MILEMBE YAPOKEA WAGONJWA WA AKILI ZAIDI YA MIA TANO, NDUGU WAWATELEKEZA

Na. Emmanuel Charles
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM Tawi la Chuo cha Mipango Dodoma wametembelea Hospital ya Taifa ya Afya ya Magonjwa ya Akili Milembe na kuwapatia Mahitaji mbalimbali
Tukio hilo limefanyika leo April 02, 2022 Hospitalini hapo Jijini Dodoma ambapo Wanafunzi hao kupitia Idara ya Binti CCM Wamefika na kuwaona wagonjwa, mazingira na kutoa mahitaji ikiwemo mchele, sukari, mafuta, sabuni na vinginevyo

Wakizungumza baada ya kufanyika kwa Zoezi hilo Viongozi na Washiriki mbalimbali waliweza kueleza namna walivyoguswa
Mwenyekiti wa Tawi la CCM Chuo cha Mipango Ndugu. Thabit Ahmed aliwashukuru Viongozi wa Hospital ya Milembe kwa ushirikiano waliouonesha kwao
Alieleza kuwa lengo ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mwenyekiti wa Chama hicho Rais Samia Suluhu Hassan
“Tunaipongeza Serikali na tunatoa wito kwa vijana wengine kufanya kama tulivyofanya sisi hapa”
Akielezea maana ya Binti CCM Mwenyekiti alisema ni Idara iliyopo ndani ya Tawi ikiwa na lengo la kuwainua mabinti wa Chama hicho.

Kwa upande wake Rosemary Joseph ambaye ni Mratibu wa UVCCM Chuo cha Mipango alisema wameamua kufanya hivyo baada ya kuguswa huku jamii ikiwasahau watu wenye changamoto ya Afya ya Akili na kuwanyanyapaa
“Sisi tumeamua kuwa Chanzo baada ya kuona watu hawa wanatengwa na jamii nyingi na tumewaona hakika wanapata huduma nzuri na wengi wameshaanza kujitambua na tumezungumza nao Vizuri tu”

Naye Fatma Mfaume kutoka idara ya Binti CCM, alisema kuwa
“tuliwahi kuja mara ya kwanza kama chama, baada ya hapo tukaguswa na ndipo tukawashawishi na wenzetu hadi kuamua kuja kuwatembelea leo”

Kwa upande wake Janeth Emmanuel ambaye ni Mwanafunzi kutoka Chuo cha Mipango, Alieleza kuwa amejifunza wao ni watu kama binadamu wengine na kusihi watu kuendelea kwenda kuwaunga mkono na kuwa pamoja nao kama sehemu ya kuwafariji

Aidha, Zuhura Mohammed yeye alisema watakwenda kuwa mabalozi wazuri kuhakikisha wanakwenda kuwahamasisha watu mbalimbali ili kuwasapoti Wagonjwa wenye changamoto ya Afya ya Akili


Pia, Katibu wa Hamasa CCM Mipango Bwana Japhet Masota alipongeza kwa Hatua hiyo
“CCM inafanya kazi kubwa katika kuwahudumia wananchi wake na katika Sekta ya Afya Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele, na mojawapo ni hapa Hospitali ya Milembe”

Halikadhalika, Katibu wa Idara ya Itifaki CCM mipango Ndugu Jamal Adam aliongeza kuwa jambo lililofanywa ni mfano wa kuigwa kwa Watanzania wote
“Tukio lililofanyika ni ishara tosha kwamba tunapaswa kuwa mfano na niwashukuru sana Vyombo vya Habari kwa kuendelea kuguswa na kuwahabarisha watanzania mambo yanayotokea katika jamii”

Akitoa neno la Shukrani Katibu wa Afya Hospital ya Taifa ya Milembe Dodoma Dkt. Jackson Mjinja aliwashukuru Mabinti CCM kwa kuja na mpango huo
Alieleza kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo Ndugu wa Wagonjwa kuwatenga na kuiachia mzigo serikali
“Hospital imekuwa ikiwahudumia baadhi ya wagonjwa ambao jamii zao zimewakataa baada ya kufanya matukio ya uhalifu, na wengine ndugu zao wakishawaleta hata tukiwaambia wagonjwa wao wamepona waje kuwachukua basi wanakuzimia kabisa simu”


Alisema kutokana na changamoto hizo wamekuwa wakiwasiliana na Idara ya ustawi wa jamii juu ya ndugu ambao wanawanyanyapaa wagonjwa wao
Aliitaka jamii kuachana na kuwahusisha wagonjwa hao na imani za kishirikina na kuwapeleka kwa Waganga wa kienyeji
“Hospitali yetu ina wagonjwa zaidi ya mia tano ambao tunaendelea kuwahudumia ili kuwarejesha katika hali ya kawaida, niwaombe watu waje watibiwe hapa kwani huduma zetu ni Bora na gharama zake ni nafuu.Ukiachana na Ugonjwa wa Afya ya Akili tunatoa huduma za magonjwa mengine pia”
Dkt. Mjinja aliwataka wanajamii kuacha kuwatenga wagonjwa hao na kuacha kutumia lugha ngumu kwa kuwaita Vichaa badala ya Kuwaita watu wenye changamoto ya Afya ya Akili.

PICHA KATIKA MATUKIO MBALIMBALI

PICHA ZOTE NA UHONDO TV

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *