Serikali kwa kushirikiana na Benki ya KfW kwa niaba ya Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund – GCF) inatekeleza mradi wa kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabia nchi katika Wilaya tano (5) za Mkoa wa Simiyu ambazo ni Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu. Katika awamu ya kwanza mradi wa maji utatekelezwa katika Wilaya za Busega, Itilima na Bariadi.
Akizungumza na Kamati ya Wataamu wa Sekta mtambuka, jijini Dodoma Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandishi Anthony Sanga amesema maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi zinakwenda vizuri na kwamba wako katika hatua za mwisho za kuanza utekelezaji.
Mradi huo unakadiriwa kugharimu jumla ya kiasi cha EURO Milioni 171, ambapo GCF watachangia EURO Milioni 102.7, Benki ya KfW itachangia EURO Milioni 26.1, Serikali ya Tanzania EURO Milioni 40.7 na Wananchi kupitia nguvu zao watachangia EURO Milioni 1.5. Hadi mwezi Februari 2022, awamu ya kwanza ya fidia kiasi cha shilingi 1,519,074,522.16 kimelipwa kwa wananchi wapatao 1,201 kati ya 1,308 walio tathiminiwa. Aidha, taratibu za kuwapata wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa mradi zipo katika hatua za mwisho.



