CCBRT NA TAASISI YA JAKAYA KIKWETE WAJITOA KUSAIDIA MAMA NA MTOTO

HOSPITALI YA CCBRT KWA KUSHIRIKIANA NA TAASISI YA JAKAYA MRISHO KIKWETE WAMEANDAA CHAKULA CHA USIKU KWA DHUMUNI LA KUCHANGISHA FEDHA KWA AJILI YA UENDESHAJI WA KITENGO KIPYA CHA MAMA NA MTOTO. HOTELI YA SERENA MEI 7, 2022.

Dar es Salaam 27 Aprili, 2022. Katika kutatua changamoto zinazowakabili akina mama wajawazito walioko katika mazingira magumu na uzazi hatarishi, hospitali ya CCBRT kupitia kitengo chake kipya cha afya ya uzazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete wameandaa chakula cha usiku cha hisani kwa ajili ya kuchangisha fedha zitakazotumika kutoa huduma ya uzazi salama kwenye kitengo hicho. Kitengo hiki kina miundo mbinu maalum ya kuwahudumia wanawake wajawazito wenye ulemavu, wenye historia ya fistula na mabinti wanaopata ujauzito wakiwa na umri mdogo ili kuhakikisha wanawake wote wanapata huduma ya uzazi salama.

CCBRT kupitia kitengo hiki kina dhamira ya kuunga juhudi za Serikali za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi sambamba na kuzuia ulemavu.

Mgeni Rasmi katika hafla hiyo itakayofanyika Jumamosi jioni tarehe 7 Mei, 2022, katika hoteli ya Serena Dar es Salaam anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mheshimiwa, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Kwa muda mrefu hospitali ya CCBRT kwa kushirikiana na serikali wamekuwa wakitoa huduma ya afya katika mifumo ya afya ya uzazi kwenye mkoa wa Dar es Salaam, kujenga uwezo wa wataalamu wa afya walioko kwenye vitengo vya afya ya uzazi katika hospitali za umma za mkoa wa Dar es Salaam sambamba na ujenzi wa kitengo cha afya ya uzazi katika hospitali ya CCBRT.

“Ingawa kitengo hiki tunategemea kufunguliwa rasmi mwezi Juni, tumeanza kutoa huduma kwa awamu tokea mwezi januari na kufikia sasa tumezalisha akina mama wajawazito wapatao 37. Kitengo hiki kitatumika kama hospitali ya rufaa ya kanda na tutakapoanza kutoa huduma kwa ukamilifu wake tutakuwa na uwezo wa kuwahudumia akina mama wenye ujauzito hatarishi wapatao 12,000 kwa mwaka”, anasema Brenda Msangi Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa hospitali ya CCBRT katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Brenda alitumia mkutano huo kuwaomba wadau wote wa afya ya uzazi kuwaunga mkono ili kuwezesha mazingira ya uzazi yaliyo salama, yenye staha na ubora kwa mama zetu na kwamba ifike siku moja kila mwanamke aweze kutarajia ujauzito na kujifungua salama, heshima na kwa furaha.

Kuhusu mradi wa kujenga uwezo, Brenda anasema CCBRT inatambua kuwa kinga huleta matokeo mazuri na ya muda mrefu kuliko tiba na kwamba uzazi salama huzuia ulemavu wa maisha, kwa sababu hiyo mwaka 2010 CCBRT kwa kushirikiana na timu ya afya ya mkoa wa Dar es Salaam, na Manispaa zake tano walianza kutoa huduma pana za afya katika mifumo ya afya ya uzazi kwenye mkoa wa Dar es Salaam, tangu wakati huo hadi sasa wameweza kuvifikia vituo vya afya na hospitali 23 za umma mkoani humo.

Brenda anasema; “kwa sasa, vituo hivi vina vifaa tiba na maboresho yamefanyika kwenye miundombinu kuongezeka kwa utendaji kazi na hivyo kuwezesha huduma salama na zinazofikika kiurahisi kwa akina mama na watoto. Mifumo ya rufaa imeimarishwa ili kupunguza msongamano hasa kwenye hospitali kubwa. Vituo vinakusanya takwimu sahihi na zenye ubora kwa kutumia mifumo ya kisasa kama vile mpango wa kutambua changamoto za vifo vya watoto wachanga. Hii husaidia watoa huduma kuelewa zaidi sababu za vifo na hivyo kuzuia vifo zaidi visitokee. Upatikanaji wa damu safi na salama unazidi kuboreka ili kuhakikisha kwamba akina mama na watoto wachanga wanaweza kupata damu ikihitajika na kama kuna dharura.” 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *