WAHASIBU TUME YA MADINI WATAKIWA KUENDELEA KUSIMAMIA KWA UFANISI RASILIMALI FEDHA KWENYE UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU

Lengo kuiwezesha Tume ya Madini kuendelea kupata hati safi na kuwezesha ukusanyaji wa maduhuli.

Mkurugenzi wa Huduma za Tume, CPA.William Mtinya amewataka Wahasibu wa Tume nchini kuhakikisha wanasimamia kwa ubunifu wa hali ya juu matumizi ya fedha ili kuhakikisha Tume inaendelea kupata hati safi huku Sekta ya Madini ikiendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Pato la Taifa.

Mtinya ametoa wito huo leo tarehe 11 Aprili, 2022 jijini Dar es Salaam kwenye kikao kilichokutanisha Wahasibu kutoka Tume ya Madini Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa chenye la lengo la kupokea taarifa za fedha na kuanza maandalizi ya taarifa ya pamoja ya fedha kwa mwaka 2021-2022 sambamba na kubadilishana uzoefu na kujifunza mifumo mbalimbali ya usimamizi wa fedha za umma.

“Kutokana na utendaji na usimamizi mzuri kwenye matumizi ya fedha zinazopokelewa Tume ya Madini, Tume imekuwa ikipata hati safi, ni vyema mkaendelea kuwa wabunifu katika kuhakikisha shughuli za Tume ya Madini zinafanyika kwa gharama ndogo na kwa ubora wa hali ya juu,” amesema Mtinya.

Katika hatua nyingine amewataka Wahasibu kuendelea kuwa washauri wazuri wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa hekima na nidhamu ya hali ya juu na kujiepusha na rushwa.

Katika hatua nyingine, amewataka Wahasibu kujiendeleza kielimu ili kuhakikisha wanafanya kazi kulingana na mabadilko ya teknolojia.

Aidha akizungumza kupitia mahojiano maalum, Mtinya ameongeza kuwa ili kuboresha utendaji kazi wa Tume ya Madini, Kurugenzi ya Huduma za Tume imekuwa ikiboresha mazingira ya kazi ikiwa ni pamoja na ununuzi wa magari ambapo mpaka sasa Tume imeshapokea magari 7 kati ya magari 40. Hata hivyo Magari 33 yanatarajiwa kupokelewa Mwishoni mwa Mwezi April, 2022.

Amesema kuwa pia Tume ya Madini inaendelea na mradi wa ujenzi wa Ofisi za Tume ya Madini jijini Dodoma lengo likiwa ni kuweka mazingira mazuri ya watumishi pamoja na wadau wa madini wanaofuata huduma katika ofisi hizo.

Amesisitiza kuwa ili kuhakikisha wachimbaji wa madini wanafanya shughuli zao kwa faida huku Serikali ikipata mapato yake stahiki, Tume ya Madini sambamba na kusogeza huduma kwa wachimbaji kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, imeendelea kuboresha huduma katika masoko 42 ya madini na vituo vya ununuzi 75 vya madini.

Amesema kuwa wananchi wengi wanaoishi karibu na migodi wamehamasishwa kupitia kanuni za ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini ambapo kwa sasa wameanza kutoa huduma mbalimbali kwenye migodi ya madini kama vile vyakula, usafiri, ulinzi n.k

Akizungumzia hali ya usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa Madini, Mtinya amefafanua kuwa Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira inaendelea kutoa mafunzo kuhusu usimamizi wa mazingira, afya na baruti kwenye shughuli za uchimbaji wa madini lengo likiwa ni kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini haziathiri mazingira na wananchi wanaoishi katika maeneo ya jirani na kuwa na uchimbaji endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *