MAKAMU WA RAIS AZINDUA MBIO ZA MWENGE 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 2 Aprili 2022 amezindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 , halfla iliofanyika katika uwanja wa sabasaba mkoani Njombe.

Akizungumza kabla ya uzinduzi wa mbio hizo, Makamu wa Rais amewataka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia na Rushwa (TAKUKURU) kukamilisha uchunguzi wa miradi 52 iliyotiliwa shaka wakati wa mbio za Mwenge za Mwaka 2021 na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani haraka iwezekanavyo endapo kutakua na ushahidi wa kutosha.

Aidha Makamu wa Rais amewataka wakimbiza mwenge kwa mwaka 2022 kuhakikisha wanajiridhisha endapo miradi watakayotakiwa kuizindua inalingana na thamani ya fedha iliyotumika, amewataka kufanya uchunguzi endapo watatilia shaka na hatua za sheria zichukuliwe.

Kuhusu suala la Sensa, Dkt Mpango, amewaelekeza viongozi wote na waratibu wa zoezi hilo kuwaandaa wananchi ili waweze kushiriki zoezi la Sensa kikamilifu. Halikadhalika amewaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa dini na Viongozi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kuwaelimisha na kuhamasisha wafuasi au wanachama wao kuhesabiwa.

Makamu wa Rais ametumia hadhara hiyo kuwasisitizia wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi, ugonjwa wa malaria pamoja na kuzingatia masuala ya lishe kwa maendeleo ya afya zao na uchumi kwa ujumla. Kuhusu suala la mazingira Dkt. Mpango amesema hali ya uhifadhi wa mazingira nchini bado si yakuridhisha hivyo kazi ya kuhifadhi mazingira ikiwemo kulinda vyanzo vya maji, misitu, upandaji miti, kupendezesha miji yetu na kufanya usafi ni lazima ziwe za kudumu.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa tangu kuhasisiwa kwa Mbio za Mwenge, zimeendelea kudumisha uhuru, amani, mshikamano, uzalendo na umoja wa kitaifa. Aidha amesema mbio za mwenge zimekuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo – Zanzibar Mheshimiwa Tabia Maulid Mwita, amesema kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na MIchezo, itahakikisha kuwa mambo yote yaliyopangwa kwa ajili ya maslahi ya vijana yanatekelezwa.

Ujumbe mkuu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 umelenga Sensa ya Watu na Makazi chini ya Kaulimbiu isemayo, “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa tuyafikie Maendeleo ya Taifa.”

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Mwenge wa Uhuru kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa kwa mwaka 2022, Tahili Nyandabara mara baada ya kuuwasha na kuzindua mbio hizo,hafla iliofanyika katika uwanja wa Sabasaba Mkoani Njombe leo tarehe 2 Aprili 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwasha Mwenge wa Uhuru wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge kwa mwaka 2022, hafla iliofanyika katika uwanja wa sabasaba uliopo mkoani Njombe leo tarehe 2 Aprili 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 2 April 2022 akiwasili katika uwanja wa Sabasaba uliopo Mkoani Njombe kwaajili ya kuzindua mbio za Mwenge kwa mwaka 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia hadhara iliojitokeza katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022, hafla iliofanyika katika uwanja wa Sabasaba uliopo Mkoani Njombe leo tarehe 2 April 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *