
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP ISDOR MPANGO, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 58 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
TAREHE 26 APRILI, 2022
UKUMBI WA JAKAYA KIKWETE, DODOMA
Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar:
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;
Mheshimiwa Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania;
Mheshimiwa Khamis Ramadhan Abdallah, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Waheshimiwa Viongozi Wastaafu:
- Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu (Warioba, Malecela, Sumaye, Pinda);
- Waheshimiwa Spika Wastaafu (Msekwa, Makinda, Kificho); na
- Waheshimiwa Viongozi wa Chama Wastaafu (Mangula).
Mheshimiwa George Boniface Simbachawene (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu);
Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar;
Mheshimiwa Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Komred Daniel Chongolo, Katibu Mkuu wa CCM;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wa SMT na SMZ;
Waheshimiwa Wanasheria Wakuu wa Serikali wa SMT na SMZ;
Mheshimiwa Katibu Mkuu Kiongozi – SMT;
Mheshimiwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi – SMZ;
Ndugu Makatibu Wakuu – SMT na SMZ;
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Viongozi wote wa Vyama mbalimbali vya Siasa mliopo;
Wakuu wa Taasisi na Asasi mbalimbali mliopo;
Mzee Hasaniel Mrema;
Viongozi wetu wa Dini;
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wanahabari;
Mabibi na Mabwana.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…….
Nami niungane na wenzangu walionitangulia, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa tukiwa na afya njema, kuadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao uliasisiwa rasmi tarehe kama ya leo mwaka 1964.
Pili, namshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kunipa heshima kubwa na kunielekeza nimwakilishe katika shughuli hii ya Maadhimisho ya 58 ya Muungano inayoshirikisha wadau mbalimbali hususan Taasisi na Asasi zisizo za Kiserikali, Vyama vya Siasa na makundi mbalimbali kutoka pande zote za Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Aidha, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kujumuika nasi siku hii ya leo.
Tatu, nitumie nafasi hii pia kuwapongeza Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Sherehe za Muungano, na Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, pamoja na Kamati ya wataalam, kwa kusimamia na kufanikisha maandalizi ya maadhimisho haya muhimu ambayo yamefana sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na wadau wote hongereni sana!
Nne, nawapongeza pia wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuadhimisha miaka 58 ya Muungano unaojidhihirisha kwa Umoja, Mshikamano, Ushirikiano, Upendo na Amani miongoni mwetu. Miaka 58 ya Muungano wa nchi mbili huru sio jambo rahisi, ni suala la kujivunia na kujipongeza. Hongereni sana watanzania wote Bara na Visiwani. Niwasihisote kwa pamoja kuuenzi Muungano wetu na tuhakikishe unaendelea kudumu na kuimarika zaidi.
Waheshimiwa Viongozi,
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana
Tunapoadhimisha miaka 58 ya Muungano, hatuna budi kuwakumbuka na kuwashukuru viongozi wetu Waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwa maono makubwa, uamuzi wa busara, hekima na utashi wa kurasimisha na kuunganisha nchi zetu mbili huru kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awapumzishe waasisi hao mahali pema peponi, Amina.
Pamoja na viongozi wakuu walioasisi Muungano wetu, tunawapongeza pia viongozi wengine na wananchi walioshiriki kufanikisha na kurasimisha Muungano wetu. Kwa namna ya pekee nawashukuru wazee walioshiriki katika tukio la kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Mzee Hasanieli Mrema (ambaye tunaye hapa leo), Mzee Hassan Omari Mzee, Mama Sifaeli Mushi na Mama Khadija Abbas Rashid. Hakika tulitamani sana kuwa na wazee wetu wote hawa katika Maadhimisho haya ya Miaka 58 ya Muungano wetu lakini kutokana na sababu mbalimbali hawakuweza wote kuwa nasi. Tunakushukuru sana Mzee Mrema kwa kushiriki pamoja nasi katika maadhimisho haya. Jambo kubwa ambalo Watanzania wote tunapaswa kulifanya kwa wazee wetu hawa ni kuendelea kuuenzi, kuuimarisha na kuudumisha Muungano na pia kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuwajalia afya njema. Kwa niaba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba baada ya Hotuba yangu niwakabidhi Wazee wetu hawa zawadi ya Kadi ya Bima ya Afya kila mmoja ambayo itakidhi mahitaji muhimu ya kupata matibabu popote pale ndani ya nchi yetu.
Waheshimiwa Viongozi,
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana
Tunapoadhimisha miaka 58 ya Muungano, yafaa kujikumbusha kwa ufupi kuhusu historia ya muungano wa nchi zetu mbili zilizokuwa huru. Tukio muhimu la kuziunganisha rasmi nchi hizi lilifanyika tarehe 22 Aprili, 1964 ambapo Hati ya Makubaliano ya Muungano ilisainiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kufuatiwa na matukio mbalimbali ya Muungano yaliyohitimishwa rasmi tarehe 26 Aprili, 1964.
Nia na dhamira ya dhati ya viongozi wetu Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume kujitoa na kuachia madaraka ya nchi zilizokuwa huru na kuamua kuunda nchi moja siyo jambo rahisi. Hivyo, ni jukumu letu sisi sote viongozi tuliopewa dhamana ya kuiongoza nchi yetu kuhakikisha kuwa Muungano unaendelea kuenziwa na vizazi vya sasa na vijavyo ili kuendelea kufurahia amani, mshikamano na umoja tulioachiwa wa waasisi wa Muungano.
Tuna kila sababu ya kujivunia Muungano wetu ambao umeendelea kudumu, kustawi na kuimarika na kuweza kufikia miaka 58 tangu kuasisiwa kwake. Wapo wenzetu, Barani Afrika kama Ethiopia na Eritrea, na pia Senegal na Gambia walioungana lakini hawakufanikiwa kama sisi kwani muungano wao ulidumu muda mfupi na kusambaratika.
Naomba ninukuu maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere:
“Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru. Nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka katika Ukoloni. Tanzania ni ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe, baada ya kukomboa sehemu zake kutoka katika Ukoloni.” mwisho wa kunukuu.
Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa dhati Viongozi wetu wa awamu mbalimbali za Serikali zetu mbili, kwa uongozi wao bora uliowezesha Muungano huu kudumu, kustawi na kuzidi kuimarika hadi leo hii. Pamoja na changamoto zilizojitokeza katika Muungano wetu nyakati mbalimbali, hekima, busara na uongozi wao makini umewezesha changamoto hizo kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya maelewano.
Waheshimiwa Viongozi,
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana
Kwa takwimu zilizopo, Watanzania walio wengi wamezaliwa baada ya Muungano. Kwa mantiki hiyo, wananchi wengi na hasa vijana wanaufahamu Muungano huu ama kwa kusimuliwa au kusoma machapisho mbalimbali. Aidha, kumekuwepo mijadala mingi kuhusu historia, mantiki ya aina ya muungano wa nchi zetu mbili, faida na changamoto zake. Kupitia mijadala hii inaonekana kuwa wananchi wengi hawana uelewa mpana kuhusu Muungano wetu. Hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kuhusu Muungano wetu na Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuendelea kuelimisha zaidi wananchi juu ya muungano.
Ninayo furaha kubwa sana leo, kwani pamoja na makongamano, maonesho, michezo na burudani yaliyofanyika Tanzania Bara na Zanzibar katika kuadhimisha miaka 58 ya Muungano, muda mfupi ujao tutakuwa na tukio muhimu la uzinduzi wa Kitabu cha ‘Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Chimbuko, Misingi na Maendeleo’.
Kitabu kimeeleza mazingira ya kihistoria na misingi iliyowezesha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kufanyika, kuimarika na kudumu kwa miaka 58 sasa; na jinsi waasisi wa Muungano walivyokuwa viongozi wa mfano, waliotanguliza maslahi ya Taifa mbele kabla ya maslahi yao binafsi. Aidha, Kitabu hicho kimeainisha mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka 58 ya Muungano pamoja na hojaza muungano zilizojitokeza na hatua zilizochukuliwa kuzipatia ufumbuzi. Vilevile, Kitabu kimeelezea kwa kina utaratibu ambao Serikali zetu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimejiwekea kwa ajili ya kujadili hoja za Muungano zinazojitokeza kwa lengo la kuzipatia majawabu ya kudumu.
Napenda nitumie fursa hii kwanza, kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kupitia kitabu hiki na kutoa maoni/ushauri ambao umeboresha sana yaliyomo katika kitabu hiki, na vilevile kuandaa tamko lao la pamoja ambalo limo kwenye Kitabu hicho na kuridhia kichapishwe. Pia nawapongeza Mheshimiwa Dkt. Selemani Said Jafo (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar, kwa kuratibu vizuri maandalizi ya kitabu hiki. Aidha, naiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia upande wa Tanzania Bara na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar zijipange kuhakikisha Kitabu hicho kinapatikana Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Mimi naamini kwa dhati kabisa kuwa Tukiuelewa Muungano wetu, tutaulinda!
Waheshimiwa Viongozi,
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Katika miongo zaidi ya mitano ya Muungano, nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Mambo ya Muungano yanayoonekana katika nyanja zote za maisha ya Watanzania, yaani, kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kiusalama. Kupitia hadhara hii, ningependa kuyataja baadhi ya mafanikio ya Muungano kama ifuatavyo:
Jambo la kwanza, sisi sote ni mashahidi kuwa Muungano wetu umekuwa na manufaa makubwa sana Kisiasa na Kijamii. Muungano umesaidia kujenga Taifa moja, lenye watu wamoja na wanaozungumza lugha moja. Kabla ya Muungano na muda mfupi baada ya kuungana kwa nchi zetu, tulikuwa tunatumia sheria mbili tofauti za uraia na uhamiaji. Jambo la kujivunia ni kuwa, sasa masuala haya yanasimamiwa na Sheria moja. Aidha, kwa kufurahia matunda ya uraia wa nchi moja, wananchi wamekuwa na uwezo wa kwenda au kuishi sehemu yeyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila vikwazo. Kwa mfano ukienda Sumbawanga utawakuta Wapemba na ukienda Unguja utawakuta Wachaga, Wamasai, Wasukuma nk. Kumekuwapo muingiliano wa tamaduni kama aina ya vyakula, mitindo ya mavazi na burudani ikiwemo michezo, sanaa na ngoma na kuoleana pande zote mbili za Muungano, mambo ambayo yamepelekea wananchi kuwa wamoja zaidi. Sambamba na haya, hata katika nafasi za kisiasa na kiutawala tumeona Viongozi wa Juu wa Vyama vya Siasa na Serikali wakitoka upande wowote wa Muungano na kushika madaraka katika mihimili ya dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli hili ni jambo la kujivunia sana!
Jambo la Pili, hali ya Ulinzi na Usalama wa nchi yetu katika kipindi chote cha Miaka 58 imendelea kuimarika ambapo sote tunafurahia uwepo wa utulivu na amani nchini ambao umewawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Watanzania wa pande zote mbili za Muungano tumeweza kulinda uhuru wetu na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar dhidi ya matishio mbalimbali. Umoja wetu na mshikamano ndani ya Muungano pamoja na uwezo na weledi tulioujenga katika vyombo vya ulinzi na usalama ndiyo siri ya mafanikio hayo. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinavyoundwa na vijana walio katika sare na wasio na sare kutoka Tanzania bara na Zanzibar vimeendelea kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kulinda usalama wa raia na mali zao; kuzuia na kupambana na uhalifu; kupeleleza makosa ya jinai; kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa; na kudumisha usalama na amani ya nchi.
Jambo la Tatu kwa upande wa Elimu na Ajira, kuna mafanikio makubwa sana. Mazingira mazuri yaliyojengwa na Muungano wetu katika kipindi cha miaka 58 yamewezesha wanafunzi wote bila kujali upande wa Muungano watokako kupata elimu bila ya ubaguzi. Wanafunzi wa Zanzibar wanapata elimu Tanzania Bara katika ngazi yoyote wanayoitaka kama Watanzania. Halikadhalika, wanafunzi kutoka Bara wanapata elimu Tanzania Zanzibar katika ngazi yoyote wanayoitaka. Aidha, pande zote mbili za Muungano zimepiga hatua kubwa ambapo shule za msingi, shule za sekondari, Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vimeongezeka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na kipindi ambacho Muungano uliasisiwa. Katika kuwezesha wanafunzi kupata Mikopo ya Elimu ya Juu, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar bila ubaguzi na hivyo kuwawezesha vijana wetu kupata elimu ya juu Tanzania Bara ama Zanzibar.
Aidha, kupitia Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2003 kumekuwa na utaratibu wa wazi wa ajira katika Utumishi wa Umma na kuondoa dosari zilizokuwepo. Serikali ya Jamhuri ya Muungano imekuwa ikitoa fursa sawa za ajira kwa Wananchi wa pande zote mbili za Muungano. Katika ajira, tumeshuhudia Wananchi kutoka Zanzibar wakipata ajira Tanzania bara na wa kutoka Tanzania Bara kupata ajira na kufanya kazi Zanzibar. Mathalan, tumekuwa na wanazuoni maarufu kutoka Zanzibar kama Hayati Profesa Haroub Othman, Profesa Saida Yahya Othman, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal wakifundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Profesa Khatib Haji Semboja, Profesa Ntahondi Nyandwi na Profesa Desiderius Masalu kutoka Tanzania Bara wakifundisha Vyuo Vikuu vya Zanzibar. Haya yote ni matunda ya Muungano wetu.
Jambo la Nne, kwa upande wa Uhusiano wa Kimataifa, Nchi yetu imekuwa na mchango mkubwa katika medani ya Kimataifa kuanzia katika Jumuiya za Kikanda hadi Umoja wa Mataifa. Heshima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kimataifa ni kubwa kutokana na mchango wake katika mapambano ya Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, ushiriki katika Vikosi vya kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afika na SADC na usuluhishi wa migogoro ya kisiasa katika nchi mbalimbali. Ujasiri na umahiri wa makamanda na wapiganaji wa majeshi yetu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar unasifika sehemu zote walipofanya kazi. Diplomasia ya Kisiasa na Kiuchumi ya nchi yetu imeongozwa na wana diplomasia nguli kutoka pande zote mbili za Muungano, wakiwemo Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Mzee Benjamin William Mkapa, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mheshimiwa Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim, Mheshimiwa Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, Mheshimiwa Balozi Getrude Mongela, Hayati Balozi Dkt. Augustino Mahiga, Mheshimiwa Balozi Amina S. Ali na wengine wengi.
Jambo la Tano, katika kipindi cha miaka 58 ya Muungano nchi yetu imepata maendeleo makubwa ya kiuchumi. Baada ya Muungano, nchi zetu zilikubaliana kuwa na sarafu moja. Matumizi ya sarafu moja yamechochea sana katika kuongezeka kwa biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ambapo tumeona wawekezaji wakubwa kutoka pande zote mbili za Muungano wakifanya biashara kwa urahisi bila haja ya kubadili fedha. Aidha, Wafanyabiashara kutoka Tanzania Bara wananunua bidhaa za viungo hasa karafuu kutoka Zanzibar na Wafanyabiashara kutoka Zanzibar wananunua bidhaa kama za saruji, mbao, maharage na nyama kutoka Tanzania Bara. Vilevile, wananchi wanafanya biashara za kuuza na kununua bidhaa kila siku katika masoko maarufu ya Kariakoo – Dar es Salaam na Darajani – Zanzibar hivyo kuhamasisha kuongezeka kwa biashara na kipato cha mwananchi. Halikadhalika, Zanzibar inafaidika na vyanzo vya uzalishaji wa umeme kutoka Tanzania Bara na hivyo kuweza kuendesha shughuli za uzalishaji na kuwezesha wananchi kujiajiri kwa kufungua biashara mbalimbali na viwanda.
Vilevile, makampuni ya mawasiliano, mabenki pamoja na makampuni mengine makubwa, yameweza kutumia soko kubwa lililotokana na Muungano wetu, kufanya biashara. Mazingira ya kufanya biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar yameendelea kuimarika ambapo tumeweza kuona kupitia mabenki yetu kama NMB, PBZ na CRDB wananchi hawana haja ya kubeba pesa mkononi wanaposafiri kwenda upande wowote wa Muungano na badala yake wanachohitaji ni kubeba kadi zao za Benki tu ili kuweza kupata huduma za kifedha mahali popote nchini. Aidha, sisi sote ni mashahidi kuwa kupitia makampuni ya simu, wananchi wameweza kufanya miamala kwa kupitia simu za viganjani wakati wowote, mahali popote kwa urahisi.
Sambamba na haya, kupitia sekta ya Utalii, tumeweza kufanya biashara kwa pamoja kama soko moja ambapo watalii wanaweza toka upande mmoja wa Muungano kwenda upande mwingine kwa ajili ya shughuli za utalii. Aidha, tukiwa kama nchi moja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), tumeendelea kunufaika na fursa za kibiashara na sasa tunatarajia kunufaika zaidi kama taifa katika Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (African Continental Free Trade Area). Vilevile, kama nchi moja, tumeweza kupata misaada na mikopo nafuu ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali kama kilimo, uvuvi, miundombinu, mazingira, elimu, teknolojia na sekta nyinginezo ambapo wananchi pia wamefaidika kiuchumi kwa kushiriki katika minyororo ya thamani.
Waheshimiwa Viongozi,
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Hayo machache niliyoyataja yanadhihirisha wazi kuwa, wananchi wa pande mbili wamepiga hatua kubwa na kasi ya ushirikiano imeongezeka. Wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara wa pande zote, wameonyesha kuwa, Muungano wetu ni zaidi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano na orodha ya Mambo ya Muungano. Ushirikiano wetu umeimarika na wananchi wamejenga mshikamano, udugu, ushirikiano katika utoaji wa huduma, ubadilishanaji wa bidhaa na kutegemeana katika nyanja zote.
Waheshimiwa Viongozi,
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Sote tunafahamu kuwa tarehe 23 Agosti, 2022 nchi yetu itafanya Sensa ya Watu na Makazi ambayo ni sensa ya Sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Lengo la kufanya Sensa ya Watu na Makazi ni kupata takwimu ambazo zitawezesha Serikali kuainisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano; watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee na hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yalipo. Hivyo, natoa rai kwa wananchi wote kutoa ushirikiano na kuwa tayari kuhesabiwa siku ya Sensa. Aidha, niwaombe pia kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kutekeleza zoezi la Mfumo Mpya wa Anuani za Makazi na Misimbo ya Posta (Post Code) ambao unalenga kila mwananchi kuwa na anuani kamili inayotambulisha makazi yake ili kutoa huduma mbalimbali ikiwemo zile za kijamii, bila vikwazo.
Waheshimiwa Viongozi,
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Kabla sijamaliza hotuba yangu, napenda pia nitumie fursa hii kusisitiza kuhusu suala la uhifadhi na usimamizi wa Mazingira. Kazi ya kuhifadhi misitu, kulinda vyanzo vya maji, upandaji miti ya mbao, matunda, mitidawa, kivuli, kupendezesha miji yetu na kufanya usafi ni lazima iwe shirikishi na ya kudumu. Nawaomba wananchi wote hasa wanaoishi pembezoni mwa fukwe za bahari kuendelea kupanda miti katika fukwe zetu ili kuimarisha kingo za bahari na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kufaidika na fursa za Uchumi wa Buluu na biashara ya hewa ya ukaa. Tuyatunze mazingira yetu, ili yatutunze!
Waheshimiwa Viongozi,
Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Muungano wetu umetunufaisha kwa kiasi kikubwa na zipo fursa nyingi ambazo hatujazitumia kikamilifu. Hatuna budi kuyalinda na kuyaendeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. Ni ukweli kuwa, elimu kwa umma ni muhimu katika kuhakikisha kuwa wananchi wote wanaelewa vyema historia ya Muungano, mafanikio na fursa za Muungano zilizopo ili waweze kuzitumia kuwaletea maendeleo na kuimarisha uhusiano mzuri ulipo kati ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano. Kitabu tunachozindua leo ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuendeleza na kuimarisha elimu ya Muungano kwa wananchi. Hivyo, natoa rai kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutumia Kitabu hiki kikamilifu ili kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ya Muungano kwa umma. Aidha, nawasihi wananchi kukisoma kitabu hiki ili kuweza kuijua historia ya muungano wetu na fursa zilizopo kwa maendeleo yetu.
Mwisho kabisa, kwa niaba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninawashukuru na kuwapongeza sana Watanzania wote wa Tanzania bara na Zanzibar kwa ushiriki wenu katika maadhimisho haya.
‘‘Miaka 58 ya Muungano: Uwajibikaji Na Uongozi Bora; Tushiriki Sensa ya Watu na Anuani ya Makazi kwa Maendeleo Yetu’’
Mungu Ubariki Muungano Wetu!
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni kwa Kunisikiliza