JESHI LA POLISI DODOMA LAWATIA MBARONI WANAUME WATATU KWA KUMILIKI SILAHA KIHARAMU,
WANANCHI WAPEWA TAHADHARI SIKUKUU YA PASAKA

Na Emmanuel Charles

Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma limeendelea kufanya doria na kufanikiwa kukamata silaha 2 za moto zinazomilikiwa bila vibali ambazo ni aina ya Short gun yenye namba 86387 na gobole lisilo na namba na vipande vitano vya nondo yenye muundo wa duara, ganda moja la risasi aina ya shortgun na kopo lenye unga udhaniwao kuwa ni baruti.
Akitoa Taarifa kwa Vyombo vya Habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP Onesmo Lyanga ameeleza kuwa Wanaume watatu wamekamatwa Kijiji cha Ndogowe, Tarafa ya Mpwayungu Wilayani Chamwino, Dodoma wenye umri wa miaka 35, 45 na 60 ambao mpaka sasa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na taratibu zinaendelea kuwapeleka mahakamani.
Lyanga alisema, Silaha hizo zimegundulika hazina utaratibu wa kisheria
“Katika hilo niwaonye wananchi inawezekana silaha hizi walikuwa nazo kwa nia njema lakini sasa kwa kutokufuata utaratibu ni lazima tuwashughulikie.nawaomba wananchi waendelee kutii sheria bila shuruti”

Pia Jeshi la Polisi Dodoma limetoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kuelekea Sikukuu ya Pasaka kutokuacha makazi yao bila uangalizi ili kuepuka uhalifu

Kamanda Lyanga ameagiza Kamati za ulinzi na Viongozi wa Dini kuhakikisha usalama katika maeneo ya Ibada na kuimarisha umakini

RPC Lyanga amesema jukumu la Jeshi la Polisi katika sherehe hizi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ni kuhakikisha sherehe inasherehekewa kwa utulivu na amani
“Itatokana na sisi jeshi la polisi kuimarisha usalama wa wananchi kwa kufanya doria za mitandaoni, kutumia mbwa, farasi, pikipiki mifuu na magari hivyo wasiwe na hofu watakapotuona na watoe ushirikiano pale ambapo panakuwa na viashiria vya uhalifu”
Kamanda amewataka wananchi kuacha tamaa na kutumia vilevi kupitiliza na pia kuacha kuendesha vyombo vya moto wakiwa katika ulevi

Aidha, Amepiga marufuku Disko toto kwa kipindi hiki kwa lengo la kuwalinda usalama watoto huku akisema watoto watakaoenda kwenhe maeneo ya sherehe waongozwe na wazazi wao

Aliongeza kuwa, Jeshi halitasita kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaovunja sheria.

Kwa upande mwingine amesema Mkoa wa Dodoma unaendelea kuwa shwari na hali ya usalama imeimarika.
“Wananchi waendelee kufurahia na kufanya shughuli zao katika mazingira yaliyo salama”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *