
Mhe. Mchengerwa atembelea Wasafi, awapongeza kwa vipindi bora vya Michezo na Burudani
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa @mmchengerwa ameupongeza uongozi wa kampuni ya Wasafi inayomiliki Wasafi TV na Wasafi FM redio kwa kazi nzuri ya kuibua vipaji na kutoa ajira nchini.
Mhe. Waziri ametoa pongezi hizo leo Machi 25 baada ya kutembelea na kukagua shughuli na vipindi mbalimbali vya michezo na burudani vinavyotolewa na vituo hivyo.
Akimtembeza katika Idara mbalimbali za vituo hivyo mmiliki wa Wasafi na Msanii maarufu ndani na nje ya Bara la Afrika Nasibu Abdul maarufu Diamond Platinumz amesema vituo vyake vinajitahidi kwenda na teknolojia ya kisasa katika kuendesha vipindi vyenye maudhui ya kuelimisha na kuburudisha jamii.
Aidha, amesema vituo vyake vinazingatia kuchuja taarifa ili zizingatie maadili ya mtanzania katika vipindi vyote ikiwa ni pamoja na vipindi vya miziki na michezo.
Mkurugenzi wa vipindi wa Wasafi Nelson Kisanga amesema Wasafi FM imekuwa na vipindi maarufu vya michezo vya Sports Arena na Sports court ambavyo vimekuwa na wasikilizaji wengi.
Diamond ametumia muda huo kumshukuru Mhe. Mchengerwa kwa mapinduzi makubwa yanayofanywa na Serikali kupitia Wizara yake.