BARAZA LA WAFANYAKAZI TMA WAKUTANA DODOMA KUPITIA BAJETI YA MWAKA 2022/ 2023.

NA NOEL RUKANUGA.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amewapongeza Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuendelea kufanya kazi vizuri na kutekeleza majukumu kwa ufanisi mkubwa licha changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TMA. Waziri Pro. Mbarawa, amesema kuwa Mabaraza ya Wafanyakazi yameanzishwa kisheria kwa lengo la kuwashirikisha wafanyakazi katika shughuli mbalimbali za utendaji wa Taasisi.

 “Nimejulishwa kwamba mmekuwa mkitekeleza vyema takwa la kisheria, hivyo nawapongeza sana. nimefurahi kusikia kwamba Baraza hili lina wajumbe kutoka vituo vyote vya Hali ya Hewa Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuzingatia muundo wa mkataba wa Baraza lenu” amesema Prof. Mbarawa.

Amesema kuwa hali hiyo inaonesha jinsi mawazo wafanyakazi  kwa pamoja yanavyotumika katika kuboresha huduma mnazotoa na kupelekea mafanikio makubwa ambayo mnaendelea kuyapata ikiwa ni pamoja na kuendelea kumiliki cheti cha ubora ISO 9001:2015.

Amesema Wizara yake  iko tayari kuwasaidia endapo kutatokea changamoto yoyote katika utekelezaji wa jukumu ikiwemo ukusanyaji wa mapato.

“Hata hivyo, kuna jambo ambalo nadhani ni vizuri mkalifamu na kulifanyia kazi.Majadiliano yenu yajikite kuwaelimisha wadau kuitekeleza Sheria.Kuchangia huduma ni suala la kisheria hivyo kila mdau hana budi kulitekeleza,” amesema Prof. Mbarawa.

Prof.Mbarawa ameitaka Mamlaka hiyo iainishe  bajeti na  njia za ukusanyaji wa mapato ili kuiwezesha taasisi kujiendesha kwa ufanisi.

“Natambua Serikali ni mdau mkubwa katika huduma zitolewazo kwa jamii (Public Good), wakati Serikali inatekeleza jukumu hilo wadau wanaotumia huduma kibiashara nao pia watekeleze wajibu wao wa kuchangia huduma,” amesema.

Kuhusu changamoto ya maslahi duni ya wafanyakazi, Prof. Mbarawa amesema Wizara  kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – UTUMISHI inalishughulikia suala hilo ambapo ameahidi  taratibu zikikamilika maslahi ya watumishi ikiwemo mishahara itaboreshwa.

Ameeleza kuwa amefurahi kusikia kuwa wapo  katika hatua mbalimbali za majadiliano ya kukubaliana Tozo mpya kwa sekta nyingine.

“Mmetoa mfano wa sekta ya Ujenzi, Kwenye maji kwa maana ya wale wanao miliki vyombo, na watalii; ambao hawajaanza kuchangia, na kwamba majadiliano yanaendelea vizuri. Nawapongeza sana katika jitihada hizi,” amesema Prof. Mbarawa.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi ambaye ni Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, amesema kuwa Mamlaka imehakikisha viwango na taratibu za kimataifa za utoaji wa huduma za hali ya hewa pamoja na usimikaji wa vifaa na mitambo vinazingatiwa.

Amefafanua kuwa kwa mujibu wa sheria, Mamlaka inafanya udhibiti wa shughuli kuu tatu ambayo ni uangazi wa hali ya hewa (meteorological observation), utabiri wa hali ya hewa (weather and climate forecasting) pamoja na kubadilisha mwenendo wa hali ya hewa (weather modification).

Amesema kuwa wamefanikiwa kuendelea kumiliki Cheti cha utoaji huduma bora ISO 9001:2015 ambapo katika ukaguzi wa kimataifa uliofanyika mwaka jana Disemba, 2021 Mamlaka ilifanya vizuri katika ukaguzi huo na hakukuwa na hoja ya ukaguzi (Non – Confirmity).

Amesema kuwa wanaendelea na taratibu za ununuzi wa Rada nne (4) za hali ya hewa zitakazofungwa katika Mikoa ya Mbeya, Kigoma, Dodoma na Kilimanjaro.

“Malipo ya awali yameshafanyika na Rada hizo zinaendelea kutengenezwa huko Marekani. Rada hizo zinatarajiwa kufungwa kati ya mwezi wa Julai, 2022 na Juni, 2023, ukamilishaji wa mtandao wa Rada za hali ya hewa utasaidia utoaji wa huduma kwa Umma na kwa sekta binafsi na pia kuboresha na  kupunguza madhara yanayotokana na hali mbaya ya hewa  na hivyo kukuza uchumi wa Taifa letu” amesema Dkt. Kijazi.

Ameeleza kuwa TMA imendelea kuiwakilisha nchi katika nyanja za kimataifa zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa. na katika kipindi hiki tangu Baraza lililopita, pamoja na changamoto za UVIKO-19, TMA imefanikiwa kutekeleza vyema jukumu lake la kuiwakilisha nchi katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa.

Amefafanua kuwa wataalamu mbalimbali wa Mamlaka wameteuliwa na wameendelea kutekeleza majukumu yao katika vikosi kazi mbalimbali vya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

lengo la baraza hilo ni kupitia bajeti ya Mamlaka ya mwaka 2022/2023 na kufanya tathmini ya utendaji wa Mamlaka. Hii itasaidia kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.

Dk.Kijazi amsema kuwa Mamlaka imehakikisha viwango na taratibu za kimataifa za utoaji wa huduma za hali ya hewa pamoja na usimikaji wa vifaa na mitambo vinazingatiwa.

“Kuidhinishwa kwa Muundo wa Taasisi na Miundo ya Maendeleo ya Watumishi (Schemes of Services). Muundo wa Mishahara bado unaendelea kufanyiwa kazi,” amesema.

Pia, kuendelea na taratibu za ununuzi wa Rada nne  za hali ya hewa zitakazofungwa katika Mikoa ya Mbeya, Kigoma, Dodoma na Kilimanjaro.

“Malipo ya awali yameshafanyika na Rada hizo zinaendelea kutengenezwa huko Marekani.Rada hizo zinatarajiwa kufungwa kati ya mwezi wa Julai, 2022 na Juni, 2023,”amesema.

Amesema kuwa TMA inakabiliana na changamoto ya  maslahi madogo ya watumishi hali inayopelekea wataalamu kuhamia katika Taasisi zingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *