NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewataka Waratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) Mkoa wa Mwanza kusimamia kwa uadilifu miradi 104 yenye thamani ya Sh Bilioni 7.8 itakayotekelezwa ndani ya Mkoa huo.
Ndejembi ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza wakati alipokua akizungumza na watendaji wa TASAF Mkoa huo ambapo aliwataka kusimamia miradi hiyo kwa uzalendo huku pia akiwataka Waratibu hao kuwashirikisha viongozi wa Wilaya na Mkoa kwenye kila mradi unaotekelezwa na TASAF.
“Ndugu zangu Rais Samia ametoa Sh Bilioni 7.8 kwenye Mkoa huu pekee kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 104 ambayo imepitishwa na Wizara. Miradi 31 ya Afya, Miradi 49 ya Elimu na Miradi 24 ni ya kutoa ajira za muda.
Miradi Hii itatekelezwa kwenye Halmashauri zote nane za Mwanza, hakikisheni inakamilika kwa wakati na thamani ya fedha ionekane, kama kuna mtu anafikiria hizo fedha ajue zitamtokea puani, hatutoruhusu ubadhirifu wowote utokee na TAKUKURU niwatake muwe macho kwenye ujenzi wa miradi Hii yote,” Amesema Ndejembi.
Naibu Waziri Ndejembi pia amewataka Waratibu hao kuwashirikisha viongozi wengine juu ya utekelezaji wa miradi hiyo ili waweze kuifahamu na kuifanyia ufuatiliaji pindi inapokua inatekelezwa.
