
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 26 Aprili 2022 ameongoza maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Maadhimisho hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma yakienda sambamba na Kongamano la Muungano pamoja na uzinduzi wa kitabu cha historia ya Muungano.
Akitoa hotuba katika maadhimisho hayo Makamu wa Rais amesema watanzania wana kila sababu ya kujivunia Muungano ambao umeendelea kudumu, kustawi na kuimarika na kuweza kufikia miaka 58 tangu kuasisiwa kwake. Ameeleza kwamba viongozi wote kwa pamoja wanapaswa kuhakikisha Muungano unaendelea kuenziwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo ili kuendelea kufurahia amani, mshikamano na umoja ulioachwa na waasisi wa Muungano.
Makamu wa Rais amesema Muungano umesaidia kujenga Taifa moja, lenye watu wamoja na wanaozungumza lugha moja pamoja na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama inayowezesha watanzania kuendelea na shughuli kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa amani na utulivu. Aidha amesema kupitia muungano sekta ya elimu na ajira imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kuwezesha wanafunzi wote bila kujali upande wa Muungano watokako kupata elimu na ajira bila ya ubaguzi.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema zipo fursa nyingi za kimuungano ambazo bado hazijatumika kikamilifu na kuwataka viongozi kuongeza kasi ya utoaji elimu ya Muungano kwa umma ili wananchi waweze kuzitumia fursa hizo kujiletea maendeleo na kuimarisha uhusiano mzuri ulipo kati ya pande zote mbili za Muungano.
Pia Makamu wa Rais amewasihi wananchi wote kuhakikisha wanashiriki zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 agosti 2022 ili kuiwezesha serikali kupata takwimu ambazo zitakazosaidia kuainisha mahitaji yao. Aidha amewasihi watanzania kuendelea kutunza mazingira pamoja na kupanda miti katika maeneo yao ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Katika maadhimisho hayo, Makamu wa Rais amemkabidhi kadi ya bima ya Afya mmoja wa waliochanganya udongo siku ya Muungano Aprili 26 mwaka 1964 mzee Hasaniel Mrema pamoja na kutoka kadi ziwafikie wahusika wengine wa uchanganyaji udongo ambao walishindwa kufika katika maadhimisho hayo.
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Kitabu cha Historia ya Muungano mmoja
wa waliochanganya Udongo siku ya Muungano mwaka 1964 mzee
Hasanieli Mrema wakati wa Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano
yaliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Mkoani
Dodoma. Aprili 26,2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. Philip Mpango akimkabidhi kadi ya bima ya Afya mmoja wa
waliochanganya Udongo siku ya Muungano mwaka 1964 mzee Hasanieli
Mrema wakati wa Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano yaliofanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Mkoani Dodoma. Aprili 26, 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. Philip Mpango akimkabidhi zawadi Saada Omary Ali mwanafunzi wa
Skuli ya Hifadhi Zanzibar akiwa miongoni mwa washindi wa uandishi wa
insha katika mada za Muungano wakati wa Maadhimisho ya Miaka 58 ya
Muungano yaliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete
Mkoani Dodoma. Aprili 26,2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. Philip Mpango akizindua Kitabu cha Historia ya Muungano wakati
wa Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
yaliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Mkoani
Dodoma. Aprili 26,2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi, Wanafunzi na wananchi
mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano
yaliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Mkoani Dodoma


