MAELEZO YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS – TAMISEMI KUHUSU HOJA ZA WAHESHIMIWA WABUNGE ZILIZOJITOKEZA WAKATI WA KUJADILI HOTUBA YA BAJETI YA OFISI YA RAIS-TAMISEMI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23

1.     Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu, kutuwezesha kufikia hatua hii ya kuhitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.

2.         Mheshimiwa Spika, kipekee ninakupongeza  wewe binafsi, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri uliowezesha Bunge lako Tukufu kujadili bajeti ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa weledi mkubwa. Aidha, ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii na wale ambao hawakupata fursa ya kuchangia kutokana na sababu mbalimbali. Maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge umesaidia kutoa mwelekeo wa kuboresha Mpango na Bajeti  ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

3.         Mheshimiwa Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa ninampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za kuwezesha Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Taasisi zilizo chini yake, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake katika kuhakikisha  huduma bora zinatolewa kwa wananchi.

4.         Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipoishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mheshimiwa Jaffari Abdallah Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la  Mbagala, na Mheshimiwa Denis Lazaro Londo Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Wajumbe wa Kamati na Sekretarieti kwa uchambuzi makini wa  Mafungu 28 ya Bajeti yanayosimamiwa na  Ofisi ya Rais -TAMISEMI. Kimsingi pongezi nyingi ambazo Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepata katika utendaji wake zimetokana na ushirikiano mkubwa Kamati ya USEMI na LAAC Mheshimiwa  Grace Tendega Mwenyekiti na Mheshimiwa Seleman Zedi Makamu Mwenyekiti .

5.         Mheshimiwa Spika, napenda kutambua mchango mkubwa wa Viongozi wenzangu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Kipekee, nawashukuru Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Festo John Dugange, Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe na Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Jimbo la Tunduma na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa Tanzania Bara kwa msaada wanaonipa katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Aidha, namshukuru Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –  TAMISEMI Prof. Riziki Silas Shemdoe na Naibu Makatibu Wakuu . kwa mchango wake katika kufanikisha maandalizi ya Mpango na Bajeti

Ununuzi wa Pikipiki 68 za Maafisa Ustawi wa Jamii

6.         Mheshimiwa Spika; Tarehe 14/04/2022 niliwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais–TAMISEMI kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23. Katika eneo la utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi Rais-TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2021/22, sehemu ya Huduma za Ustawi wa Jamii nilisoma kwamba, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imefanya ununuzi wa Pikipiki 68 aina ya “boxer”zenye thamani ya Shilingi milioni 789.9 kwa ajili ya Maafisa Ustawi wa Jamii’.

7.         Mheshimiwa Spika; Ninaomba kutoa taarifa kwamba, idadi ya pikipiki 68 iliyotajwa kwenye hotuba yangu sio sahihi na hii imetokana na makosa ya kiuandishi. Usahihi ni kwamba pikipiki 68 zimenunuliwa na wadau kwa gharama ya Shilingi milioni 227.50 ambao walikuwa wanatekeleza miradi ya “USAID Kizazi Kipya” katika baadhi ya Halmashauri katika Mikoa 21 ambazo zilinunuliwa na kusambazwa mwezi Septemba, 2021.

8.         Mheshimiwa Spika; kwa lengo la kutosheleza mahitaji ya pikipiki kwa Maafisa Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais-TAMISEMI iliona inunue pikipiki 200aina ya “boxer”. ambazo kwasasa ziko katika hatua ya mwisho ya manunuzi. Pikipiki hizi zinanunuliwa kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19 kwa gharama ya Shilingi milioni 562.40. Pikipiki hizo zitasambazwa kwenye maeneo ambayo hayakupata mgao wa pikipiki 68. Hivyo, jumla ya Pikipiki 268 zitanunuliwakwa gharama ya Shilingi milioni 789.90. Aidha, taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba OR-TAMISEMI imenunua pikipiki moja kwa Shilingi milioni 11 sio sahihi. Taarifa sahihi ni kwamba kila pikipiki kati ya pikipiki 68 ilinunuliwa na mdau wa maendeleo kwa Shilingi milioni 3.34.

9.         Mheshimiwa Spika, Nashukuru Manaibu Mawaziri kwa kutoa ufafanuzi mzuri kwenye kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge zimejikita katika maeneo ambayo napenda kuyatolea ufafanuzi kwa mtiririko ufuatao:-

 1. Miundombinu ya Wafanyabishara Wadogo (Machinga)
 2. Dodoma Machinga Complex Model (Budget 7.1 bilioni, 4.1 bilion Mapato ya Ndani)

10.       Mheshimiwa Spika, katika kuboresha miundombinu ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo (machinga), Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa tija. Hatua ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuwapanga Machinga kwenye maeneo rasmi kwa utulivu pasipo kutumia nguvu katika Halmashauri zote zilizokuwa na machinga wengi kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa. Hatua nyingine iliyochukuliwa ni Serikali kutoa Shilingi bilioni 5.0 kwa ajili ya kuboresha maeneo ya kufanyia biashara machinga katika Halmashauri 11.

11.       Mheshimiwa Spika, Hatua nyingine inayoendelea ni kuwepo kwa majadiliano na Wizara ya Fedha na Mipango ili kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 ili kuruhusu sehemu ya fedha za Mikopo ya asilimia 10 kutumika katika kuboresha miundombinu ya Machinga. Marekebisho ya Sheria hii yanapendekezwa kufanyika kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022. Majadiliano hayo yakikamilika, tunatarajia kiasi cha Shilingi bilioni 38.01 zitapatikana kupitia mlango huo kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Wafanyabiashara Wadogo (Machinga).

12.       Mheshimiwa Spika, chanzo kingine cha mapato kinachotarajiwa ni kupitia asilimia 10 ya fedha zilizotengwa kwenye miradi ya maendeleo za mapato ya ndani ya Halmashauri. Kupitia chanzo hiki, kiasi cha Shilingi bilioni 36.82 kinakadiriwa kupatikana. Mapendekezo ya kutumia asilimia 10 ya fedha za miradi ya maendeleo zinalenga kuhusisha Halmashauri zenye mapato yanayozidi Shilingi bilioni 5 pamoja na Halmashauri nyingine ambazo zimejumuishwa kwenye mpango wa kuboresha maeneo ya machinga.

13.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/23 kupitia vyanzo hivyo, Halmashauri zitakusanya jumla ya Shilingi bilioni 74.83 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya machinga. Aidha, jumla ya fedha itakayotumika katika kuboresha miundombinu hiyo itakuwa Shilingi bilioni 79.83 ikijumuisha Shilingi bilioni 5 ambazo zimekwishatolewa.

14.       Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa kundi hili katika kukuza uchumi, hivyo, ninapenda nitumie fursa hii kuwaelekeza viongozi wote wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha vitendo vya kuwanyanyasa machinga na kutumia nguvu katika kuwaondoa na kuwapanga ikiwemo kuharibu bidhaa zao kama ilivyotokea kwa Jiji la Mwanza vinakomeshwa.

Tangazo la Ajira

15.       Mheshimiwa Spika, Nachukua fursa hii kwa kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa idhini ya ajira za watumishi wa Sekta ya Elimu na Afya 17,412 ambapo nafasi 9,800 ni za walimu na 7,612 ni za kada za afya ambao wataajiriwa katika mwaka huu wa Fedha 2021/22. Naomba kutoa taarifa rasmi kuwa Watanzania wenye sifa wanaelekezwa kuanza kuomba kuanzia leo. Aidha, napenda kuwaelekeza kuwa maombi ya ajira hizi ni bure na yanafanyika kupitia mfumo wa kielektroniki ambao maelekezo yake yatakuwa katika tangazo la ajira. Asilimia tatu (3%) ya ajira hizo ni kuajiri Watu wenye Ulemavu kulingana na Sheria. Aidha, naelekeza Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuhakikisha wanawanunulia watu wenye ulemavu wa Ngozi (Albino)

ii. Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)

16.       Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa. Wajumbe wa Kamati ya USEMI na Waheshimiwa. Wabunge wote kwa pongezi walizotoa kufuatia utekelezaji wa agizo la TARURA kuanza mapema ununuzi wa mikataba ya utekelezaji wa miradi ya barabara. Katika mwaka wa fedha 2022/23, ununuzi wa kazi utaanza mwanzoni mwa mwezi Mei, 2022. Utaratibu huu umetokana na mapendekezo ya Kamati ya USEMI pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako tukufu. ninaagiza Mameneja wa TARURA wa Mikoa na Wilaya wawashirikishe Wadau ikiwa ni pamoja na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuainisha vipaumbele.

17.       Mheshimiwa Spika, ili kuboresha ugawaji wa rasilimali fedha TARURA inafanya mapitio ya formula itakayotumika katika kugawa rasilimali fedha za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara kulingana na hali ya maeneo husika.

18.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI tutapima utendaji kazi wa Mameneja wa TARURA ngazi ya Mikoa na Wilaya

iii. Ufuatiliaji na Tathmini (Uratibu katika ngazi ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri)

19.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika ngazi ya Makao Makuu, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kama ifuatavyo:

Katika kuimarisha usimamizi kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Rais amemteua Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Sekta za Uchumi na Uzalishaji kama ilivyo kwa Sekta za Elimu na Afya. Kuimarisha mifumo ya TEHAMA ambayo inasaidia kazi ya ufuatiliaji wa fedha zinazokusanywa na kupelekwa katika Halmashauri, kufuatilia matumizi ya fedha pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

20.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imeongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa kutoka Shilingi bilioni 57.44 hadi Shilingi bilioni 79.09 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hizo, ikiwemo ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, muundo wa Sekretarieti za Mikoa umehuishwa kwa kuboresha iliyokuwa Seksheni ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa na kuwa Seksheni ya Menejimenti, Ufuatiliaji na Ukaguzi ambayo ina jukumu la ufuatiliaji wa mapato, matumizi na utekelezaji wa miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.  

21.       Mheshimiwa Spika, Katika ngazi ya Halmashauri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kuendelea kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani na Watendaji katika ngazi ya Halmashauri na Kata ili waweze kupata uelewa wa kusimamia ukusanyaji wa mapato na miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.

22.       Mheshimiwa Spika, Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeimarisha mfumo wa kupima utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kutumia viashiria muhimu (KPI) vikiwemo ukusanyaji wa mapato ya ndani, upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo, matumizi sahihi, usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ikiwa ni pamoja na marejesho, usimamizi wa miradi ya maendeleo na uzuiaji na utekelezaji wa hoja za ukaguzi.

23.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya upimaji yatatoa tafsiri ya utendaji wa Viongozi wengine katika ngazi ya Mkoa na Wilaya ambao wana jukumu la kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatimiza majukumu yao. Hivyo, nitoe rai kwa Viongozi wote katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutimiza wajibu wao kwa kuwa utendaji wao utapimwa kwa kutumia viashiria hivyo. Miradi ya Afy na Elimu nje ya ile ya UVIKO-19 ikamilike ifikapo tarehe 30 Mei, 2022. Hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Mikoa simamieni hii deadline.

24.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais – TAMISEMi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imeanza kuboresha Mfumo huu ili uweze kutumika kwa urahisi kwa vituo vyote 5,934 vya Serikali hususan vilivyopo Vijijini, uweze kuunganika na kusomana na mifumo ya kitaifa ili kupata taarifa na takwimu ngazi ya Taifa na kuhakikisha usalama wake. Lengo la Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni kuweka Mfumo huu kwenye vituo vyote ifikapo mwaka wa fedha 2024/25. Kazi hii itafanywa kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo na kusimamiwa na Ofisi za Wakuu wa Mikoa.

iv. Hatua za Kinidhamu kwa Watumishi

25.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais -TAMISEMI katika kusimamia masuala ya nidhamu na maadili ya kazi katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, imekuwa ikichukua hatua za kinidhamu kwa Watumishi wanaokiuka Sheria na taratibu za kazi ikiwa ni pamoja na ubadhirifu, uzembe, ukiukwaji wa maadili ya kazi na taaluma zao.

26.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa fedha 2021/22 OR-TAMISEMI imewasimamisha kazi Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanne (4), imewashusha vyeo Waganga Wakuu wa Mikoa wawili (2), Waganga Wakuu wa Halmashauri 14, Afisa Elimu Mkoa mmoja (1), Maafisa Elimu ngazi ya Wilaya tisa (9), na Wakuu wa Vitengo vya Manunuzi ngazi ya Halmashauri 24.

27.       Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Watumishi wote wa Umma kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma. Aidha, nazielekeza Mamlaka za nidhamu kuhakikisha zinachukua hatua stahiki kwa wale ambao wamebainika kukiuka taratibu. Serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kukiuka taratibu na maadili ya kazi na taaluma zao.

v. Ujenzi wa Vituo vya Afya vya Tarafa na Kata za Kimkakati

28.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais -TAMISEMI inatambua umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika uendelezaji wa miundombinu sambamba na kuiwezesha kutoa huduma za afya kwa kuwa na Vifaa Tiba na watumishi.  Katika kutekeleza hilo Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeweza kufanya tathmini ya uhitaji wa vituo vya afya 428 ambavyo vitajengwa kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ijayo kuanzia Mwaka wa Fedha 2023/24 ambavyo vitajengwa katika Tarafa zisizokuwa na Vituo vya Afya na Kata za kimkakati. Katika mwaka wa Fedha 2022/23 Serikali itatafuta fedha kutoka kwa wadau mbalimbali, bajeti ya Serikali na Halmashauri kutumia Mapato ya Ndani.

vi. Ukarabati wa Shule, Vituo vya Afya na Zahanati Kongwe

29.       Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2015/16 mpaka 2021/22 OR-TAMISEMI imeweza kufanya ukarabati wa Shule Kongwe za Sekandari 89 kati ya shule 92. Kwa mwaka wa fedha 2022/23, OR-TAMISEMI imepanga kufanya ukarabati wa Shule za Msingi Kongwe. Jumla ya shule za msingi zilizoanza kabla ya mwaka 1961 ni shule 2147. Shule hizi zitakarabatiwa kwa awamu baada ya kukamilisha tathmini ya gharama za ukarabati. Ukarabati huu ni endelevu. Katika mwaka wa fedha 2022/23 jumla ya vyumba vya madarasa 1700 vya shule za msingi kongwe ambavyo vimetengewa jumla ya Shilingi bilioni 34 vitakarabatiwa.

30.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Afya ya Msingi kwa mwaka 2022/23 OR-TAMISEMI imepanga kufanya ukarabati wa Hospitali za Halmashauri Kongwe 19 kati ya Hospitali 77 ambapo jumla ya Shilingi bilioni 16.55 zimetengwa. Aidha, ofisi ya Rais TAMISEMI itafanya zoezi la kutambua Vituo vya Afya na Zahanati zilizojengwa kati ya mwaka 1961 hadi1970 ili kuweka mkakati wa kuvikarabati

vii. Ukamilishaji wa Miradi iliyoanzishwa na Kutokamilika

31.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais -TAMISEMI inakubaliana na hoja za Waheshimiwa Wabunge za kuwepo kwa miradi iliyoanzishwa miaka ya nyuma na bado haijakamilika. Ninapenda kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya kina kuhusu miradi na gharama zake za ukamilishaji ili Ofisi ya Rais TAMISEMI iweze kuitambua miradi hiyo na kuweka mikakati ya ukamilishaji. Taarifa hiyo iwasilishwe kabla ya Tarehe 30 Juni, 2022.

viii. Vifaa na Vifaa Tiba

32.       Mheshimiwa Spika, nakubaliana na hoja za Waheshimiwa Wabunge kuhusu ukosefu wa Vifaa na Vifaa tiba katika vituo vya afya vilivyokamilika kujengwa. Kuanzia Mwaka wa Fedha 2018/19 hadi mwaka 2021/22 Serikali imetoa kiasi cha Shilingi bilioni 82.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba katika ngazi ya afya msingi, ambapo Shilingi bilioni 15 zimetumika kununua vifaa na vifaa tiba na kuvisambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha, vifaa vingine manunuzi yake yanaendelea. Vifaa hivi vinajumuisha Vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya utoaji wa huduma za upasuaji na huduma za Mionzi. Aidha, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2022/23 imetenga Shilingi bilioni 47.70 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye Vituo vya Afya 159. Ofisi ya Rais TAMISEMI inafuatilia Vifaa na Vifaa tiba ambavyo tayari vimeshalipiwa fedha kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kuondoa changamoto ya Vituo vya Afya vilivyokamilika na kukosa huduma hiyo.

Motisha kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa

Kuimarisha Makusanyo ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri

33.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaendelea kuzisimamia Halmashauri ili ziongeze wigo wa ukusanyaji wa Mapato ya ndani. Mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuwajengea uwezo maafisa wanaokusanya mapato, kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato na utambuzi wa fursa na uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato. Aidha, utendaji wa Halmashauri utapimwa kwa kuzingatia upelekaji wa asilimia 40/60 na 70 kwa  Halmashauri chache zenye Makusanyo  Makubwa zinazotokana na makusanyo ya mapato ya ndani yasiyolindwa katika miradi ya maendeleo, utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, na urejeshaji wa mikopo na ujibuji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ili kuleta tija na kuimarisha utoaji wa huduma.   

34.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Halmashauri ziliidhinishwa kukusanya Shilingi bilioni 863.85 kutoka katika vyanzo vya Mapato ya Ndani. Hadi Februari, 2022 zimekusanywa Shilingi biliioni 586.07 sawa na asilimia 68.  Fedha zilizoiidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Shilingi bilioni 331.08, hadi Februari 2022 Shilingi bilioni 216.11 sawa na asilimia 65.27. Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kusimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapelekwa kwa wakati katika miradi husika.

USIMAMIZI WA MASHINE ZA KUKUSANYA MAPATO ( POS)  NA KUONGEZA MAPATO YA NDANI YA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

35.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais – TAMISEMI katika Mwaka wa Fedha 2022/23 imepanga kuongeza mapato ya ndani ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa kufika Shilingi Trilioni 1.01 sawa na ongezeko la asilimia 17.18. Mafanikio haya yatafikiwa kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake, kufanya ufuatiliaji mara kwa mara, fedha zote zinazokusanywa kuingizwa benki kabla ya matumizi, vyanzo vyote kuwa na PoS katika kukusanya mapato, kufanya tathmini ya wadaiwa na kuweka mikakati ya kukusanya madeni hayo, na matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki ikiwemo LGRCIS/TAUSI na GoTHOMIS katika vituo vya kutoa huduma za afya.

36.       Mheshimiwa Spika, matumizi sahihi ya Mashine za kukusanya mapato (PoS) ni muhimu, hivyo ninaelekeza kila Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya yafuatayo:-

 1. Kuhakikisha PoS zote hasa zile za zamani kabla ya Mwaka 2019, zinawekewa toleo jipya la APK Toleo la 4.9.9.6.49 ili kuondoa mianya ya kupoteza mapato.
 2. Kufanyika kwa ukaguzi wa PoS  kila mwezi ili kubaini PoS zipo ngapi, zipo wapi, ngapi zipo online na ni nani wanazotumia.
 3. Kuhakikisha POS zote ambazo haziko hewani (offline) kutokana na ubovu au kutojulikana zilipo zinafifishwa kwenye Mfumo (deactivate).
 4. Kufanya “Job rotation”, kuzungusha wanaosimamia ecosystem nzima ya ukusanyaji wa Mapato (ICTO, Wahasibu na wengine).
 5. Kuhakikisha mapungufu ya POS kwenye maeneo ya ukusanyaji yanabainika na mkakati wa kununua POS unawekwa kukidhi mapungufu hayo ili kuongeza mapato.
 6. Kuhakikisha rejista zote za POS zinahuishwa kuendana na taarifa za mfumo kwa usahihi.
 7. Kutoa hamasa ya kudai risiti kwa kila huduma kutoka kwa mkusanya mapato

27.       Mheshimiwa Spika, Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI inahuisha Mfumo wa ukusanyaji wa mapato (LGRCIS/TAUSI) ambao utafanya yafuatayo:-

 1. Usimamizi wa PoS (POS management)
 2. Usimamizi wa Float ili kuondoa matumizi ya fedha mbichi na kuondoa madeni (Float Management)
 3. Kuhamasisha malipo ya kodi, tozo na ushuri kwa kielektroniki bila kufika ofisi za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Online payment – cashless),
 4. Kujifanyia tathmini ya kiasi mlipaji anachopaswa kulipa (Online assessment)
 5. Kutoa leseni na vibali vya kielektroniki (Digital Licence and Permit)
 6. Kuunganisha Mfumo na Mifumo ya TRA kupata mapato ghafi ya wafanyabiasha kwa ajili ya kupata kodi halisi ya huduma (service levy)

38.       Mheshimiwa Spika, Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Mamlaka ya Serikali Mtandao inaendelea kuboresha mfumo wa GoTHOMIS ili uweze kutumika na vituo vyote vya kutoa huduma za afya vya ngazi ya msingi haswa maeneo ya vijijini. Maboresho yatazingatia maelekezo yaliyotolewa na Mhe Rais kuhusu kuimarisha mifumo ili izungumze. Mfumo huu unasaidia kusimamia na kudhibiti madawa na vifaa tiba, kutoa taarifa ya magonjwa na ugonjwa na kusimamia mapato yatokanayo na uchangiaji wa huduma. Mfumo kwa sasa upo kwenye vituo 1,161 na utawekwa kwenye vituo vyote vya afya ifikapo Mwaka wa Fedha 2015/16,

SERIKALI ITOE WARAKA MPYA WA POSHO ZA MADIWANI

39.       Mheshimiwa Spika, Waziri mwenye Dhamana na Serikali za Mitaa alishatoa Waraka wenye Kumb. Na. 215/443/01/50 wa tarehe 23/12/2014 juu ya posho za mwezi za Madiwani. Aidha, Posho za vikao za Waheshimiwa Madiwani zimeelekezwa katika waraka Kumb. Namba CHB/443/01 wa tarehe 26/11/2007 na kusisitizwa katika waraka Kumb. Na PM/P/1/567/59 wa terehe 16/08/2012 ambapo ni shilingi 40,000. Hivyo, posho za Waheshimiwa Madiwani si hisani ya Mkurugenzi wa Halmashauri. Kwa sasa Serikali inaandaa Mwogozo juu ya utaratibu wa ulipaji wa Posho za Vikao kwa Madiwani ambao utapaswa kutumika kwa Halmashauri zote.

KUHUSU KAMATI YA FEDHA PEKEYAKE KUKAGUA MIRADI KATIKA HALMASHAURI

40.       Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 77(5-6) ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri inaeleza kuwa “Kamati za Kudumu za Halmashauri, zinaweza kutembelea miradi ya maendeleo au shughuli yoyote inayotekelezwa na au kwa niaba ya Halmashauri na ambayo inaihusu Kamati husika ’’Kanuni ya 77(1-4) ya kanuni za kudumu za Halmashauri inaelekeza Madiwani kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika meneo yao.

Hatahivyo, Katika Halmashauri nyingi Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango ndio imebeba jukumu hilo pekeyake kitu ambacho ni kinyume na Kanuni za Kudumu za Halmashauri. 

Changamoto Mikopo ya Asilimia 10

41.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI inatambua changamoto ambazo zimejitokeza katika usimamizi wa Mikopo ya asilimia 10 Hapa tayari tumefanya tathmini hadi Machi, 2022 na maoni na ushauri wa Kamati ya USEMI na michango ya Wabunge itasaidia usimamizi thabiti ikiwemo utumiaji mfumo wa Kielektroniki

iv. Ukamilishaji wa Miradi iliyoanzishwa na Kutokamilika

42.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais -TAMISEMI inakubaliana na hoja za Waheshimiwa Wabunge za kuwepo kwa miradi iliyoanzishwa miaka ya nyuma na bado haijakamilika. Ninapenda kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya kina kuhusu miradi na gharama zake za ukamilishaji ili Ofisi ya Rais TAMISEMI iweze kuitambua miradi hiyo na kuweka mikakati ya ukamilishaji. Taarifa hiyo iwasilishwe kabla ya Tarehe 30 Juni, 2022.

Mamlaka ya Miji Midogo

43.       Mheshimiwa Spika, kuhusu namna bora ya kushughulikia Mamlaka ya Miji Midogo ili kubaini ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yake, Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaunda timu kwa ajili ya kufanya tathmini kuhusu uendeshaji na ufanisi wa Mamlaka ya Miji Midogo.

SUALA KUHUSU MSHITIRI

44.       Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nimshukuru Mheshimiwa Stanslaus Nyongo kwa jinsi anavyofuatilia suala la uapatikanaji wa dawa na kupelekea kupatikana kwa taarifa hii muhimu. Kwa kuwa usimamizi wa dawa na vitendanishi ni kipaumbele cha OR TAMISEMI, taarifa hii tumeichukua kwa umuhimu mkubwa na nikuhakikishie kwamba tutaifuatilia kwa umakini mkubwa. Aidha, OR TAMISEMi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kuendelea kuimarisha mfumo wa Prime Vendor System (Mshitiri) ili kuhakikisha inakomesha upotevu na wizi wa dawa na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma ngazi ya Msingi. 

MAOMBI YA FEDHA

45.       Mheshimiwa Spika, sasa naomba Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 jumla ya Shilingi Trilioni Nane Bilioni Mia Saba Sabini na Tisa Milioni Mia Nane Thelathini na Nane na Mia Saba Sitini na Tatu Elfu na Mia Mbili (Shilingi 8,779,838,763,200.00) kwa ajili ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI Fungu 56, Tume ya Utumishi wa Walimu Fungu Na. 2 na Mafungu 26 ya Mikoa yanayojumuisha Halmashauri 184.

 • Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *