WATAALAMU SEKTA YA MAJI SHIRIKISHANENI MAARIFA – NAIBU WAZIRI MAJI

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewataka wataalamu na wadau wa sekta ya maji kwa ujumla kushirikishana ujuzi na taaluma kuweza kutatua changamoto zinazoikumba sekta ya maji kwa pamoja. Amesema Serikali kupitia Wizara ya Maji itahakikisha inawapa msaada wa hali na mali ili kuwezesha malengo maalumu ambayo ni pamoja na kumtua mama ndoo ya maji inafikiwa.

Mhandishi Maryprisca ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la kisayansi la maji lililofanyika jijini Dar es salaam leo Aprili 4, 2022. Aidha, Amekipongeza Chuo cha Maji kwa kuandaa kongamano hilo na kuwa msaada mkubwa katika kuwaandaa wataalamu wanaohudumu katika sekta ya maji nchini.

“Uchaguzi wa kauli mbiu ya ‘Usimamizi wa Rasilimali za Maji kwa Huduma Endelevu za Ugavi wa Maji na Usafi wa Mazingira’ katika Kongamano hili imekuwa sambamba na Malengo ya 2025 ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni ‘kuwezesha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wote’. Inafurahisha kujua kuwa Kongamano hili linakuwa ni sehemu ya kushirikishana, na kupeana ujuzi katika taaluma na kuleta utatuzi wa changamoto zinazoikumba sekta ya Maji na nyiginezo.” Amesema Mhandisi Mahundi.

Amewataka Chuo cha Maji waendeleze Kongamano hilo kwa kila mwaka kwani litasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza maarifa na kuondoa changamoto zinazoikumba sekta ya maji.

Kongamano la Kisayansi la maji limeandaliwa na Wizara ya Maji kupitia Chuo cha Maji na kuhudhuriwa na mataifa mbalimbali kutoka nje na ndani ya Afrika. Matokeo ya tafiti zaidi ya 60 yanatarajiwa kuwasilishwa, huku washiriki zaidi ya 400 wakitarajia kushiriki kwa siku mbili kuanzia Aprili 4 hadi 5.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akipata maelezo kwenye moja ya mabanda ya maonesho ya wadau walioshiriki katika Kongamano la Kisayansi la maji jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi (wa tano kutoka kulia) katika picha ya pamoja mara baada ya kukagua kazi zinazofanywa na moja ya washiriki kutoka Uholanzi
Mhandisi Mahundi akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jarida la usimamizi wa rasilimali maji, uhandisi, menejimenti na sera. Jarida hilo linalenga kuboresha taarifa na kuweka jukwaa la wadau na wataaluma walio katika sekta ya maji kuchapisha kazi zao za kitafiti.
Picha ya pamoja ya Mgeni Rasmi na baadhi ya wajumbe wa kongamano la Kisayansi la maji
Wajumbe wakiendelea na kongamano katika ukumbi wa JKulius Nyerere jijini Dar es Salaam

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *