Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amefanya kikao na wadau wa Sekta ya Maji wa Handeni na kuelekeza hatua za haraka kuchukuliwa, ikiwamo kusimamishwa kazi kwa Watumishi wanne wa Wizara ya Maji kufuatia kusuasua kwa kazi ya ujenzi wa bwawa la Kwankambala.
Kikao hicho kilichofanyika Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa Wilaya ya Handeni ni moja ya hatua zilizochukuliwa baada ya ziara ya kikazi ya Mhe. Aweso (Mb) wilayani hapo aliyoifanya tarehe 12 Aprili, 2022, ambapo ilibainika mkandarasi anayejenga bwawa la Kwankambala amelipwa kiasi cha Shilingi Milioni 602,859,075.66 sawa na asilimia 33 ya gharama ya Mkataba na kazi iliyofanyika ni asilimia 20 ya kazi zilizopangwa kufanyika.

Aidha, iligundulika kampuni iliyopewa kandarasi ya kazi hiyo iitwayo Civil Loth Enterprises Ltd iliondoa vifaa vya kazi katika eneo la ujenzi, ingawa ilikuwa imeongezewa muda wa utekelezaji wa ujenzi.
Kutokana na hali hiyo, kikao kilichoongozwa na Mhe. Aweso (Mb) kimeelekeza yafuatayo;
a) Kufanyika mapitio ya Mkataba wa nyongeza wa Mkandarasi
b) Kuwasimamisha kazi Watumishi wafuatao ili kupisha
uchunguzi
i. Hamisi M. Matungulu – Msimamizi wa Mradi – RUWASA
Makao Makuu
ii. CPA Jimmy Mwanyakunga – Mhasibu Mkuu – RUWASA
Makao Makuu
iii. Amos Mtweve – Meneja Udhibiti Ubora wa Miradi na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi – RUWASA Makao Makuu
iv. Zam R. Mlimira – Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi – RUWASA Makao Makuu
c) Katibu Mkuu, Wizara ya Maji kuunda Tume ya Uchunguzi ili kubaini changamoto zinazokabili utekelezaji wa mradi .
d) Kushikiliwa kwa Mkandarasi Civil Loth Enterprises Ltd kwa hatua za uchunguzi zaidi.
Hatua nyingine za kukwamua ujenzi wa bwawa hilo zinaendelea.

