SPIKA DKT. TULIA ATOA AHADI YA KUIBADILISHA MBEYA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), ameahidi kuacha historia katika Jimbo hilo kwa kuboresha miundombinu ya elimu ambayo imekuwa changamoto kwa muda mrefu.

Dkt. Tulia ametoa ahadi hiyo leo Aprili 14, 2022 wakati wa hafla ya
utoaji tuzo za elimu kwa Walimu, Wanafunzi na Shule za msingi na sekondari zilizofanya vizuri kwa mwaka 2021 katika Jiji hilo ambazo zinaratibiwa na taasisi ya Tulia Trust kila mwaka.

“Kama Tulia Trust tulikuja na wazo la tuzo hizi ili kuongeza chachu ya maendeleo ya elimu katika Jiji letu hili la Mbeya na kuanzia mwakani tutaanza kuzitoa kimkoa kwa maana ya kushindanisha shule zote za Mkoa wa Mbeya ili kuinua viwango vya elimu yetu”

“Ndugu wananchi wenzangu, nataka niwaambie kwamba nimedhamiria kwa dhati kabisa kuhakikisha nawatumikia kwa nguvu zote kadri Mwenyezi Mungu anavyonijaalia” amesema Dkt. Tulia

Kuhusu changamoto ya madarasa, Dkt. Tulia amewaeleza wananchi kwamba Serikali tayari imeshatoa Bilion 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 92 ya Sekondari katika Jimbo hilo na tayari madarasa yamejengwa.

Aidha, Dkt. Tulia amesema kuwa, Jimbo lake limekuwa na changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu ikiwemo uhaba wa madawati kwa baadhi ya shule ambapo ameahidi kuhakikisha anazimaliza kabisa katika kipindi chake cha uongozi huku akiishukuru Serikali kwa kuunga mkono jitihada za Wananchi.

“Nimeelezwa kuhusu changamoto ya madawati katika baadhi ya shule zetu, niwaambie tu kwamba kwa mwaka huu tunataka kulimaliza kabisa na isiwe hoja tena ndani ya Jimbo letu, itapofika mwakani wakati wa kupeana tuzo hizi basi tutapeana mrejesho wa hili kwamba tumelimaliza” amesisitiza Dkt. Tulia

Amesema kuwa, Wananchi wanapaswa kumshukuru sana Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwawezesha ikiwemo mchango wa shilingi Milioni 400 za ujenzi wa shule ya sekondari Iziwa, Milioni 600 Sekondari ya Itende na nyingine nyingi ambapo amewataka waendelee kumuombea maisha marefu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, DKt. Rashid Chuachua, amemshukuru na kumpongeza Spika Dkt. Tulia kwa namna ambavyo amekuwa akijitoa kwa wananchi wake katika kuhakikisha anawafikishia maendeleo ya haraka ambayo waliyakosa kwa muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *