 na iliyostawi ni 165,501,119 sawa na asilimia 81.6. Halmashauri 27 kati ya 184 zilivuka lengo la kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka. Napenda kutumia fursa hii kuzipongeza Halmashauri zilizofikia lengo na kuzitaka Halmashauri zote ambazo hazikufikia lengo kuchukua hatua za makusudi ili kunusuru Wilaya zao na athari zitokanazo na uharibifu wa ardhi na vyanzo 

vya maji.  Nitoe rai kwa wananchi na wadau kuongeza kasi ya upandaji miti katika maeneo yao na kushauri Mamlaka zote za Serikali za Mitaa kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria ndogo zinazohusu uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao.

Kampeni ya Kukijanisha Dodoma 

54. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea kuratibu utekelezaji wa Kampeni ya Kukijanisha Dodoma. Katika kipindi hicho, Jumla ya miti 692,247 ilipandwa katika wilaya zote za Mkoa wa Dodoma kama ifuatavyo: Dodoma Mjini miti 584,790; Wilaya ya Mpwapwa miti 21,450; Wilaya ya Bahi miti 20,720; Wilaya ya Chemba miti

4,000; Wilaya ya Kongwa miti 45,587; Wilaya ya Kondoa miti 11,200; na Wilaya ya Chamwino miti 4,500. Aidha, napenda pia kutoa wito kwa Jiji la Dodoma, TFS na wadau wengine kuongeza kasi katika utekelezaji wa mpango wa kukijanisha Dodoma ili kutimiza azma ya Serikali ya kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la kijani.

Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira 

55. Mheshimiwa Spika, kufuatia uwepo wa changamoto mbalimbali za mazingira nchini kama ilivyoainishwa katika taarifa ya Hali ya Mazingira ya Mwaka 2019, katika kipindi cha Mwaka 2021/22 Ofisi inaandaa Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira (Master Plan of Environmental Interventions) wenye lengo la kuibua changamoto za kimazingira kwa kuzingatia tofauti za kimaeneo utakaoambatana na Mpango Kazi wa utatuzi wa changamoto hizo. Mpango huo utatumika kama mwongozo wa uibuaji na utekelezaji wa miradi yote ya mazingira nchini.

Mpango huu unatarajiwa kuzinduliwa mwezi Juni, 2022.

Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira

56. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22 Ofisi imeendelea kutekeleza Kampeni Kabambe ya Kitaifa ya Uhifadhi na Usafi wa Mazingira iliyozinduliwa na Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 5 Juni, 2021 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani. Kampeni hiyo imelenga kuongeza ushiriki wa jamii na uwajibikaji wa mamlaka za usimamizi wa hifadhi na usafi wa mazingira ili kuchangia katika ustawi wa jamii na maendeleo endelevu. Katika kipindi hiki Ofisi imeandaa Mpango – Kazi wa utekelezaji wa Kampeni kabambe wa mwaka 2021 – 2025. Aidha, kupitia kampeni hiyo, Ofisi kwa kushirikiana na Mabalozi wa Mazingira, Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wadau mbalimbali imeendelea kuhamasisha usafi wa mazingira, upandaji miti, matumizi ya nishati mbadala, na hifadhi ya mazingira ya vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali nchini. Nitumie fursa hii kuwashukuru Mabalozi wa mazingira kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhamasisha uhifadhi na usafi wa mazingira nchini. Ni matumaini yangu kuwa wataendelea kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kufanya usafi na kutunza mazingira katika maeneo yetu.

Kampeni ya Soma na Mti

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22 Ofisi imeendelea kuhamasisha upandaji miti kupitia Kampeni ya “Soma na Mti” niliyoizindua tarehe 20 Januari, 2022 katika Jiji la Dodoma. Kampeni hiyo imelenga kujenga tabia kwa wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo nchini kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti.

Aidha, Kampeni imeendelea kuhamasishwa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya; na Mabalozi wa

Mazingira katika mikoa mbalimbali nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipanda mti na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma wakati alipozindua Kampeni ya upandaji wa miti kwa wanafunzi wa shule na vyuo jijini Dodoma Januari 20, 2022. Kampeni hiyo inafahamika kama ‘Soma na Mti’.

        (vi)        Elimu kwa Umma Kuhusu Uhifadhi wa

Mazingira

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa  uhifadhi na usimamizi wa mazingira kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii; warsha na semina, kampeni; hotuba za viongozi; na maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kuhusu mazingira.Elimu iliyotolewa ilihusu: Sera, Sheria na Kanuni za usimamizi wa mazingira; mabadiliko ya tabianchi; matumizi ya nishati mbadala; uhifadhi wa tabaka la Ozoni; usimamizi wa matumizi ya zebaki katika shughuli za wachimbaji wadogo; viumbe vamizi; hifadhi ya bionuai; mikataba ya kikanda na kimataifa ya mazingira; Upandaji miti; udhibiti wa taka na usafi wa mazingira katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; hifadhi ya vyanzo vya maji; hifadhi ya mazingira ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi; katazo la mifuko ya plastiki; na matumizi ya nishati mbadala.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akijumuika na viongozi na wadau wa mazingira kushiriki zoezi la usafi wa mazingira katika ufukwe wa Feri Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam Machi 26, 2022.

 • Mheshimiwa Spika, elimu hiyo imeongeza hamasa kwa wadau kushiriki katika masuala ya hifadhi na usimamizi wa mazingira hususan upandaji miti, usafi wa mazingira na utekelezaji wa marufuku ya mifuko ya plastiki.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea na Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayotarajiwa kufanyika tarehe 5 Juni 2022. Madhumuni ya maadhimisho haya ni kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira na fursa zilizopo kwa ustawi wa jamii ya sasa na kizazi kijacho.  
 • Mheshimiwa       Spika,    kwa        mwaka   2022 maadhimisho       ya   Siku       ya   Mazingira      Duniani, Kimataifa yatafanyika nchini Sweden na Kauli Mbiu ya maadhimisho hayo ni: “Dunia ni moja, tujali mazingira yetu”.  Aidha, Kilele cha maadhimisho haya kitaifa kinatarajiwa kufanyika Jijini Dodoma. Katika maadhimisho hayopamoja na mambo mengine Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira utazinduliwa.

Maadhimisho ya Siku ya Kuhifadhi Tabaka la Ozoni Duniani

62. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22 Ofisi iliratibu maadhimisho ya Siku ya Ozoni Duniani yaliyokuwa na Kauli Mbiu ya “Montreal Protocol – Keeping us, our food and vaccines cool” ambayo huadhimishwa tarehe 16 Septemba kila mwaka. Kitaifa maadhimisho hayo yalifanyika Jijini Dodoma yakiongozwa na Kauli Mbiu isemayo: “Tulinde Afya ya binadamu, hifadhi ya chakula na kuhakikisha chanjo za UVIKO 19 zinakuwa salama”. Katika maadhimisho hayo shughuli zilizofanyika ni pamoja na: kutoa tamko la Serikali kuhusu maadhimisho ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni; kukagua karakana zinazojishughulisha na matengenezo ya majokofu na viyoyozi vya magari na majumbani katika majiji ya Dodoma na Dar Es Salaam kwa lengo la kuhamasisha uzingatiaji wa Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni za mwaka 2007; kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda Tabaka la Ozoni kupitia vipindi sita (6) vya redio na vipindi viwili (2) vya Runinga; na kutoa mafunzo kwa maafisa forodha na wataalam kumi na tisa (19) kutoka Mamlaka za Usimamizi wa Kemikali kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni. Vilevile, mafunzo maalum yalitolewa kwa mafundi mchundo 40 wanaojishughulisha na utengenezaji wa majokofu na viyoyozi.

(vii) Ushiriki wa Nchi Katika Mikutano ya

Kikanda na Kimataifa ya Hifadhi na

Usimamizi wa Mazingira

Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi

63. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi iliratibu ushiriki wa ujumbe wa

Tanzania katika Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Glasgow, Uskochi (Scotland) kuanzia tarehe 25 Oktoba hadi 12 Novemba, 2021 ambapo Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na ulishiriki katika Masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano huo ambayo ni pamoja na: Uhimili wa athari za mabadiliko ya tabianchi; Upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi; Upatikanaji na uhawilishaji wa teknolojia; Kujenga uwezo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; Utafiti na sayansi ya mabadiliko ya tabianchi; Upunguzaji wa gesi-joto; na Athari za sera za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Tanzania iliwasilisha andiko la mchango wa nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Nationally Determined Contribution).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia katika Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP26 uliofanyika katika Mji wa  Glasgow, Scotland tarehe 02 Novemba, 2021.

Mkutano wa Tano wa Nchi Wanachama wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira

64. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi iliratibu ushiriki wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tano wa Nchi Wanachama wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira uliofanyika tarehe 28 Februari – 04 Machi 2022 Nairobi, Kenya. Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Masuala muhimu yaliyopitishwa na nchi wanachama katika mkutano huo ni pamoja na: kuanzishwa kwa Mkataba wa udhibiti wa uchafuzi wa mazingira utokanao na taka za plastiki; kuweka mikakati ya hifadhi ya bionuai na athari za mabadiliko ya Tabianchi; na upatikanaji wa rasilimali fedha na kujenga uwezo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za mazingira. Katika mkutano huo, Tanzania iliahidi kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na changamoto za mazingira zinazoikabili dunia.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akitoa salamu za Tanzania kwa niaba ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano maalum wa miaka 50 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) uliofanyika Machi 3, 2022 jijini Nairobi, Kenya.

 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis (kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe.

Dkt. John Simbachawene wakishiriki ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la

Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA 5) Nairobi nchini Kenya

Mkutano wa Tisa wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika

65. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tisa wa Mawaziri wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika uliofanyika katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji tarehe 16 Desemba, 2021 ambao ulishirikisha nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo, Zambia na Tanzania. Mgeni rasmi katika Mkutano huo alikuwa ni Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Masuala muhimu yaliyojadiliwa na kupitishwa katika mkutano huo ni pamoja na kuanzisha taratibu mahsusi za kikanda za uvuvi endelevu katika Ziwa Tanganyika; na kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya kitaifa na kikanda ya usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika. Aidha, katika mkutano huo Tanzania ilikabidhiwa uenyekiti wa nchi wanachama kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Desemba, 2021 hadi Desemba, 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza wakati wa ufunguzi Mkutano wa Tisa wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika uliofanyika mkoani Kigoma.

(viii) Utekelezaji wa Miradi ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira

66. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea kuratibu utekelezaji wa miradi ya hifadhi na usimamizi wa mazingira. Katika kipindi hicho jumla ya miradi nane (8) ilitekelezwa kama ifuatavyo: –

Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi Kupitia Mifumo Ikolojia

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi iliendelea kutekeleza Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi Kupitia Mifumo Ikolojia unaotekelezwa katika Wilaya za Mvomero,

Simanjiro, Kishapu, Mpwapwa na Kaskazini A Unguja, Zanzibar. Lengo la mradi ni kuongeza uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii za vijijini nchini Tanzania. Katika kipindi hiki, kiasi cha Shilingi 1,880,662,028 kilitumika. 

Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza Usalama wa Chakula katika maeneo kame ya Tanzania

 • heshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea kutekeleza Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame nchini katika Wilaya za Magu (Mwanza), Nzega (Tabora), Mkalama (Singida), Kondoa (Dodoma) na Micheweni (Pemba), Zanzibar. Lengo la mradi ni kuboresha mifumo – ikolojia ili kuongeza usalama wa chakula katika maeneo husika. Katika Kipindi hicho,kiasi cha Shilingi 1,040,000,000 kilitumika. 

Mradi wa Majaribio wa Kikanda wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Bonde la Ziwa Victoria 

69. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi iliendelea kutekeleza mradi wa Majaribio wa Kikanda wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Bonde la Ziwa Victoria katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza. Lengo la mradi huu ni kuwezesha jamii zinazoishi katika maeneo ya Ziwa Victoria kuweza kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo yao.  Katika kipindi hicho, kiasi cha Shilingi 439,274,405 kilitumika. 

Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai katika mifumo ikolojia ya Bonde la Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa

70. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeanza kutekeleza Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na Urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai katika mifumo ikolojia ya Bonde la Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa. Lengo la mradi ni kuimarisha usimamizi jumuishi wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibiwa ili kujenga uhimilivu wa mifumo – ikolojia na jamii kwa ujumla nchini Tanzania. Mradi huu utatekelezwa katika Wilaya za Iringa Vijijini, Mbeya Vijijini, Mbarali, Wanging’ombe, Tanganyika, Mpimbwe na Sumbawanga Vijijini. Jumla ya Shilingi 643,619,178.76 zilitumika.  

Mradi wa Kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Mkataba wa Stockholm Unaohusu Kemikali zinazodumu katika Mazingira kwa Muda Mrefu 71. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi imeendelea kuratibu Mradi wa

Kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Mkataba wa Stockholm Unaohusu Kemikali zinazodumu kwenye Mazingira kwa Muda Mrefu.

Lengo la mradi ni kulinda afya ya binadamu na mazingira kutokana na athari za kemikali zinazodumu kwenye mazingira kwa muda mrefu. Kiasi cha Shilingi 248,646,090 kimetumika. 

Mradi     wa Kupunguza Hewa     Ukaa inayosababishwa na Ukataji na Uharibifu wa Misitu nchini

72. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Ofisi iliendelea kutekeleza Mradi wa Kupunguza Hewa Ukaa inayosababishwa na Ukataji na Uharibifu wa Misitu nchini. Lengo la mradi ni kuiwezesha Tanzania kuwa tayari katika utekelezaji wa makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi na kunufaika na biashara ya hewa ukaa. Kiasi cha Shilingi 279,045,948.87 kimetumika. 

Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kitaasisi wa utekelezaji wa Itifaki ya Montreal Kuhusu Udhibiti wa Kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni 73. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22,     Ofisi imeendelea   kutekeleza    Mradi unaolenga kujenga Uwezo wa   Kitaasisi        wa utekelezaji wa Itifaki ya Montreal Kuhusu Udhibiti wa Kemikali    zinazomong’onyoa      Tabaka la Ozoni ambapo kiasi cha Shilingi 102,590,610 kilitumika.

Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kitaasisi wa Kutekeleza Sheria ya Usimamizi wa Mazingira

74. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka

2021/22, Ofisi iliendelea kutekeleza Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kitaasisi wa Kutekeleza Sheria ya Usimamizi wa Mazingira nchini. Lengo la mradi ni Kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa kusimamia utekelezaji na uzingatiaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 ambapo kiasi cha Shilingi 641,900,000 kimetumika.

MASUALA YA UTAWALA NA MAENDELEO YA WATUMISHI

 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22 Ofisi imeendelea kusimamia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maadili ya Utumishi wa Umma na imewezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Aidha, utendaji kazi wa watumishi umeendelea kupimwa kwa kutumia mfumo wa wazi wa Tathmini na Mapitio ya Utendaji Kazi (OPRAS).
 • Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho jumla ya watumishi 94 wamewezeshwa kuhudhuria mafunzo mbalimbali ili kuwajengea uwezo na kuongeza ujuzi na maendeleo kulingana na kada zao ambapo watumishi 10 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na watumishi 84 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi. Aidha, katika kuendelea kuboresha mazingira ya kazi, Ofisi imenunua vitendea kazi kwa ajili ya watumishi, ukarabati wa Makazi ya Makamu wa Rais yaliyoko Kilimani – Dodoma na kuanza ujenzi wa Ofisi ya kudumu ya Makamu wa Rais awamu ya pili Mtumba Dodoma. 

CHANGAMOTO NA MIKAKATI ILIYOPO 

 • Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo: Kuendelea kuwepo kwa hoja za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi; kutotekelezwa kikamilifu kwa Mfumo wa Kitaasisi wa Usimamizi wa Mazingira katika ngazi ya Sekta na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191; uelewa mdogo wa jamii kuhusu masuala ya Muungano na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira; uzingatiaji mdogo wa jamii kuhusu sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi wa mazingira; na kuongezeka kwa madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya Tabianchi.
 • Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizi, hatua zifuatazo zimechukuliwa:- kuandaa Andiko la Historia ya Muungano litakalotumika kuelimisha umma kuhusu faida za Muungano kiuchumi, kijamii na kisiasa; kuendelea kutafuta ufumbuzi wa hoja za Muungano ambazo hazijatatuliwa; kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhusu kuimarisha muundo wa

Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuratibu shughuli za uhifadhi na usimamizi wa mazingira;kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Kujenga Uwezo wa Utekelezaji wa Sheria ya Mazingira, Sura 191 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa kitaasisi wa usimamizi wa mazingira katika Wizara za Kisekta na Mamlaka za Serikali za Mitaa; kuendelea na majadiliano na Wizara za Kisekta kuhusu kuimarisha uratibu wa masuala ya mazingira katika sekta husika; na kuendelea kukuza uelewa wa jamii kuhusu Masuala ya Muungano, Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.

BARAZA LA TAIFA LA HIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA (NEMC)

79. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira limendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191, Mpango Mkakati wa Baraza 2021/22 – 2025/26, miongozo na mikakati mingine ya kitaifa ya kuhifadhi mazingira ili kuleta maendeleo endelevu hapa nchini.

        (v)         Uzingatiaji na Usimamizi wa Sheria ya

Mazingira Sura 191  

Ukaguzi wa Maeneo ya Uwekezaji na Mazingira

 • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, Baraza limefanya kaguzi katika miradi 2,455 kwa dhumuni la kutathimini uzingatiaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 na Kanuni zake. Changamoto kubwa za kimazingira zilizobainika kufuatia kaguzi hizo ni: utiririshaji wa majitaka kwenye mazingira ikiwemo vyanzo vya maji na makazi ya watu; Matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za misitu ya asili kwa ajili ya nishati na ujenzi; Ukosefu wa  mifumo ya kuhifadhi, kurejeleza na kuteketeza taka ngumu na taka hatarishi; Uzalishaji wa hewa chafu; Uzalishaji na usambazaji wa mifuko mbadala isiyokidhi viwango; Upigaji  wa kelele na mitetemo zaidi ya viwango vinavyoruhusiwa kikanuni; na uchafuzi wa mazingira katika masoko na machinjio. Changamoto hizi pamoja na mambo mengine zinatokana na kutozingatiwa kwa sheria, kanuni, miongozo na taratibu za Mipango Miji.
 • Mheshimiwa Spika, Hatua zilizochukuliwa kutokana na changamoto hizo ni pamoja na kutoa ushauri, maelekezo, onyo na amri ya kizuizi kwenye shughuli zenye madhara makubwa kwa mazingira, amri za urejeshaji wa mazingira na faini. Jumla ya miradi 2,105 ilipewa ushauri na maelekezo, miradi 350 ilipewa amri ya kizuizi kulinda mazingira. Hatua hizi zimesaidia kulinda afya ya binadamu, viumbe hai na mazingira.  
 • Mheshimiwa Spika, Baraza limepokea malalamiko kuhusu uchafuzi wa mazingira na kuyapatia ufumbuzi kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 na Kanuni zake. Katika kipindi hicho, jumla ya malalamiko 369 yalipokelewa. Malalamiko hayo yalihusu kelele kutoka kwenye kumbi za starehe na mitetemo, utiririshaji majitaka na uchafuzi wa hewa kutoka viwandani, utupaji holela wa taka ngumu, uchimbaji wa mchanga katika vyanzo vya maji na maeneo mengineyo. Malalamiko 359 yalishughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa sheria ikiwemo kutoa ushauri, maelekezo, onyo na amri mbalimbali za kimazingira. Jumla ya malalamiko 300 yalitatuliwa kupitia ushauri na maelekezo na malalamiko 59 kutatuliwa kupitia maonyo na amri mbalimbali za kimazingira. Aidha, Baraza limeendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Jeshi la Polisi kushughulikia malalamiko hayo.

Udhibiti wa Taka Hatarishi 

83. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Baraza limepokea maombi 36 ya usimamizi wa uteketezaji wa taka hatarishi ikiwa ni pamoja na dawa na bidhaa za viwandani zilizokwisha muda wake na kemikali zisizofaa kwa matumizi. Kiasi cha tani 660 za taka hizo zimeteketezwa kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

        (vi)     Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) 

Usajili wa Miradi na Utoaji wa Vyeti vya Mazingira

84. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, Baraza lilisajili jumla ya miradi 1,702 ambapo miradi 339 ilisajiliwa kwa njia ya kawaida yaani kuwasilisha nakala ngumu na miradi 1,363 ilisajiliwa kwa mfumo wa ki-elektroniki. Kati ya hiyo, miradi 967 ni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na Miradi 735 ni ya Ukaguzi wa Mazingira. Aidha, katika kipindi hicho jumla ya miradi 731 imeidhinishwa na kupata vyeti vya mazingira,sawa na ongezeko la asilimia 23 ikilinganishwa na mwaka 2020/21. Kati ya miradi hiyo iliyopata vyeti, miradi 573 ni ya TAM na Miradi 158 ni ya Ukaguzi wa Mazingira. Aidha, miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za upembuzi. Ongezeko hili limetokana na matumizi ya mfumo wa kielektroniki unaotumika katika utoaji wa vyeti.

Usajili na uhakiki wa Wataalam Elekezi wa Mazingira

85. Mheshimiwa Spika, Baraza limeendelea kusimamia utendaji kazi wa Wataalam Elekezi na Kampuni za Ushauri ili waweze kutoa ushauri wa masuala ya mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191. Vile vile, daftari la wataalam elekezi waliosajiliwa na Baraza na wenye sifa za kufanya kazi za TAM na Ukaguzi wa Mazingira limeendelea kuhuishwa. Jumla ya wataalam elekezi 164 wa TAM na 102 wa ukaguzi wa Mazingira pamoja na kampuni za ushauri 70 za TAM na 51 za ukaguzi wa mazingira ziko hai katika utoaji wa huduma ya utalaam elekezi. 

        (vii)         Elimu kwa Umma Kuhusu Hifadhi ya

Mazingira

Kukuza Uelewa na Kujenga Uwezo wa Wadau Kuhusu Hifadhi ya Mazingira

86. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2021/22, Baraza limetoa elimu ya mazingira kupitia vyombo vya habari ili kujenga uelewa kwa jamii kuhusu masuala ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Aidha, Baraza lilishiriki katika maadhimisho mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya mazingira kwa Jamii. 

MALENGO NA MAOMBI YA FEDHA ZA MATUMIZI YA KAWAIDA NA MAENDELEO KWA MWAKA 2022/23

MASUALA YA MUUNGANO

(i) Kuratibu Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano

87. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/23, Ofisi itaendelea Kuratibu utatuzi wa changamoto zilizobakia na zitakazojitokeza katika utekelezaji wa masuala ya Muungano kupitia Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano. Vikao hivi vitafanyika katika ngazi tatu (3) ambazo ni: – Kamati ya Pamoja; Mawaziri; na Makatibu Wakuu. Aidha, kutakuwa na Vikao vya Kamati Ndogo za Fedha, Uchumi na Biashara na Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala vitakavyofanyika kulingana na mahitaji. Vikao hivyo vitaratibiwa na Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ.

 • Kuratibu Masuala ya Kiuchumi na Kijamii  88. Mheshimiwa Spika, Ofisi itaendelea kuratibu masuala ya kiuchumi na kijamii kwa kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa pande mbili za

Muungano ikiwa ni pamoja na kuratibu utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kwa fedha za Kuchochea Mfuko wa Jimbo, Zanzibar. Aidha, Ofisi itatoa mafunzo ya usimamizi wa miradi inayogharamiwa na fedha za mfuko wa jimbo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na wataalamu katika Halmashauri za Zanzibar.  

 • Kuratibu masuala yasiyo ya Muungano ili kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

89. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/23, Ofisi itaendelea na uratibu wa masuala yasiyo ya Muungano kupitia vikao vya ushirikiano vya Wizara, Idara na Taasisi za SJMT na SMZ zisizo za Muungano zenye majukumu yanayoshabihiana.

 • Kutoa Elimu ya Muungano kwa Umma 90. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/23, Ofisi itaendelea kutoa elimu ya Muungano kwa umma kwa makundi tofauti ya kijamii kupitia njia mabalimbali ikiwemo kupitia Redio, Runinga, Magazeti, Jarida la Ofisi ya Makamu wa Rais na Mitandao ya Kijamii kwa lengo la kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano wetu.
 • Kuratibu utekelezaji wa masuala 22 ya Muungano

91. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/23, Ofisi itaendelea kuratibu utekelezaji wa masuala 22 ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 4(3) kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ambapo pamoja na mambo mengine, Ofisi inatakiwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa mambo ya Muungano na kuchukua hatua kwa changamoto zinazobainika.

HIFADHI NA USIMAMIZI ENDELEVU WA MAZINGIRA

 • Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha  hifadhi endelevu ya mazingira, kwa mwaka 2022/23, Ofisi imepanga kutekeleza vipaumbele sita (6) vifuatavyo:Kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021; Kuratibu utekelezaji wa Mpango Kabambe wa hifadhi ya Mazingira; kufanya mapitio ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191; kuratibu utekelezaji wa Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira; kuendelea kujenga uwezo kwa jamii katika kukabiliana na athari za  mabadiliko ya Tabianchi; na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.                                
 • Kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 
 • Mheshimiwa Spika,katika kipindi cha Mwaka 2022/23, Ofisi itaendelea kusimamia, kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na Mikakati mbalimbali ya Hifadhi ya Mazingira katika sekta na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
 • Kuratibu utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191
 • Mheshimiwa Spika, Ofisi itaendelea kuratibu utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 katika Wizara za Sekta na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Ofisi itaratibu mapitio ya Sheria hiyo ili kuzingatia matakwa ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na kuandaa kanuni na miongozo mbalimbali ya utekelezaji wake. Vilevile, Ofisi itaendelea kuchambua maombi na kutoa vibali vya mazingira ikiwa ni pamoja na vibali vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM); Ukaguzi wa Mazingira; Tathmini ya Mazingira Kimkakati (TMK); na taka hatarishi ikiwemo taka za kielektroniki.  
 • Utekelezaji wa Mpango Kabambe wa hifadhi ya Mazingira
 • Mheshimiwa Spika, Ofisi itaanza utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira kupitia miradi inayotekelezwa na kuibua miradi mipya ya Hifadhi ya Mazingira katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, katika utekelezaji wa mpango huu, mwongozo kuhusu utekelezaji wa miradi ya mazingira nchini utatolewa.
 • Kuratibu       utekelezaji   wa Kampeni

Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira 96. Mheshimiwa Spika, Ofisi itaendelea kuratibu utekelezaji wa kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira kwa kuhamasisha wadau mbalimbali kuongeza kasi ya upandaji miti, uhifadhi wa vyanzo vya maji, udhibiti wa taka ngumu na taka hatarishi, uzalishaji endelevu viwandani, kuongeza matumizi ya nishati mbadala, udhibiti wa viumbe vamizi, kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi, uchimbaji endelevu wa madini, kilimo, ufugaji na uvuvi endelevu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza na Mkuu wa Jershi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Rajabu Mabele pamoja na Mkuu wa Kikosi namba 834 JKT Makutupora, Dodoma, Luteni Kanali Festo Mbanga wakati alipokuwa akitoa maagizo ya upandaji miti pembezoni mwa barabara ya kuingia jiji la Dodoma Machi 26,2022.

 • Kuratibu utekelezaji wa Mpango – Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu Nchini

(2020 – 2025)

 • Mheshimiwa Spika, Ofisi itaendelea kutoa elimu kuhusu athari za Zebaki na kuhamasisha matumizi salama ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu. Aidha, Ofisi itaendelea kushirikiana na Mamlaka za udhibiti kuimarisha udhibiti wa uingizaji zebaki nchini ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa wa Mamlaka hizo. 

        (vi)     Elimu kwa Umma

 • Mheshimiwa Spika, Ofisi itaendelea kutoa elimu kuhusu Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na: vyombo vya habari na mitandao ya kijamii; maadhimisho ya Kitaifa na Kimataifa ya Mazingira; ziara za Viongozi; Mabalozi wa Mazingira; semina na warsha; makongamano; machapisho; matangazo; na maonesho. Aidha, Ofisi itaendelea kutekeleza Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira inayolenga kutoa elimu na kuhamasisha umma kushiriki katika shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira. Vilevile, Ofisi itaendelea kutekeleza Kampeni ya Soma na Mti inayolenga kujenga tabia ya kupanda na kutunza miti kwa wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo. 
 • Mheshimiwa Spika, masuala mengine yatakayotekelezwa ni pamoja na: – Kuhifadhi Mazingira ya Vyanzo vya Maji; udhibiti wa taka ngumu;kuendelea kuratibu utekelezaji wa Mikataba ya Kikanda na kimataifa ya hifadhi na usimamizi wa mazingira na Itifaki zake; kuratibu maadhimisho ya siku ya mazingira duniani; na kuendelea kufuatilia Kampeni ya Kitaifa ya upandaji miti milioni 1.5 kwa mwaka kwa kila Halmashauri, na Kampeni ya Kukijanisha Dodoma.

(vii) Kuratibu Utekelezaji wa Miradi ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira 

100. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2022/23,Ofisi itaratibu utekelezaji wa miradi ya hifadhi na

usimamizi wa mazingira kama ifuatavyo: –

Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa

101. Mheshimiwa Spika, Mradi huu utagharimu Shilingi 2,987,654,000.00 na unatekelezwa katika Wilaya za Ludewa na Makete (Njombe), Kyela (Mbeya), Nyasa na Mbinga (Ruvuma).  Lengo la Mradi ni kuhifadhi mazingira ya bonde la Ziwa Nyasa na kuboresha hali ya maisha ya jamii inayozunguka eneo hilo. Katika mwaka 2022/23, Shilingi 736,967,714.00 zimetengwa kwa ajili ya kuwezesha shughuli mbadala za kiuchumi kwa jamii ili kukabiliana na uharibifu wa ardhi. 

Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai

102. Mheshimiwa Spika, mradi huu utagharimu Dola za Marekani 11,205,872.00. Lengo la mradi ni kurejesha uoto wa asili na hifadhi ya bioanuai kupitia usimamizi jumuishi wa mifumo ikolojia. Mradi huu unatekelezwa kwenye Bonde la Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa katika Wilaya za Iringa Vijijini, Mbeya Vijijini, Mbarali, Wanging’ombe, Tanganyika, Mpimbwe na Sumbawanga Vijijini. Katika mwaka 2022/23, Shilingi 5,775,235,425.00 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na urejeshaji wa misitu na mazingira.

Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kitaasisi Kutekeleza Mkataba wa Montreal Kuhusu Udhibiti wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni

103. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Shilingi 94,775,000.00 zimetengwa kwa ajili ya kuendesha mafunzo kwa mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu kutoka Zanzibar na kukusanya takwimu za matumizi ya kemikali husika.

Mradi wa Kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Mkataba wa Stockholm Unaohusu Kemikali Zinazodumu katika Mazingira kwa Muda Mrefu

104. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Shilingi 339,427,360.00 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za mradi ikiwemo kuandaa Mpango wa Kitaifa wa uondoshaji wa kemikali zinazodumu katika mazingira jamii ya Polychlorinated Biphynels (PCBs); na Kutekeleza mradi wa majaribio unaohusisha ujenzi wa vituo vya kukusanya na kuchakata taka zinazorejelezeka katika Manispaa za Ubungo na Kigamboni.

Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza Usalama wa Chakula katika maeneo kame ya Tanzania

105. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Shilingi 2,750,521,020.00 zimetengwa kwa ajili ya uchimbaji wa malambo, ujenzi wa mabwawa, ujenzi wa mifumo ya uvunaji maji ya mvua, ujenzi wa mabirika ya kunyweshea mifugo na majosho, kukarabati tuta la kuzuia maji ya baharí katika bonde la Koowe – Micheweni Pemba.

Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi Kupitia Mifumo ya Ikolojia

106. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23 Shilingi 7,370,839,681.00 zimetengwa kwa ajili utekelezaji wa shughuli za mradi ikiwemo uchimbaji wa malambo; ujenzi wa majosho na mabirika ya kunyweshea mifugo; kuwezesha ufugaji endelevu; na miradi mingine rafiki kwa mazingira katika

Halmashauri mbalimbali nchini. 

Mradi wa Kupunguza Hewa Ukaa inayosababishwa na Ukataji na Uharibifu wa Misitu 

107. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23 Shilingi 965,194,800.00 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha Mwongozo wa Taifa wa Kupunguza Hewa Ukaa; kuhuisha Mkakati wa Kupunguza

Uharibifu wa Misitu na Ukataji Miti katika Sera na Mipango ya Wizara za Kisekta; na kujenga uwezo wa taasisi katika kusimamia na kuratibu shughuli za kupunguza hewa ukaa.

Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kitaasisi wa Kutekeleza Sheria ya Usimamizi wa Mazingira

108. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23 Shilingi 826,736,000.00 zimetengwa kwa ajili ya kuanzisha kanzidata ya usimamizi wa taka nchini; kufanya tathmini ya ufanisi wa Sheria ya Mazingira, Sura 191 pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi katika kutekeleza Sheria hiyo.  

Mradi wa Ujenzi na ukarabati wa Kingo za fukwe katika maeneo ya mwambao Mikindani Mtwara na Sipwese Zanzibar

109. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23 kiasi cha Shilingi 282,000,000.00 kimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa kingo katika fukwe za Mikindani na Sipwese.

MASUALA YA UTAWALA NA MAENDELEO YA WATUMISHI

 1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/23, Ofisi imepanga kuajiri na kupandisha vyeo watumishi kwa kuzingatia utendaji kazi na miundo inayotawala kada zao. Aidha, Ofisi itaendelea kusimamia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na kuimarisha Maadili na Utawala Bora katika Utumishi wa Umma. Ofisi itawezesha watumishi kushiriki mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na mfupi. Mafunzo ya muda mfupi yatahusisha mafunzo ya uongozi, usimamizi wa miradi, maadili na itifaki pamoja na kutoa elimu na ushauri kuhusu masuala ya UKIMWI, Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza na UVIKO – 19. Vilevile, Ofisi itaendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kuwapatia Watumishi vitendea kazi pamoja na stahili zao.
 2. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/23 Ofisi itaendelea kusimamia ujenzi wa awamu ya pili wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mtumba – Dodoma ili kuwezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. 

BARAZA LA TAIFA LA HIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA 

112. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/23 Baraza limepanga kuendelea kutekeleza kazi zifuatazo: kuratibu mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa kusajili na kufanya mapitio ya miradi na kusajili Wataalam Elekezi wa Mazingira; kuendelea kutoa elimu kwa umma na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya mazingira; kushirikiana na wadau kuandaa miongozo ya kisekta kwa lengo la kurahisisha mapitio ya taarifa za TAM za sekta husika; kuendelea na kaguzi za mazingira katika maeneo mbalimbali ili kulinda na kutunza mazingira;kufanya tafiti za mazingira; kukamilisha tathmini ya eneo la Rufiji-Mafia-Kibiti-Kilwa (RUMAKI) ili kujumuishwa katika Mtandao wa Dunia wa Binadamu na Hifadhi Hai uliopo Chini ya Shirika la Kimataifa la UNESCO; na kuendelea kuratibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya hifadhi na usimamizi wa mazingira na kujenga weledi wa wadau kuhusu utekelezaji wa Sheria.

HITIMISHO NA SHUKRANI

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba nitumie nafasi hii kuwashukuru walionisaidia kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi. Shukrani zangu za dhati na za kipekee ni kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake, dira na maelekezo aliyotupatia kuhusu majukumu yetu. Aidha, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa busara na uongozi wake pamoja na maelekezo anayotupatia katika kutekeleza majukumu. Vilevile, ninamshukuru Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kutusimamia vema katika kutekeleza majukumu yetu. Ninapenda pia kumshukuru Mheshimiwa Khamis H. Khamis (Mb.), Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa ushirikiano anaonipa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Ninazishukuru pia Kamati za Kudumu za Bunge za Katiba na Sheria na Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kupitisha bajeti hii ni nayoiwasilisha kwa mwaka 2022/23. 
 1. Mheshimiwa Spika, Vilevile, ninapenda kuwashukuru Bi. Mary N. Maganga, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais; Bw. Abdallah H. Mitawi,

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano); na Bw. Edward G. Nyamanga Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Ninawashukuru pia Prof. Mhandisi Esnath O. Chaggu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya

Baraza la Hifadhi ya Mazingira, Dkt. Mhandisi Samwel G. Mafwenga, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira,Wakuu wa Idara na Vitengo; na Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza kwa mchango wao katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi. Pia ninawashukuru wale wote waliotuwezesha kutekeleza majukumu ya Ofisi kwa kipindi kilichopita, na ambao wamesaidia katika kuandaa Mpango na Bajeti ya mwaka 2022/23.

 1. Mheshimiwa Spika, Ofisi imefanikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo na Wadau mbalimbali. Ninapenda kuwataja baadhi ya washirika wa maendeleo ambao Ofisi imefanya nao kazi kwa karibu kama ifuatavyo: Serikali ya Norway; Serikali ya Sweden; Umoja wa Nchi za Ulaya – EU; Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa – UNDP;

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa – UNEP; Mfuko wa Mazingira wa Dunia – GEF; Benki ya Dunia; Benki ya Maendeleo ya Afrika – AfDB; CRDB;

UNCDF; Foreign and Commonwealth Development Organization (FCDO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda – UNIDO; Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani – WWF; Mfuko wa Kimataifa wa Kuendeleza Kilimo – IFAD; Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi – GCF; Shirika la  Kilimo na Chakula Duniani – FAO; Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani – GIZ; Asasi Zisizo za Kiserikali (AZISE); Sekta Binafsi;  Kamati Maalum ya Usimamizi wa Kampeni Kabambe, na Mabalozi wa Mazingira. Aidha, ninapenda nitumie fursa hii kuwaomba Washirika wa Maendeleo na Wadau wengine kuendelea kushirikiana na Ofisi katika kuimarisha Muungano wetu na kuhifadhi mazingira yetu.

MAOMBI YA FEDHA

116. Mheshimiwa Spika, ili Ofisi iweze kufikia malengo tarajiwa kama nilivyobainisha kwenye hotuba yangu, ninaomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liidhinishe maombi ya fedha kwa mwaka

2022/23 kama ifuatavyo: –

FUNGU 26: MAKAMU WA RAIS

117. Mheshimiwa Spika, ninaomba Bunge lako Tukufu liidhinishe Makadirio ya Matumizi ya Shilingi 12,974,292,000 ikiwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida kwa mwaka 2022/23. Kati ya kiasi hicho, Shilingi 974,292,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya watumishi na Shilingi 12,000,000,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo.

FUNGU 31: OFISI YA MAKAMU WA RAIS

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba Bunge lako

Tukufu, liidhinishe makadirio ya Matumizi ya Shilingi 40,142,025,000.00 kwa ajili ya Fungu hili. Kati ya kiasi hicho, Shilingi 18,180,328,000.00 ni kwa ajili Matumizi ya Kawaida na Shilingi 21,961,697,000.00 ni Matumizi ya Miradi ya Maendeleo. Matumizi ya Kawaida yanajumuisha Shilingi 3,297,558,270.00

Mishahara ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Shilingi 4,362,627,730.00 Mishahara ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingirana Shilingi 10,520,142,000.00 Matumizi Mengineyo. Aidha, Matumizi ya Miradi ya Maendeleo yanajumuisha Shilingi 3,602,000,000.00 fedha za Ndanina Shilingi 18,359,697,000.00 fedha za Nje.

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *